Mbowe, Profesa Lipumba, Mchungaji Mtikila wahutubia.PICHA\MAKTABA
Na Talib Ussi na Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Zanzibar. Viongozi wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), wameapa kuendelea kudai mfumo wa Muungano wa serikali
tatu nje ya Bunge la Katiba kwa nguvu zote, ikiwamo kufanya maandamano
ya amani nchi nzima.
Msimamo huo ulielezwa na viongozi hao kwa nyakati
tofauti katika mkutano wa hadhara uliofurika mashabiki kwenye Viwanja
vya Kibandamaiti, Unguja jana.
Mwenyekiti Ukawa, Freeman Mbowe alisema wameamua
kuliacha Bunge la Katiba kutokana na harufu za rushwa, vitisho na matusi
huku baadhi ya wabunge wakiahidiwa vyeo. Mbowe ambaye hata hivyo
hakufafanua zaidi, alisema Ukawa wameamua kwenda kwa wananchi kuwaeleza
dhamira chafu walionayo wabunge wa CCM katika mpango wao wa kukataa
Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyowasilishwa na Jaji Joseph
Warioba.
“Ni jambo la hatari katika mchakato wa Katiba
wananchi kuwa waoga au hofu... Lazima tuwe tayari kuwaonyesha watawala
kuwa tuna umoja imara, tunayapigania mataifa huru ya Tanganyika na
Zanzibar, Rais Kikwete (Jakaya) asiwatishe wananchi kwa kivuli cha jeshi
kuchukua madaraka,” alisema Mbowe.
Lipumba anena
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim
Lipumba alisema wajumbe wa Ukawa wameamua kujitoa bungeni kutokana na
kauli ya Rais Jakaya Kikwete ambayo alidai kuwa iliibeza na
kuidhalilisha Tume ya Warioba.
Alisema hawatarudi bungeni na kwamba hawawezi kujadili Katiba ambayo siyo maoni ya wananchi.
Alidai kwamba kwa makusudi Rais Kikwete aliamua
kutetea sera za chama chake na kupingana na maoni yaliyotolewa na
wananchi kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Rais Kikwete ameharibu nia ya kupatikana Katiba
Mpya, amekuwa akijulishwa kila hatua na jinsi maoni ya wananchi
walivyokuwa wakipendekeza serikali tatu katika Rasimu ya Kwanza na ya
Pili naye akawa anaafiki, inashangaza amegeuka na kukataa maoni ya
wengi,” alisema Profesa Lipumba.
Mtikila akumbushia jela
Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila
alisema aliwahi kufungwa jela mara tatu, kuwekwa mahabusu mara 43 kwa
kudai lipatikane Taifa la Tanganyika huku watawala wakikataa matakwa ya
wengi kwa sababu na hoja dhaifu.
Mchungaji Mtikila aliongeza kusema kwamba
wanachokitaka CCM na Serikali zake ni kuendelea kuwabana wananchi wa
Tanganyika na Zanzibar wasiweze kuwa huru na kujivunia mataifa yao.
No comments:
Post a Comment