Writen by
sadataley
9:08 AM
-
0
Comments

Na Stephen Maina
Katika utamaduni wa Mwafrika mtoto ni kiungo muhimu katika familia.Ndoa ambayo haina mtoto huonekana imepwaya na hata upendo hupungua na hata kutoweka baina ya wanandoa.
Mara nyingi anayelaumiwa kwa kukosa mtoto ni mwanamke kuwa hajazaa, lakini mara nyingine mwanamume pia anaweza kuwa na dosari za kiafya.
Ndiyo maana tunashauri kuwa kabla vijana wapendanao hawajaamua kufunga ndoa, waende kwanza hospitali wapimwe siyo tu kama wameambukizwa Ukimwi bali pia kama mbegu za mvulana na mayai ya msichana yako sawa.
Mtoto anapozaliwa na kukua hupewa huduma zote muhimu kama chakula, mavazi, maji,makazi na upendo wa hali ya juu. Kitu ambacho hapewi ni uhuru a kujiamulia anachotaka.
Mtoto hashirikishwi katika kuamua atakula nini, atavaa nini na atalala wapi. Wazazi wake kufanya uamuzi kwa niaba yake.
Nakumbuka baada ya kumaliza darasa la nane na kufaulu mtihani wa ‘Standard Eight Territorial Examination’ nilifanikiwa kuchaguliwa kwenda Seminari ya St James Kilema Moshi, Chuo cha Ualimu Singachini Moshi Shule na shule ya Sekondari Umbwe.
Wazazi wangu ndio walioamua niende shule ipi ili niendelee na masomo ya juu zaidi. Kimyomoyo nilitaka kwenda seminari kusomea uchungaji lakini wazazi walinikataza kinyume cha mawazo na matamanio yangu.
Najutia uamuzi wao hadi leo. Kwani hawakunishirikisha kutoa mawazo yangu.
Katika kipindi hiki cha ukweli na uwazi, watoto wanatakiwa wapewe fursa ya kushirikishwa kuhusu mambo yanayowahusu na kujieleza bila woga na wala siyo kuwatumia mama zao kuwasemea kwa baba wanapokuwa na matatizo.
Baba na mtoto wawe karibu na wawe wawazi na wakweli. Mtoto ajengwe kusema ukweli kwa kujiamini hata kama kufanya hivyo kutasababisha adhabu.
Watoto katika familia wanatakiwa wakisema wasikike na wasikilizwe. Maana yake ni kwamba watoto wawe huru kujieleza na kutoa madukuduku yao bila woga.
Wazazi wa kisasa waliopata elimu ya kizungu wameiga uzungu katika malezi ya watoto wao na wakati mwingine wamevuka mpaka.
Kwa mfano, mtoto ananunuliwa kitu na bila woga anakikataa na kusema hakitaki. Mzazi naye anashindwa kumwelimisha juu ya manufaa ya kitu hicho. Hatimaye mzazi anakubaliana na matakwa ya mtoto.
Hali hii inapojitokeza tunalalamika na kusema kuwa watoto wa siku hizi wana kiburi, kumbe sisi ndio chanzo cha kiburi hicho.
Niliwahi kusema hapo siku za nyuma kuwa kuwe na uwiano kwa malezi ya watoto. Tusiwe wakali kiasi cha kuogopwa na watoto lakini pia tusiwe wapole kiasi cha mtoto kufanya anavyotaka.
Huko Ulaya kuna wakati mtoto alimpeleka mzazi wake kwenye kituo cha polisi eti anapiga kelele na kumzuia mtoto kusoma kwa utulivu. Ukweli ni kuwa mzazi alikuwa na wageni na walikuwa wakicheka mara kwa mara.
Ukweli ni kuwa wazazi wa sasa wako njia panda au kwa maneno mengine wako kama popo, ambaye siyo mnyama wala ndege.
Wakati umefika kwa Serikali kutayarisha sera ya malezi ili kuwe na mahali pa marejeo. Sera ya aina hii itawawezesha wazazi, walezi, walimu na viongozi wengine katika vyombo vya dola kufahamu wajibu wao katika jamii.
No comments
Post a Comment