Friday, December 13, 2013

Watu 11 wafariki ajali ya basi, 55 wajeruhiwa


Basi la abiri la kampuni ya Burdan lililopaja ajali jana eneo la Taula, wilayani Handeni mkoani Tanga na kusababisha vifo vya watu 11 na wengine 55 kujeruhiwa. Picha na Salim Mohammed 
Korogwe.Abiria 11 waliokuwa wakisafiri na basi la Kampuni ya Burudani kutoka Korogwe kuelekea Dar es Salaam akiwamo dereva wamefariki, huku wengine 55 wakijeruhiwa baada ya basi hilo aina ya Nissan kuacha njia na kupinduka kwenye kona wakati likijaribu kupishana na lori aina ya Fuso.
Hata hivyo, taarifa iliyowekwa mtandaoni na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo inasema waliofariki ni 12, majeruhi 93 na 11 walipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutokana na hali zao kuwa mbaya.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe, ajali hiyo ilitokea jana saa 1:30 asubuhi Barabara Kuu ya Segera- Chalinze, Kijiji cha Kwaluguru, Kata ya Kwedizinga, wilayani Handeni.
Mashuhuda wa ajali hiyo walisema basi hilo lilikuwa kwenye mwendokasi, lilipofika kona ya Kwaluguru liliacha njia na kupinduka.
Kamanda Massawe alisema majeruhi walipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Korogwe Magunga, kupata matibabu.
Alisema dereva wa basi hilo, Luta Mpenda (35) ni miongoni mwa waliokufa na kwamba, miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Magunga. “Majeruhi walipelekwa Hospitali ya Magunga na hali zao siyo nzuri, pia miili ya marehemu imehifadhiwa hapohapo,” alisema Massawe.
Hata hivyo, Massawe alisema chanzo cha ajali ni mwendokasi wa dereva wa basi, alipofika kona ya eneo la Kwalaguru usukani ulimshinda na kupinduka.
Francis Bendera ambaye ni miongoni mwa majeruhi, alisema kulikuwa na gari aina ya Fuso ambalo walikuwa wagongane nalo uso kwa uso, lakini dereva wa basi alipojaribu kukwepa basi lilimshinda na kupinduka.
“Tukiwa tunakaribia kona ile kuna Fusso ilitupita kwa kasi lilikuwa litugonge uso kwa uso, dereva wa basi letu akawa anajitahidi kukwepa lakini kutokana na ile kona kuwa kali gari ilimshinda na kupinduka,” alisema Bendera.Mashuhuda walisema walisikia kishindo kikubwa, walipokaribia eneo la tukio walikuta tayari gari imeshapinduka na baadhi ya watu kufa papo hapo.

No comments:

Post a Comment