Writen by
sadataley
6:12 AM
-
0
Comments
Zanzibar. Mabaraza ya Katiba yaliyosimamiwa na Tume ya Katiba kwa sehemu kubwa yametupa picha ya namna watu walivyokuwa wameyafikiria. Ingawa Tume ilitoa muongozo, wengi hawakuusoma au nisema hawakutaka kuelewa.
Tulichokiishuhudia ni baadhi ya wajumbe kutoka katika vyama vya siasa kushiriki katika mabaraza wakiwa na waraka mfukoni wenye maelekezo ya vyama vyao!
Ni jambo la kushangaza, lakini ndio demokrasia yenu ilipofikia kwamba watu wazima wanashindwa kujenga hoja wenyewe aina ya katiba wanaitakayo, wanasubiri kulishwa maneno kutoka kwa wanasiasa.
Ninaipongeza Tume ya Jaji Warioba kwa kuwa haikuruhusu taratibu na miongozo iliyowekwa na Tume hiyo kuvunjwa kwa makusudi, muda wote walisimama kwenye upande wa haki na pale alipozuka mtu akiwa na “waraka” wenye maelekezo alipigwa ‘stop’, ili aeleze ya kwake.
Siku chache baada ya kuanza kwa mabaraza tulimsikia Jaji Warioba akiwakosoa wajumbe wa mabaraza hayo waliokuwa wakienda na matamko au nyaraka za vyama, badala ya maoni ya wananchi waliowachagua.
Inavyoelekea baadhi ya watu bado wana mawazo kuwa mfumo wa chama dola unaendelea katika nchi yetu na inawezekana mfumo huo umewalemaza baadhi ya watu kiasi cha kuingia woga hata katika yale mambo yenye uhusiano wa maisha ya kila siku.
Bado wanafikiri chama kushika hatamu katika wakati huu wa mfumo wa vyama vingi vya siasa. Wanasahau kuwa Katiba ni mali ya wananchi, na ni wao wenye haki na mamlaka ya kueleza wanataka namna gani nchi yao iongozwe.
Wananchi ndio wenye uamuzi wa mwisho kuamua Katiba yao iweje na wala sio watawala wala vyama vya siasa vinavyoweza kujigeuza au kupora mamlaka na nguvu za wananchi.
Kwa maana hii sera za vyama vya siasa hazina upenyo wa kwenye suala zima la Katiba Mpya maana wananchi wanaweza hata wakasema kwa mfano hawaoni ulazima wa kuwepo kwa vyama vya siasa na badala yake wakapendekeza aina nyingine ya mifumo ya kidemokrasia ambayo inakubalika.
Sisemi kuwa tuachane na vyama vingi, la hasha, isipokuwa ninachora picha kwamba nguvu ya mwisho ya uamuzi katika nchi yeyote ya kidemokrasia ni kwa wananchi wenyewe.
Tunasimama pamoja na Tume ya Jaji Warioba kwa kitendo chao cha ushupavu katika kuona Taifa letu linapata Katiba ambayo inatokana na matakwa ya wananchi badala ya wanasiasa.
Kamwe tusikubali kufanya mambo kwa ajili ya maslahi ya muda mfupi, lazima tutangulize uzalendo kwa ajili ya kupata Katiba bora inayotokana na matakwa ya watu wenyewe na sio kundi fulani.
No comments
Post a Comment