Wednesday, April 11, 2018

Yanga ni timu kubwa na Singida ni timu ambayo imekuja sasa hivi


Klabu ya Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga imefunguka na kuanza kujigamba kuwa mchezo wao dhidi ya Singida United leo wameuchukulia kwa umakini mkubwa ili waweze kujipatia ushindi mnono na kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa ikiwa yamebakia masaa machache kuelekea mtanange huo wa kukata na shoka utakaopigwa katika dimba la Taifa majira ya saa 10:00 alasiri kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.

"Yanga ni timu kubwa na Singida ni timu ambayo imekuja sasa hivi na pengine inaweza ikajitutumua nayo kutafuta kupata ukubwa lakini bado ni mapema sana kwao, itawachukua miaka mingi mpaka kuyapata yale ambayo Yanga wameyafanya katika soka la Tanzania mpaka hii leo", amesema Mkwasa.

Pamoja na hayo, Mkwasa ameendelea kwa kusema "kwa hiyo niseme sisi mechi tumeichukulia 'very serious' na tuwaombe tu mashabiki wetu na wapenda burudani wajitokeze kwa wingi kama walivyofanya juzi ili tuweze kupata matokeo mazuri ili tujiweke vizuri katika ligi".

Yanga wanashuka dimbani wakiwa wameshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu kwa alama 46, Azam FC ikiwa nafasi ya tatu kwa alama 45, Tanzania Prisons FC akiwa na alama 37 akikamatia nafasi ya nne, Singida United ikishika nafasi ya tano kwa pointi 36 huku Simba SC ikiwa bado anaendelea kuongoza ligi kwa pointi 52.

No comments:

Post a Comment