Rais Donald Trump wa Marekani amesaini kuwa sheria mpango wa vikwazo uliopitishwa na Bunge la Wawakilishi na Seneti ya nchi hiyo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia na Korea Kaskazini.
Duru mbili za Ikulu ya White House zimeripoti kuwa Trump amesaini mswada huo katika hali ya faragha, mbali kabisa na kamera za wapiga picha.
Licha ya kusaini mswada huo, Rais wa Marekani ameeleza kupitia taarifa wasiwasi alionao kuhusu athari hasi zinazoweza kutokea kutokana na mpango huo ikiwemo kupungua mamlaka ya rais ya kuondoa vikwazo dhidi ya Russia na kupungua pia uwezekano wa kupata ushirikiano wa waitifaki wa Washington katika kadhia hiyo.
Kwa kuzingatia kuwa mswada huo ulipitishwa takribani kwa kauli moja katika mabunge yote mawili ya Marekani ya Wawakilishi na Seneti, hakukuwepo na uwezekano wa Trump kuupigia kura ya veto.
Kupungua mamlaka ya rais wa Marekani katika kuondoa vikwazo na kutekeleza vikwazo vipya dhidi ya Russia kumeifanya Ikulu ya White House isiwe na raghaba ya kuusaini mswada huo wa vikwazo.
Mpango wa vikwazo dhidi ya Iran, Russia na Korea Kaskazini ulipitishwa wiki mbili zilizopita na Baraza la Wawakilishi na kisha Seneti ya Marekani.
Mpango huo wa vikwazo umeungwa mkono na wawakilishi wa vyama vyote viwili vya Republicans na Democrats vya nchi hiyo.
Parstoday
No comments:
Post a Comment