Dar es Salaam. Yanga imempa mkataba wa miaka miwili mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajibu wenye thamani ya Sh50 milioni na gari lakini Simba wao wamesema kwamba hawakuwa na mpango naye na tayari Kamati ya Usajili ilikata jina lake.
Ajibu ni miongoni mwa wachezaji wa Simba ambao wamemaliza mikataba ndani ya klabu hiyo ingawa mkataba wake unamalizika ramsi mwezi ujao lakini watani zao Yanga tayari wamembana na mkataba mpya.
Yanga walianza mazungumzo na Ajibu kabla hata ya kumalizika kwa msimu wa ligi ambao umewapa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo huku Simba nao wakitafuta mbinu za kumwongeza mkataba mpya lakini mchezaji huyo alikuwa akiwasumbua kila walipohitaji kukutana ili kufanya mazungumzo upya.
Habari za uhakika ni kwamba Ajibu amemalizana na Yanga mchana wa leo Alhamisi, na tangu Jumatatu ya wiki hii alikuwa akikutana na viongozi wa Yanga ili kuweka mambo sawa na leo wamekamilisha dili hilo.
Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema kuwa Ajibu hawatakuwa naye tena na wanafahamu kwamba watani zao Yanga wanamuhitaji hivyo Kamati ya Usajili iliamua kuondoa jina lake kwenye mipango ya msimu ujao.
No comments
Post a Comment