““Swali langu ni kamba ni azimio gani lilifuta Baraza la Mapinduzi
ambalo ndicho kilikuwa chombo cha juu? Karume alisema Mapinduzi Daima
bila mapinduzi hakuna Zanzibar,”
Peter Kisumo.
Na Daniel Mjema, MwananchiMoshi. Mwanasiasa wa siku nyingi, Peter Kisumo
amesema Baraza la Mapinduzi Zanzibar aliloliacha Rais wa Kwanza wa
visiwa hivyo, Abeid Aman Karume limeuawa kimyakimya.
Kisumo alisema jana kwamba baada ya miaka 50 ya
Mapinduzi Zanzibar, nafasi ya baraza hilo imechukuliwa na Baraza la
Mawaziri Zanzibar.
Akizungumza kwa simu kutoka wodi ya wagonjwa wa
moyo ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikolazwa, Kisumo alisema:
“Nataka Shein (Rais Dk Ali Mohamed) aniambie kutoka moyoni mwake kama
Baraza la Mapinduzi Zanzibar lingalipo? Kama lipo ni nini mipaka ya
Baraza la Mawaziri Zanzibar?”
Waziri huyo katika Serikali ya Awamu ya Kwanza,
ambaye alirejea nchini wiki mbili zilizopita kutoka India alikokwenda
kwa matibabu ya moyo na figo alisema mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar
1964, Karume alitembelea Tanzania Bara akiwa na Thabit Kombo na
walichagua kutembelea Mkoa wa Kilimanjaro... “Wakati huo nikiwa mkuu wa
mkoa nikawapeleka Usseri, Kituo cha Afya wakati huo kilikuwa sawa na
hospitali. Pale nilimsikia ‘Sisi Wazanzibari tumekubali kuungana na
Tanganyika... Mapinduzi haya Daima, Mapinduzi milele’, hapo ndipo mwanzo
wa kusikia neno Mapinduzi Daima.”
Kisumo alisema anachokiona leo ni mabadiliko kiasi
kwamba Baraza la Mawaziri Zanzibar ndilo limeshika hatamu badala ya
Baraza la Mapinduzi aliloliacha Karume.
“Swali langu ni kwamba ni azimio gani lilifuta
Baraza la Mapinduzi ambalo ndicho kilikuwa chombo cha juu? Karume
alisema Mapinduzi Daima bila mapinduzi hakuna Zanzibar,” alisema Kisumo.
Alielezea kushangazwa kwake na Mwenyekiti wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kutouona uasi huo
uliofanywa kimyakimya wakati akikusanya maoni ya Wazanzibari.
Mara kadhaa, Jaji Warioba amenukuliwa akisema
mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar yaliyofanyika mwaka 2010
yaliyosema Zanzibar ni nchi, yalivunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Mabadiliko hayo yalisema Zanzibar ni nchi ambayo
eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na
visiwa vidogo vilivyozungukwa na bahari yake.
Wakati Katiba ya Zanzibar ikieleza hivyo, Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sura ya 1 inaeleza kuwa Tanzania ni
nchi moja na eneo lake la mipaka ni kuanzia Tanzania Bara hadi Visiwani.
Kifungu cha 2(a) cha Katiba ya Zanzibar kimempa
uwezo Rais wa Zanzibar kuigawa Zanzibar katika mikoa na wilaya kinyume
na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Kisumo amelazwa katika Hospitali ya Muhimbili kwa
siku ya nne jana, akisumbuliwa na maradhi ya moyo pamoja na figo, hata
baada ya kurejea kutoka nchini India kwa matibabu.
No comments:
Post a Comment