Dar es Salaam. Raia Watatu wa China, Huang Gin, Xu Fujie na Chen Jinzha wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, wamedaiwa kutoa hongo ya Sh30.2 milioni kwa Polisi ili wasiwakamate.
Hayo yalibainika jana wakati Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka akishirikiana na Wakili Faraja Nchimbi kuwasomea maelezo ya awali (PH) washtakiwa hao mbele ya Hakimu Mfawidhi, Isaya Arufani.
Wakili Nchimbi akisoma maelezo ya awali, alidai Novemba 2, 2013 washtakiwa hao walikamatwa na polisi, ASP Joel Lugaye, D/SSGT Gerwin na Simon Saye wakiwa na nyara za serikali na kwamba walitoa hongo ya Sh30.2 milioni kwa askari hao ili wawaachie.
Alidai kuwa baada ya washtakiwa hao kutoa kiasi hicho cha fedha, askari hao waligoma kukipokea na kuwapeleka kwenye kituo cha polisi na hatimaye kuwafungulia mashtaka hayo yanayowakabili.
Akiendelea kusoma maelezo hayo ya awali, Wakili huyo alidai kuwa washtakiwa hao walipekuliwa na kukutwa wakimiliki ganda la risasi iliyotumika kinyume cha sheria.
Siku hiyo ya tukio, washtakiwa hao wanadaiwa kukutwa wakiwa na nyara za serikali aina ya pembe za ndovu, shehena ya Pinde 706, vyenye uzito wa kilo 1880 zikiwa na thamani ya Sh5 bilioni.
Wakili huyo wa serikali alidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao wakati wakihojiwa polisi wakiri kufanya makosa hayo, lakini walipokuwa wakisomewa maelezo hayo ya awali waliyakana yote.
Maelezo hayo yalisomwa huku mkalimani akiyatafsiri kutoka lugha ya Kiingereza kwenda lugha ya Kichina kutokana na washtakiwa kutokujua lugha ya Kiswahili ama Kingereza ili waweze kuelewa kila kilichokuwa kikiendelea mahakamani hapo.
Baada ya maelezo hayo ya awali kusomwa, Hakimu Mfawidhi, Isaya Arufani aliwauliza washtakiwa hao ni maelezo yapi wanayoyakubali na yapi wanayakataa yanayohusiana na mashtaka hayo yanayowakabili.
Washtakiwa hao, kupitia mkalimani walikubali maelezo yao binafsi na kuyakataa mashtaka yote yanayowakabili. Upelelezi wa kesi hiyo ulikamilika Januari 28, 2014.
Washtakiwa hao, kupitia kwa mawakili wao, Edward Chuwa na Richard Rweyongeza waliwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakiomba wapewe dhamana, baada ya Mahakama ya Kisutu kuwanyima dhamana kutokana na kutokuwa na uwezo wa kisheria kusikiliza kesi hiyo.
Katika maombi hayo ya dhamana namba 14 ya mwaka 2013, Wachina hao kupitia kwa mawakili wao, wanadai kuwa dhamana ni haki yao kwa mujibu wa Katiba ya Nchi. Yanasikilizwa na Jaji Rose Teemba.
DPP aliwasilisha hati ya kupinga ombi la dhamana ya washtakiwa hao akiiomba mahakama hiyo isiwape dhamana, akibainisha kuwa ni kwa masilahi ya Taifa.
Hata hivyo mawakili wa washtakiwa nao waliweka pingamizi dhidi ya hati ya DPP kuiomba mahakama iitupilie mbali, wakidai kuwa imewasilishwa mahakamani isivyo halali.
Mawakili hao, Chuwa na Rweyongeza kwa nyakati tofauti walifafanua kuwa hati hiyo ya sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai iliyotumika katika hati hiyo haitumiki katika kesi hiyo.
Pia mawakili hao walieleza kuwa hati hiyo imewasilishwa kabla ya wakati, huku wakibainisha kuwa ilipaswa kuwasilishwa baada ya upelelezi kukamilika.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraja Nchimbi alisema kuwa Sheria iliyotumika katika hati hiyo ni sahihi kwa kuwa sheria zote yaani CPA na Sheria ya Uhujumu Uchumi zinaweza kutumika katika shauri hilo.
Pia SSA Nchimbi alisema kuwa DPP anaweza kuwasilisha hati ya kuzuia dhamana ya washtakiwa mahakamani wakati wowote na si lazima mpaka upelelezi uwe umekamilika.
Wachina hao walikamatwa na nyara hizo katika nyumba walimokuwa wakiishi, mapema Novemba mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment