Shangazi ukweli nashindwa hata pa kuanzia. Ni hivi. Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 26. Nimekuwa na uhusiano na mvulana wangu kwa muda wa miaka minne sasa. Hivi sasa nina ujauzito wa miezi miwili. Kinachoniumiza kichwa, nasikia rafiki yangu mpenzi pia ana mimba ya huyu mpenzi wangu. Shangazi nasikia kufakufa hata sielewi la kufanya.
Fatihiya
Dar
Wala usife moyo mpwa wangu. Hebu fanya upelelezi kwanza. Hata ikiwa ni kweli, ndiyo yameshamwagika hayo. Hayazoleki. Lea mimba yako, uamuzi mwingine utafuata baadaye.
Nikimng’angania ataniletea magonjwa
Mimi nimeishi na mume wangu kwa miaka 11. Tuna watoto wanne. Shida ni kwamba mume wangu ana uhusiano wa kimapenzi na mama mmoja ambaye ni kahaba hodari mtaani. Nimwache mume na niwalee wanangu kivyangu? Kwani naogopa magonjwa. Tafadhali nisaidie kwani nimekuwa sina haja tena ya kuwa karibu naye.
Mama Mikaela
Mbeya
Ingawaje si sahihi kumshauri mtu aachane na mume au mke wake, lakini ikiwa umeridhika na utafiti wako si vibaya kuamua hivyo, maana utakuwa umefikiria mambo mengi sana. Ndiyo pamoja na kuwa mapenzi yapo lakini ni vyema kufikiria afya pia.
Mama mwenye nyumba anaboa!
Shikamoo mkubwa. Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka 26. Baada ya kumaliza masomo yangu na kupata kazi niliamua kuanza maisha yangu na kuondoka kabisa nyumbani kwetu. Hivi sasa naishi kwenye nyumba ya kupanga. Kinachonikwaza ni huyu mama mwenye nyumba wangu. Yaani kimtindo amekuwa akinisakizia kwa mmoja kati ya watoto wake. Pia amekuwa akinichimba mkwara, pindi ninapokuja na mpenzi wangu. Nifanye nini shangazi?
Damas
Dar.
Achana naye. Kama unamwona anazidi, tafuta nyumba nyingine upange.
Nahisi siko tayari kuoa!
Pole na mihangaiko shangazi. Mimi ni mwanamume mwenye umri wa miaka 45. Nimejaaliwa kupata watoto watatu na mke wangu mpenzi (ambaye kwa sasa ni marehemu). Tatizo ni kwamba nimekuwa mpweke mno. Ni miaka saba sasa imepita tangu kufariki dunia kwa mke wangu. Ndugu zangu wananishauri nioe mke mwingine. Lakini kwangu mimi naona bado ni mtihani. Nahisi siko tayari kuoa kwa sasa. Nisaidie shangazi.
Baba Nahila
Tanga
Pole sana Baba Nahila. Kuoa au kutokuoa ni uamuzi wako binafsi. Sioni kama kuna haja ya kushinikizwa. Fuata moyo wako.
Ni mbinafsi nahisi hana mapenzi na mimi!!!!
Shangazi mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 26. Nimeolewa miezi sita iliyopita. Tatizo ni kwamba mume wangu ni mbinafsi mno. Kiasi kwamba katika kipindi hiki kifupi tulichoishi, ameshindwa kuonyesha hisia za mapenzi kwangu. Kiukweli nampenda lakini sioni dalili za kufika naye mbali. Naona aibu kuachana naye maana sitaleta picha nzuri. Shangazi nifanye nini?
Grace
Moro
Kama umekubali kuolewa naye itakubidi uzoee na tabia yake. Kinyume cha hapo ndoa itakuwa historia.
Nahitaji vigezo mwenzenu
Pole na majukumu shangazi. Mimi ni mvulana mwenye miaka 27. Ninavyojitazama nahisi kuwa muda wa kuoa umefika. Kinachonitatiza ni je, nitajuaje vigezo vya mke bora. Maana sielewi hata kigezo kimoja.
Jacob
Ukiachilia mbali masuala ya upendo ambayo ndiyo msingi wa uhusiano yenu, anatakiwa awe mcha Mungu. Ikiwa atasimama katika ucha Mungu huo ni wazi atakuwa mke mwenye heshima maadili na utii. Nafikiri hivi ndiyo vigezo vya msingi.
No comments:
Post a Comment