London, England. Atletico Madrid imeitupa Chelsea nje ya
mashindano baada ya kuichapa mabao 3-1 katika mechi ya marudiano ya nusu
fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye Uwanja wa Stamford Bridge na
hivyo kutinga fainali ya mashindano hayo.
Katika mechi ya kwanza iliyozikutanisha timu hizo
wiki mbili zilizopita kwenye Uwanja wa Vicente Calderon mjini Madrid
zilitoka suluhu 0-0.
Kwa ushindi huo, Atletico itacheza fainali dhidi
ya Real Madrid na mechi hiyo ya fainali itapigwa Mei 24 kwenye Uwanja wa
Da Luz mjini Lisbon, Ureno.
Real Madrid walifika fainali baada ya kuichapa
Bayern Munich 4-0 katika mechi ya marudiano ya nusu fainali ya Ligi ya
Mabingwa Ulaya juzi na hivyo kutinga fainali kwa jumla ya mabao 5-0 kwa
sababu katika mechi ya kwanza wiki moja iliyopita walishinda 1-0.
Katika mechi ya jana, Chelsea walitawala mwanzoni
mwa kipindi cha kwanza na kupata bao katika dakika ya 39 ambalo
lilifungwa na Fernando Torres, lakini halikudumu muda mrefu kwani
Atletico walisawazisha bao katika dakika ya 44 mfungaji akiwa Adrian
Lopez.
Kipindi cha pili Atletico walimiliki zaidi mpira
na kufanya mashambulizi katika lango la Chelsea na kupata penalti katika
dakika ya 60 ambayo ilifungwa na Diego Costa baada ya Eto’o kumwangusha
Costa katika eneo la hatari.
Bao hilo liliwatoa Chelsea mchezoni kwani
walijikuta wakifungwa bao zuri la tatu katika dakika ya 72 ambalo
lilifungwa na Arda Turan baada ya wachezaji wa Atletico kupasiana
vizuri.
No comments:
Post a Comment