Kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero kimependekeza wilaya hiyo kugawanywa na kuwa na majimbo mawili badala ya jimbo mmoja kama ilivyo sasa.
Mapendekezo hayo yametolewa kwa kuzingatia kuwa wilaya hiyo ina jumla ya kata 23 na tarafa tano, huku likiwa na kilometa za mraba 14,610 na kwamba licha ya ukubwa huo halmashauri hiyo imekuwa na ongezeko kubwa la watu ambapo kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 Kilombero ina watu 407,880.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Azimina Mbilinyi alizitaja sababu za kugawa jimbo kuwa ni pamoja na suala la usimamizi hasa wakati wa uchaguzi mkuu.
Alisema pia hali ya kisiasa imekuwa tete katika Jimbo la Kilombero tangia mwaka 2010, kwani ushindani mkubwa wa kisiasa kwa vyama vya CCM na Chadema na mara nyingi umesababisha fujo na ghasia za kisiasa wakati wa kampeni za uchaguzi na hata siku za uchaguzi na kutolea mfano uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Ifakara uliofanyika Juni 2013.
Azimina alisema wamependekeza kuwa Jimbo la Kilombero litaanzia kata ya Michenga, Lumemo, Ifakara hadi Kidatu huku Jimbo la Mlimba likianzia kata ya Idete hadi Uchindile.
No comments:
Post a Comment