Saturday, December 21, 2013

MSEMAKWELI: Tuache kuwageuza wenye VVU kuwa watenda dhambi

Nianze kwa kukusimulia kisa kimoja cha kusikitisha kilichomkuta msichana mmoja. Kisa hiki naamini kinawakuta watu wengi kwa njia tofauti, hasa wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU).
Nilipata habari za msichana huyu wakati huo akiwa na umri wa miaka 25, alikuwa akijua kuwa anaishi na Virusi vya Ukimwi na niseme ukweli hakuwa akificha jambo hilo kwa watu wake wa karibu.
Wazazi wake walilitambua hilo na alipofikisha miaka 15 walimweleza ukweli, msichana yule alisoma na kuhitimu kidato cha sita na alifaulu vizuri masomo yake na kujiunga na chuo fulani cha elimu ya juu.
Akiwa huko chuoni alianzisha uhusiano na kijana mmoja ambaye walikuja kuoana baada ya kumaliza masomo  yao.
Tangu walipoanza uhusiano hadi kufikia hatua ya kufunga ndoa na kupata mtoto wa kwanza, yule msichana hakumwambia kijana yule kwamba alikuwa akiishi na VVU.
Baada ya miaka mitatu, yule msichana alipata mimba nyingine, hapo ndipo alipoamua kumweleza ukweli mume wake ambaye licha ya kumwelewa, alimweleza kuwa hatomwacha , hata walipokwenda kupima, mumewe alionekana hana maambukizi ya VVU.
Tatizo lilianza baada ya mume wa yule binti kuwaeleza wazazi wake kuwa mke wake anaishi na VVU, wazazi wake walitaka amwache mkewe wakiamini kuwa atamwambukiza mtoto wao VVU. Yule kijana alikataa na hadi leo hii hana uhusiano mzuri na wazazi wake.
Nimetumia mfano huu kuonyesha jinsi baadhi ya watu katika jamii wengi wanavyojitwisha jukumu la kuamini kuwa mtu anayeishi na VVU ametenda dhambi.
Dhambi kubwa ambayo adhabu yake ni kumtenga na watu wengine, kumbagua na kutoshirikiana naye kwa karibu kila jambo.
Hata kama unaumwa kifua cha kawaida, ukikohoa mara kwa mara wakati ukiwa katika daladala au kwenye kundi la watu, siyo jambo la ajabu kuona watu wakiguna, kukutazama kwa jicho la ‘ana ngoma huyu’, huku wengine wakitafuta njia za kuondoka eneo ulilopo kwa kuogopa kuwa utawaambukiza.
Baadhi ya watu wanadhani mtu anayeishi na VVU alivipata kutokana na kutenda dhambi hasa ya uzinzi. Kwa jumla, jambo hilo halina ukweli wowote, hata kama lina ukweli ni binadamu gani aliye na kinga ya milele ya kutopata maambukizi ya virusi hivi?
Wapo waliozaliwa na VVU, wapo waliopata kwa kubakwa, kulawitiwa na wapo waliopata baada ya kujiingiza katika tabia za ushoga na ukahaba kutokana na mazingira yanayowazunguka kama umaskini,  kutengwa na familia na sababu nyingine nyingi. Kuwatenga watu waliopitia na wanaoishi katika mazingira kama hayo niliyoyataja hapo juu ni kwenda kinyume hata na maandiko matakatifu yaliyo katika vitabu vyetu vya dini.
Sikatai, wapo ambao wanafanya ukahaba, usagaji, ushoga na mambo mengine mengi bila  kutumia kinga na kupata maambukizi ya VVU, pia hao wanatakiwa kupewa msaada kwani baadhi yao wanafanya vitendo hivyo kutokana na ugumu wa maisha, wengine huzaliwa na kujikuta wakipenda ngono ya mwanaume kwa mwanaume au mwanamke kwa mwanamke.
Jiulize kama hali hiyo ikiendelea, miaka 10 ijayo nchi yetu itakuwa katika hali gani?
Wenye hatari ya kupata maambukizi ya VVU siyo wanaojihushisha na tabia fulani katika maisha, wapo pia wanaopata maambukizi kwa kujichoma sindano ambazo zimetoka kutumiwa na wenzao wenye maambukizi, sasa na hao unawabagua kwa misingi ipi?
Inashangaza, kwa sababu watu wanaowanyoshea wenzao vidole kuwa wanaishi na VVU, wao ndiyo mabingwa wa kushiriki ngono, tena kwa mtindo wa ‘kuingiliana kinyume na maumbile’, sasa nao wakipata VVU wabaguliwe?
Zipo taasisi na mashirika yanayotoa elimu kuhusu maambukizi ya VVU, lakini pia Serikali yetu inatakiwa kutochoka kuelimisha jamii, ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wanaofanya kazi katika vituo mbalimbali vya afya, maeneo ya kazi, mikusanyiko ya watu, katika shule mbalimbali ili watu wajitambue na kuelewa kiundani kuhusu jambo hilo.
Katika jamii yetu mtu akijitangaza kuwa anaishi na VVU au watu wakihisi tu kumnyooshea vidole hakuishi, ‘Jamaa ana moto yule’, ‘mume au mke wake kavuta kwa ngoma naye anayo’, lugha kama hizi sidhani kama ni suluhisho la kumaliza janga hili linalozidi kulitafuna taifa letu.
Kwa sasa maambukizi kitaifa ni asilimia 5.2, binafsi naamini kwamba Watanzania tunaweza kupunguza kiwango hicho kama tutaacha tabia ya kudhani kuwa anayeishi na VVU alipata maambukizi kwa kutenda dhambi, tukubali  kuwasaidie wenye maambukizi sambamba na kubadili tabia.
Sidhani kama kuna mtu ambaye hajawahi kupoteza ndugu yake au rafiki kwa ugonjwa huu wa Ukimwi, hivyo tunatakiwa kuanza kujifunza kuanzia hapo kwamba kama usipopata wewe atapata ndugu, jirani au rafiki yako. Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kumaliza mwaka, mengi yametokea yakiwamo ya kutengwa kwa watu wanaoishi na virusi hivi.
Siku hizi zipo baadhi ya kampuni ambazo kabla ya kukuajiri ni lazima ukapimwe kama una maambukizi ya VVU, jambo ambalo halina mashiko, pengine hata baada ya mada hii wapo watakaosema ‘jamaa tayari nini, mbona kaandika kuhusu jambo hili’, hakuna aliyegongwa muhuri wa kutopata maambukizi VVU, tusiwabague.

No comments:

Post a Comment