Mchambuzi wa siasa kutoka Kenya, Profesa Patrick Lumumba amesema kitendo cha Mwenyekiti wa Barrick Gold Corporation ya Canada ambayo ni mmiliki mkubwa wa Acacia Mining Limited, Prof. John Thornton Gold nchini na kukubali kulipa fedha ambazo zimepotea kutokana na udanganyifu-kwenye biashara ya mchanga wa madini, kimedhihirisha Rais John Magufuli ni shujaa na kiongozi wa kuigwa Afrika.
Aidha, Prof Lumumba amesema endapo Rais Magufuli ataendelea na kasi hiyo, ndani ya miaka 10 ijayo Tanzania itakuwa nchi yenye uchumi mkubwa zaidi Afrika.
Aidha, amesema viongozi wengine wa Afrika wanapaswa kujiamini pia.
Profesa Lumumba aliyasema hayo jana wakati akitoa somo kwenye Tamasha la Tisa la Kigoda cha Mwalimu Nyerere lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), lililohusu 'Mwanasiasa na mchango wake katika kukua ama kuanguka barani Afrika'.
"Tunapaswa kuwa wasafi, alichokifanya Rais Magufuli dhidi ya Accacia hadi wanafunga safari kuja Tanzania kuomba msamaha ni kitendo cha ujasiri na kinapaswa kuigwa na viongozi wa Afrika," alisema Profesa Lumumba."
"(Rais) Magufuli amekua mkombozi wa Watanzania."
Alisema kwa miaka 30 Afrika imetawaliwa na viongozi mafisadi na wala rushwa lakini kwa sasa mtazamo huo umeanza kubadilishwa na viongozi wachache wakiwamo Rais Magufuli, Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari.
Prof. Lumumba ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shule Kuu ya Sheria Kenya, alisema viongozi wengi wa sasa Afrika wamekosa uzalendo tofauti na waasisi wa nchi za Afrika.
Alisema waasisi wengi wa nchi za Afrika walikuwa wazalendo na nchi zao, waliweka mbele mslahi ya nchi kuliko ubinafsi, akitolea mfano aliyekua Rais wa Zambia, Keneth Kaunda.
"Alifariki dunia akiwa na dola za Marekani 8,000 (sawa na Sh. milioni 17) katika akaunti yake ya Benki," alisema.
Alisema viongozi Afrika wamekua na utajiri mkubwa usioweza kuelezeka hata kushindwa kujenga miundombinu na kutoa huduma za kijamii, huku wananchi wao wanaowaongoza wanazidi kuwa masikini.
Alisema kuna baadhi ya nchi Afrika ambazo hadi leo wanawasafirisha wagonjwa kwenda nchi za Ulaya kutibiwa wakati wana rasilimali nyingi katika nchi zao.
Profesa Lumumba alisema kwa sasa nchi nyingi za Afrika zimetawaliwa na rushwa, ukabila, akitolea mfano Kenya ambako alisema ukabila umetawala kiasi cha kusababisha kutokuwapo kwa maendeleo.
"Kenya wanapaswa kuja kujifunza kwa Rais Magufuli, Kenya hatuzalishi chochote kwa sababu ya rushwa na ukabila," alisema Prof. Lumumba na kueleza zaidi kuwa "hadi leo Kenya wananunua mahindi kutoka nchi za Ulaya, huku Liberia wakinunua kuku kutoka Brazil."
Aidha, Profesa Lumunba aliwataka vijana wa Afrika kuwa wazalendo kwa kupenda vitu vinavyozalishwa nchini kwao kuliko kupenda vitu vya nje.
"Tunapaswa kuwa kitu kimoja, tutumie fedha moja," alisema Prof Lumumba.
"Kwa mfano leo nilipokuja hapa Tanzania nilipaswa kutumia fedha nilizotoka nazo Kenya, hati ya kusafiria iwe moja.
"Kwa kufanya hivyo tutakua tumepiga hatua ya maendeleo."
No comments
Post a Comment