Dar es Salaam. Mashabiki wa Tamasha la Pasaka wamewaomba waandaaji wa tamasha hilo kulialika kundi la Ambassadors of Christ ‘Kwetu Pazuri’ kutoka Rwanda mwaka huu.
Mashabiki hao walitoa tamko hilo hivi karibuni wakieleza kwamba kundi hilo ni kundi pendwa kwa mashabiki na wapenzi wa muziki wa injili hapa nchini kwa sababu ya nyimbo zao kukonga nyoyo za mashabiki na wapenzi wengi zaidi.
“Msama Promotions, watuletee Kwetu Pazuri, kwani ni kundi ambalo lina mashabiki na wapenzi wengi hapa nchini,” alisema mmoja wa mashabiki wa kundi hilo hapa nchini.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Msama Promotions, Alex Msama masuala yote yako kwenye taratibu za kupigiwa kura kupitia mashabiki na wapenzi wa muziki huo hapa nchini, huku wakisubiri taratibu za kupatikana kwa kibali cha tamasha hilo.
Msama alisema mwaka huu masuala yote yanayohusiana na Tamasha la Pasaka wanawakabidhi mashabiki na wapenzi wachague kupitia mfumo mpya wa upigaji kura kupitia ujumbe mfupi wa maandishi (sms).
Alisema mwaka huu wametoa nafasi hiyo ili kuwapa nafasi mashabiki wa muziki wa injili kuchagua mikoa, mgeni rasmi na waimbaji watakaoshiriki katika tamasha hilo.
Msama alisema kumchagua mwimbaji katika tamasha hilo ni kuandika neno Mwimbaji Pasaka unaacha nafasi jina la mwimbaji kwenda namba 15327 sambamba na kuchagua mkoa, unaandika neno Mkoa Pasaka unaacha nafasi kwenda namba 15327.
Aidha Msama alifafanua kuwa ili kumchagua mgeni rasmi unaanza na neno Mgeni rasmi Pasaka unaacha nafasi kisha jina la mgeni rasmi kwenda 15327.
No comments:
Post a Comment