Serikali za Tanzania na Uganda zimeanza mazungumzo maalumu yatakayotoa dira itakayoongoza zoezi la kuhakiki upya alama za mpaka zilizoko kwenye ramani zilizowekwa na wakoloni kwa zaidi ya miaka 100 iliyopita ili kuondoa uwezekano wa kuzuka kwa migogoro ya mipaka.
Hayo yameelezwa na Dkt. Augustine Mahiga ambaye ni waziri wa mambo ya nchi nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, akizungumza na ITV akiwa mkoani Kagera kwa lengo la kuhudhulia mazungumzo hayo huku akiwa ameambatana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tamisem, Naibu waziri wa maji na naibu waziri wa nishati na madini, amesema lengo la kuhakiki alama za mpaka wa nchi hizo ni kuimarisha mahusiano na kupunguza miingiliano isiyo na manufaa.
Akizungumzia juu ya utatuzi wa mgogoro wa mpaka kati ya nchi ya Tanzania na Malawi waziri Mahiga amesema mazungumzo ya kutatua mgogoro huo yanaendelea vizuri na muafaka utapatikana hivi karibuni.
Waziri Mahiga akiwa mkoani Kagera leo amepokea nakala ya hati ya utambulisho toka balozi mteule wa Uganda nchini Tanzania, Richard Kabonelo anayechukua nafasi ya balozi Doroth Hyuka ambaye anamaliza muda wake wakati wa hafla fupi iliyofanyika kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa Kagera na kuhudhiliwa na viongozi mbalimbali za serikali.
No comments
Post a Comment