Ziara hiyo ya Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa inakuja huku majeshi ya
serikali na wapiganaji wa waasi wakiendelea kupambana ili kuudhibiti mji
wenye utajiri wa mafuta wa Bentiu.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema Ban Ki Moon amekuwa mara kwa mara
akiwataka viongozi wa sudan kusini kutafuta suluhisho la kisiasa na
kuyasitisha mapigano ambayo yamewaathiri zaidi raia wasio na hatia.
Ban anatarajiwa kukutana na rais wa Sudan Kusini Salva Kiir katika ziara
hiyo ya siku moja na pia atakutana na viongozi wa jamii
wanaowawakilisha maelfu ya raia wanaojipatia hifadhi katika kambi za
majeshi ya kulinda amani ya umoja wa Mataifa.
Jumuiya ya kimataifa yaongeza juhudi za kuumaliza mzozo
Ziara hiyo ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa inakuja siku chache tu
baada ya ile waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry mjini Juba
ambako alipewa ahadi na Rais Kiir kwamba atakutana na kiongozi wa waasi
Riek Machar ili kutafuta njia ya kuumaliza mzozo huo.
Serikali ya Sudan Kusini imeahidi kuwa mkutano kati ya viongozi hao
wawili utafanyika hivi karibuni lakini kufikia sasa Machar bado
hajathibitisha iwapo yuko tayari kukutana na hasimu wake Kiir.
Kerry ametishia kuwa Marekani itamuwekea Machar vikwazo na kumchukulia
hatua nyingine kali iwapo hatajitolea kukutana na Kiir mjini Addis Ababa
kwa mazungumzo ya amani.
Katika mahojiano na jarida moja la Sudan siku ya Jumamosi,Machar
alinukuliwa akisema anadhani mkutano wa ana kwa ana na Kiir hautakuwa na
tija yoyote.
Mapigano yaendelea Bentiu
Mara ya mwisho Ban alikuwa nchini humo ilikuwa ni wakati wa sherehe za
Sudan Kusini kujinyakulia uhuru kutoka kwa Sudan mwezi Julai mwaka 2011
lakini leo yuko nchini humo huku kukiwa na mapigano makali katika mji wa
Bentiu ulioko katika jimbo la Unity na pia katika miji mingine katika
jimbo la Jonglei.
Waziri wa ulinzi Kuol Manyang amesema majeshi ya serikali yanaudhibiti
mji huo lakini kuna mapigano makali yanayoendelea viungani mwa mji huo
na kuongeza waasi walizidiwa nguvu baada ya kukabiliwa kwa saa nane.
Mapigano ya Sudan Kusini yamesababisha mauaji ya maelfu ya watu na
kuwaacha mamilioni wengine bila makaazi huku mashirika ya kutoa misaada
yakionya kuwa kiasi ya raia milioni moja wanakabiliwa na baa la njaa.
Mazungumzo ya kutafuta amani yanayosimamiwa na jumuiya ya ushirikiano ya
nchi za mashariki na pembe ya Afrika IGAD yanaendelea mjini Addis
Ababa,Ethiopia bila hatua zozote za kutia moyo.
Mwandishi:Caro Robi/afp/Reuters
No comments:
Post a Comment