Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imevitaka vituo vya redio na televisheni kuacha kusoma habari zilizoandikwa kwenye magazeti kwa kina badala yake visome vichwa vya habari pekee.
Mkurugenzi wa TCRA, Mhandisi James Kilaba alisema jana jijini hapa kwamba mamlaka hiyo imegundua baadhi ya vyombo vya habari bado havijatii agizo la Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe lililotolewa Machi 3, mwaka huu.
Alisema vyombo vyote vya redio na televisheni vinatakiwa kufuata agizo hilo kuanzia leo (jana), bila kuvunja masharti yaliyowekwa.
Agizo lililotolewa awali na Dk Mwakyembe lilivitaka vyombo hivyo kusoma vichwa vya habari vilivyochapishwa kwenye magazeti na siyo habari yote kwa kina ili kulinda soko la magazeti.
Alisema iwapo watangazaji hao watasoma habari yote iliyoandikwa gazetini hakuna mtu atakayekwenda kununua gazeti hilo tena.
Dk Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, alitoa agizo hilo kwenye maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari dunia ambayo kitaifa ilifanyika mkoani Mwanza.
“Mamlaka ina wataarifu vyombo vya habari vya kielektroniki kuacha kusoma habari kwa kina za magazeti na badala wanatakiwa kusoma vichwa vya habari,” alisema Mhandisi Kilaba.
No comments
Post a Comment