Writen by
sadataley
11:28 AM
-
0
Comments
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ameteua mjumbe wake mpya wa kufuatilia masuala ya Libya.
Ghassan Salamé (wa kwanza mbele kushoto), mjumbe mpya wa Umoja wa Mataifa nchini Libya
Taarifa ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa, Ghassan Salamé, raia wa Lebanon ameteuliwa na António Guterres kuwa mjumbe maalumu wa umoja huo katika masuala ya Libya.
Guterres alikuwa na machaguo manne katika uteuzi huo ambapo ukitoa Ghassan Salamé wajumbe wengine ambao wangeliweza kuteuliwa kushika nafasi hiyo ni Ismail Ould Sheikh Ahmad, raia wa Mauritania ambaye hivi sasa ni mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Jamal bin Omar, raia wa Tunisia, mjumbe wa zamani wa Umoja wa Mataifa na Philip Spoerri, raia wa Uswisi ambaye pia ni mkuu wa zamani wa shirika la Msalaba Mwekundu.
Ghassan Salamé ni mjumbe wa tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na Libya. Katika kipindi cha miaka ya 2000 hadi 2003 alikuwa Waziri wa Utamaduni wa Lebanon.
Martin Kobler, raia wa Ujerumani alikuwa mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya tangu mwaka 2015 hadi hivi sasa.
Uteuzi wa Ghassan Salamé umefanyika katika hali ambayo mapigano baina ya makundi yenye silaha yangali yanaendelea nchini Libya.
Nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika haijawahi kushuhudia utulivu tangu mwaka 2011 baada ya kupinduliwa Kanali Muammar Gaddafi ambapo uingiliaji wa madola ya kigeni ndiyo sababu kuu ya kuendelea machafuko, mauaji na ukosefu wa utulivu na usalama nchini Libya.
Parstoday
No comments
Post a Comment