Wednesday, February 5, 2014

Zitafutwe sababu watu kutoshiriki kupiga kura

Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva.PICHA|MAKTABA 
Na Mwananchi
Hatuna uhakika kama Serikali ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi (SMZ) au tume za uchaguzi za Nec na Zec zimejishughulisha kwa namna yoyote ile, kupata jibu na sababu zinazowafanya wananchi washindwe kushiriki katika chaguzi mbalimbali hapa nchini. Pia hatudhani kama mamlaka hizo zinasikitishwa na hali hiyo ambayo imedumaza demokrasia na kwenda kinyume cha Katiba, kwani kushiriki katika kupiga kura au kuchaguliwa ni moja ya haki za msingi za kila raia.
Hapa tunazungumzia chaguzi nyingi za kupata viongozi wa kisiasa kuanzia ngazi za Serikali za Mitaa, udiwani, ubunge na urais. Chaguzi hizo zimekuwa aibu kwa mamlaka husika katika pande zote za Muungano, kwani ni watu wachache wenye sifa za kupiga kura wamekuwa wakijitokeza kupiga kura. Hata katika chaguzi za Serikali za Mitaa, hali hiyo ya aibu imekuwa ikijitokeza kila zinapofanyika chaguzi hizo.
Jambo la kusikitisha ni kwamba hali imeendelea kuwa mbaya siku hadi siku, lakini mamlaka zote husika hazionyeshi kushangazwa au kutishwa na hali hiyo inayotia mashaka kama kweli mfumo wetu wa uchaguzi unaendana na matakwa ya demokrasia na utawala bora. Kama kweli kuna demokrasia na utawala bora katika nchi yetu, nini hasa kinachowakwaza wananchi kutojitokeza kupiga kura katika mfumo pendwa wa vyama vingi vya siasa?
Ilikuwaje kwamba wakati wa utawala wa chama kimoja wananchi zaidi ya asilimia 80 ya watu wenye sifa za kupiga kura walikuwa wakifanya hivyo. Miaka zaidi ya 20 ya mfumo wa siasa za vyama vingi imeonekana kutoleta maajabu yaliyotarajiwa. Sababu za hali hiyo zimebaki kuwa kitendawili kikubwa, kama kilivyo kitendawili kuhusu ukimya wa mamlaka zinazohusika na uchaguzi kutochukua hatua stahiki kuondoa hali hiyo.
Tukiangalia uchaguzi mdogo wa kumpata mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, uliofanyika juzi mjini Zanzibar, ni wapigakura 2,458 tu kati ya wapigakura 5,122 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura ndiyo waliojitokeza kupiga kura, sawa na asilimia 48 ya waliojiandikisha. Hali hiyo ni tofauti na chaguzi zote zilizofanyika hadi Uchaguzi Mkuu wa 2005 ambapo mwaka huo, wapigakura 12 milioni walipiga kura, kati ya milioni 16 waliokuwa wamejiandikisha kufanya hivyo.
Sote ni mashahidi wa Uchaguzi Mkuu wa 2010 ambapo wapigakura milioni 8 tu ndiyo waliopiga kura kati ya milioni 21 walioandikishwa. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa wananchi wengi kususia kushiriki katika chaguzi mbalimbali, kama tulivyoshuhudia katika chaguzi ndogo za ubunge na udiwani zilizofanyika baadaye katika majimbo na kata mbalimbali. Hatutazamii miujiza katika chaguzi ndogo zitakazofanyika katika kata 27 mwishoni mwa wiki.
Tunadhani kwamba wananchi hawana hamasa tena ya kupiga kura kutokana na sababu mbalimbali. Baadhi ya wapiga kura wanaogopa fujo kutokana na kampeni za majitaka, kupoteza imani na tume za uchaguzi, uchakachuaji wa matokeo, vitendo vya rushwa ikiwamo kuhonga wapigakura na ununuzi wa shahada, vyombo vya dola kuegemea upande mmoja na wapigakura kutoona majina yao katika mbao za matangazo.
Ni muhimu sasa serikali hizo ziboreshe mfumo wa upigaji kura, ikiwa ni pamoja na kuweka tume huru za uchaguzi, kuboresha Daftari hilo, kutoa elimu ya uraia na kuhakikisha Katiba mpya inatetea uchaguzi ulio huru na haki. Vinginevyo, tutaendelea kupata viongozi wanaotokana na kura za wapigakura wachache.

No comments:

Post a Comment