Friday, June 6, 2014

Moto kuwaka kikao cha Kamati ya Bajeti


Spika Anne Makinda.PICHA|MAKTABA 
Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Dodoma. Moto wa mjadala wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2014/15 sasa unahamia katika kikao cha ndani cha mashauriano kati ya Serikali na Kamati ya Bunge ya Bajeti kitakachofanyika kwa siku sita.
Kikao hicho kilichoanza jana na kutarajiwa kuendelea hadi Juni 11, kitajadili hoja zenye maslahi kwa taifa zilizotolewa na wabunge wakati wa kujadili bajeti za wizara. Bajeti za wizara zilianza kujadiliwa Mei 5 na kumalizika juzi jioni.
Spika Anne Makinda alitangaza jana kuanza kwa kikao hicho na kufafanua kuwa kitawahusisha pia wenyekiti wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa masuala yanayozihusu kamati zao.
Baadhi ya wizara ambazo wabunge walichachamaa kutaka ziongezewe fedha ni pamoja na Wizara ya Maji, Afya na Ustawi wa Jamii, Ujenzi, Uchukuzi, Kilimo Chakula na Ushirika, Nishati na Madini, Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
“Bajeti ni Sh19 trilioni na katika kikao hicho hakuna fedha itakayoongezeka. Kitakachofanyika ni kupunguza fedha katika eneo fulani na kuipeleka eneo jingine,” alisema Spika Makinda.
Mvutano mkali unatarajiwa kuibuka katika kikao hicho kutokana na wabunge wengi kuibana Serikali wakitaka iongeze fedha kwa baadhi ya wizara katika Bajeti ya 2014/15 na kuhakikisha inaziba upungufu wa fedha katika bajeti za baadhi ya wizara kwa mwaka 2013/14 unaomalizika Juni 30, mwaka huu.
Katika mjadala wa Wizara ya Afya, wabunge wengi, hasa wanawake, waliibana Serikali kushinikiza iongeze fedha ili kukabiliana na vifo vya akina mama na watoto.
Wizara hiyo imetengewa Sh622 bilioni ikiwa ni pungufu ya Sh131 bilioni kwa mwaka 2013/14 ambayo ilikuwa Sh753 bilioni.
Katika majibu yake, Serikali iliahidi kuongeza fedha za wizara hiyo katika kikao hicho cha mashauriano huku ikitangaza kutoa Sh12 bilioni kwa ajili ya kulipia deni la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ambalo ni Sh89 bilioni na deni la matibabu nje ya nchi ambalo ni Sh21 bilioni.
Wizara ya Maji ni kati ya wizara ambazo wabunge walichachamaa wakitaka Serikali iiongezee fedha ili iweze kukamilisha miradi ya maji vijijini. Wizara ya Ujenzi nayo ni miongoni mwa wizara zitakazojadiliwa.

No comments:

Post a Comment