Writen by
sadataley
11:43 AM
-
0
Comments
Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wasira
Na Habel Chidawali na Mwinyi Sadalla, MwananchiDodoma/Zanzibar. Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na
Uratibu), Steven Wasira amesema kauli zinazotoka kinywani mwa Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, haziendani na hadhi yake.
Wasira alikuwa anazungumzia kauli ya kiongozi huyo
aliyoitoa juzi wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika Viwanja vya
Kibandamaiti, Zanzibar na kusema kuna mpango wa siri wa kubadilisha
Sheria ya Kura ya Maoni ili Rasimu itakayopitishwa na Bunge la Katiba
ipitishwe na wananchi “kwa mteremko” kwa kuruhusu wakazi wa Tanzania
bara kupiga kura Zanzibar.
Maalim Seif alisema kitendo hicho kinakwenda
kinyume na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo imeeleza wazi kuwa
lazima kupatikane theluthi mbili ya Wazanzibari na Watanzania Bara
katika kupitisha Katiba na lazima Rasimu hiyo iungwe mkono na zaidi ya
asilimia 50 ya wananchi wa upande mbili za Muungano.
“Kitendo cha kukarabati sheria ili kuruhusu
Watanzania Bara kupiga kura ya maoni wakiwa Zanzibar ni kinyume na
sheria, hiyo ni sawa na kuamua kujitekenya na kucheka mwenyewe,” alisema
Maalim Seif.
Kutokana na kauli hiyo, Wasira alisema kumjibu
kiongozi huyo ambaye alisema: ‘amewekwa ndani ya Serikali inayoaminika’
ni kupoteza muda kwa kuwa kauli zake siku zote hazina mashiko na
zimejengwa katika misingi ya kubomoa.
“Yule ni Makamu wa Rais katika Serikali yetu,
asingepaswa kutoa kauli kama hiyo lakini anapozungumza wakati mwingine
hata huwezi kumwelewa anachokisema maana huamua kukurupuka,” alisema
Wasira.
Bila kuingia kwenye hoja ya Maalim Seif, Wasira
alisema kiwango alichofikia Makamu huyo wa Rais, alipaswa kuwa na busara
zaidi kwa kuwa ni kiongozi anayeaminiwa.
Akizungumzia suala la Wabara kupiga kura kama
Wazanzibari alisema: “hilo halipo na halitakuwapo, ukitaka njoo mle
ndani ya kamati yangu namba sita na kamati zingine halafu nianze kuwaita
mmoja na uwapige picha,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema katika kamati zote idadi
ya Wazanzibari ni kubwa na kuwa haina shaka yoyote katika upigaji wa
kura, theluthi mbili itapatikana tofauti na wengine wanavyosema.
Wasira alisema kauli zote ambazo zinatolewa na wanasiasa kwamba hakuna akidi ya kutosha kupitisha, hazina nafasi kwa wakati huu.
Katika mkutano huo, Maalim Seif ambaye pia ni
Katibu Mkuu wa CUF alisema Wazanzibari wenyewe ndiyo wenye mamlaka ya
kuamua aina ipi ya muungano wanaoutaka na Katiba ya aina gani na
kusisitiza kwamba kazi ya kudai mamlaka kamili ya Zanzibar ndiyo kwanza
imeanza visiwani humo.
“Kuna watu wanasema kuwa suluhisho la Ukawa na
Bunge la Katiba ufunguo wake anao Maalim Seif, si kweli kabisa.
Suluhisho la jambo hilo wanalo Wazanzibari wenyewe ikiwamo kuamua hatima
ya muundo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,” alisema.
Kuhusu Ukawa kurejee bungeni kwa jitihada zilizofanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, alisema wajumbe kutoka CCM katika vikao hivyo hawakuwa na nia njema ya kuheshimu Rasimu ya Katiba na hivyo mazungumzo hayo kushindwa kupata mwafaka.
Kuhusu Ukawa kurejee bungeni kwa jitihada zilizofanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, alisema wajumbe kutoka CCM katika vikao hivyo hawakuwa na nia njema ya kuheshimu Rasimu ya Katiba na hivyo mazungumzo hayo kushindwa kupata mwafaka.
No comments
Post a Comment