Writen by
sadataley
11:45 AM
-
0
Comments
Ramani ya barabara za juu itakavyokuwa kwenye makutano ya Ubungo
Na Ibrahim Yamola, MwananchiDar es Salaam. Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara nne za
juu ‘flyover’ katika jiji la Dar es Salaam ndani ya miaka mitatu na
daraja la Kigamboni Juni mwakani, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli
amesema.
Pia amesema Serikali imetenga Sh2 bilioni kununua
kivuko cha mwendo kasi kitakachokuwa kikitoa huduma kati ya Dar es
Salaam na Bagamoyo na kukamilika kwa ujenzi wa barabara za pembezoni
katika jiji hili.
Waziri Magufuli alisema hayo jana katika ziara ya
kukagua ujenzi wa barabara za jiji zinazojengwa kwa ufadhili wa Serikali
ya Japan.
“Tunajenga ‘flyover’ nne katika makutano ya
Tazara, Ubungo, Gerezani na DIT (Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam) na
ninaomba niwaahidi wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kwamba ndani ya miaka
mitatu foleni itabaki kuwa historia,” alisema na kuongeza:
“Tumetenga Sh28 bilioni kujenga kilomita 76.9 za
barabara za pembezoni au pete ambazo zikikamilika zitawezesha kupunguza
foleni.”
Alisema daraja la Kigamboni limekamilika kwa
asilimia 60 kwa gharama ya Sh214 bilioni, fedha kutoka Shirika la
Hifadhi za Jamii (NSSF), Barabara ya Mwenge - Tegeta kwa Sh89 bilioni,
Daraja la Tazara na Gerezani Sh100 bilioni.
‘Flyover’ Ubungo
Akizungumzia barabara hiyo ya juu ya Ubungo, Mkuu
Idara ya Usanifu na Viwango wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads),
Mhandisi Ebenezer Mollel alisema katika eneo la Ubungo kutakuwa na
barabara za ngazi tatu ambazo zitakuwa katika mifumo isiyowezesha
msongamano wa magari.
Mollel alisema barabara za mabasi yaendayo haraka
(BRT) itaendelea kufanya kazi kama kawaida ikiongozwa na taa, huku
magari yanayotoka barabara ya Sam Nujoma na Mandela, mfano Buguruni -
Mwenge au Mwenge - Buguruni yatakuwa yakipita juu.
“Katika barabara ya kwanza magari kutoka mjini
(Barabara ya Morogoro) kwenda Buguruni (Mandela) na Kimara (Morogoro)
kwenda Mwenge (Sam Nujoma) yataongozwa na taa. Magari yanayotoka
Buguruni kwenda Mwenge na Kimara kwenda Buguruni nayo yatafuata mfumo wa
taa,” alisema Mollel.
“Katika barabara ya pili magari yanayotoka mjini
(Barabara ya Morogoro) kwenda Mwenge na Kimara kwenda Buguruni nayo
yatatakiwa kuongozwa na taa na hii ‘Flyover Interchange’ haitakuwa na
msongamano kwani kila gari litakuwa na njia yake na hakutakuwa na
msongamano wowote.”
Alisema Serikali imekubaliana na Benki ya Dunia kufadhili mradi wa barabara hiyo itakayoondoa adha katika eneo la Ubungo Mataa.
Meneja BRT, Barakael Mmari alisema barabara ya mradi huo awamu
ya kwanza kutoka Kimara kwenda Kivukoni imekamilika lakini baadhi ya
wananchi wameanza kuharibu miundombinu yake kama taa, alama na kuiba
mifuniko ya majitaka.
“Tulitakiwa kuikabidhi barabara hii leo (jana) ili
tubaki kumalizia vituo tu, lakini Mheshimiwa Waziri (Dk Magufuli)
wananchi wameiba taa za barabarani pindi zinapogongwa na madereva
wasiozingatia sheria,” alisema Mmari
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki
aliwataka wananchi kulinda miundombinu ya barabara hizo ili iwanufaishe
watu wengi zaidi.
No comments
Post a Comment