Writen by
sadataley
1:51 PM
-
0
Comments
Ni Rais Mstaafu wa jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi akisalimiana na viongozi mbali mbali
mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Kisiwandui katika kilele cha
maadhimisho ya kumbukumbu ya mashujaa.
Ni msafara Maalum wa Vijana wa CCM
waliokuwa na Picha ya Maehemu Mzee Abeid Aman Karume na mabango
yaliyoandikwa maneno mbali mbali aliyowahi kutoa kama nasaha enzi za
uhai wake, wakipokelewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.
Abdallah Juma Abdallah (kushoto) ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Mahgarib Mh.
Ayuob Mohamed.
Ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Sita Aman
Abeid Karume akisalimiana na viongozi pamoja na Maafisa wa vikosi na
majeshi ya Ulinzi ya Tazania na Zanzibar mara baada ya kuwasili
kisiwandui.
Ni Vijana wa CCM wakiwa katika hali ya
ukakamavu na wakitembea kwa Mwendo wa haraka huku wakiwa Picha ya
Maehemu Mzee Abeid Aman Karume pamoja na mabango yenye ujumbe unaohusu
siku ya mashujaa.
Ni Mke wa Aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar na Kiongozi Mkuu wa ASP Marehemu Mzee Karume, Mama Fatma Karume.
Ni Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Idd Akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar ,
Dkt. Abdallah Juma Abdallah alipowasili Kisiwandui.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF))
Generali Venance Mabeyo akisalimiana na viongozi mbali mbali akiwemo
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdallah Juma Abdallah
alipowasili Kisiwandui.
Baadhi ya Wazee wa CCM pamoja na viongozi wa Chama na serikali wakisoma hitima katika dua ya kuwaombea Mashujaa.
Makamo wa Rais wa jamhuri ya muungano
wa Tanzania Mh. Samia suluhu Hassan akiwasili katika maadhimisho ya
kumbukumbu ya mashujaa.
Baadhi ya Mawaziri wa SMZ wakisikiliza mawaidha yaliyokuwa yakitolewa katika hitima hiyo.
Ni Makamo wa Rais wa Jamhuri ya
muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan akiweka mashada ya maua ya
heshima katika kaburi la Marehemu Mzee Karume, kwa niaba ya Rais wa
Jamguri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi akiweka mashada ya maua ya heshima katika kaburi la
Marehemu Mzee Karume. PICHA NA AFISI KUU CCM ZANZIBAR.
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
BAADHI ya Waasisi wa ASP, Wasomi na
Viongozi wa serikali na kidini walioudhuria maadhimisho ya kumbumbuku ya
Mashujaa Zanzibar, wamesema fursa na mikakati iliyoachwa na Mzee Karume
inatakiwa kuwekwa Kisheria ndani ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984,
ili serikali yoyote itakayoongoza nchi itekeleze kwa vitendo.
Walieleza kwamba miongozo na fursa za
kiuchumi, kijamii na kimaendeleo ilichoachwa na Marehemu Mzee Karume
inayotekelezwa kwa sasa haitoshi kubakia katika Ilani ya Uchaguzi ya
CCM ya mwaka 2015/2020 bali inatakiwa iwekwe rasmi katika Katiba ya nchi
ambayo ni sheria mama ya serikali yoyote inayoingia madarani.
Wito huo ulitolewa na wananchi hao mara
baada ya Dua ya hitima ya maadhimisho ya kumbukumbu ya mashujaa ambao ni
waasisi wa ASP waliokomboa Zanzibar toka katika Utawala wa Kisultani,
iliyoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dkt. Ali Mohamed Shein huko Katika Makao Makuu ya ASP ambayo kwa sasa ni
Afisi kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar eneo alilozikwa Mzee Karume.
Akizungumza katika maadhimisho hayo
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Majaliwa Kassim Majaliwa
amesema kiongozi Mkuu wa harakati za Ukombozi wa Zanzibar Mzee Karume,
ameacha urithi wa Hazina ya fikra na mawazo ya maendeleo yanayotakiwa
kuendelezwa na vizazi vya sasa na vijavyo.
Waziri Mkuu huyo amekiri kwamba miaka
nane ya utawala wa Kiongozi huyo uliwatoa Wananchi kwenye giza la uonevu
na mateso na kuwaweka kwenye mwanga wa mafanikio ya kimaendeleo
yanayoendelezwa kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Saba Zanzibar kwa
kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa
Pili wa Rais Mh. Mohamed Aboud Mohamed akitoa nasaha zake kwa wananchi
amewasihi kuendelea kuunga mkono serikali iliyopo madarakani kwani ndiyo
inayosimamia na kutekeleza, fursa zilizoachwa na Waasisi wa ASP
waliowekewa siku maalum ya kitaifa kukumbukwa kwa kusomewa dua kutokana
na juhudi zao za kukomboa nchi.
Alisema kuwa Zanzibar itaendelea
kuimarika kiuchumi endapo kila mwananchi bila ya kujali itikadi za
kisiasa na kidini ataweza kulinda amani, utulivu na kuchukia kwa vitendo
tabia ubaguzi, kama ilivyokuwa kwa mashujaa wa ASP walivyoondosha
utawala wa mabavu.
“ Leo tumeadhimisha kumbukumbu ya
mashujaa wetu lakini bado tuna kazi kubwa ya kulinda na kuendeleza
urithi wa Wazee wetu kwani bado, zipo choko choko za baadhi ya watu
wenye nia ya kuchafua amani ya nchi yetu lakini na sisi wajue tupo imara
kama wazee wetu walivyokuwa mashujaa na kutetea maslahi ya wanyonge”,
alielea Waziri Aboud.
Pia Mwenyekiti wa Chama Cha Wakulima
(AFP) Zanzibar, Said Soud Said amesema kazi aliyofanya Mzee Karume ndio
iliyozaa matunda ya wazanzibar kuishi kwa utulivu na kujiamulia mambo
yao wenyewe.
Amesema ukombozi wa Zanzibar wa mwaka
1964 aliousimamia yeye ndio hasa kioo cha Wazanzibar Duania nzima
kujiona kuwa wapo huru na wenye uwezo wa kujenga taifa lao kiuchumi bila
vikwazo vyovyote.
Soud ambaye pia ni Waziri asiyekuwa na
Wizara Maalum wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, alisema baada ya
mapinduzi hayo Mzee Karume aliweka misingi iliyofuatwa na viongozi
waliotawala baada yake ambayo kwa sasa wananchi wote wa Zanzibar
wananufaika nayo.
Aidha kwa upande wake Bi. Asha Simba
Makwega aliyelelewa na Mzee Karume na baadae akawa kada wa Afro Shiraz
Party(ASP), alisema kwamba kiongozi huyo alitumia muda wake
kushughulikia kero na matatizo ya wananchi kuliko muda alioutumia kwa
familia yake, hali inayothibitisha uzalendo na utaifa wa kweli wa shujaa
huyo.
Sambamba na hayo Makamo Mwenyekiti wa
Chama Cha ADA TADEA, Juma Ali Khatib, alithibitisha utekelezwaji wa
falsafa ya Mzee Karume ya Wazanzibar kujitawala kwa Nyanja zote zikiwemo
kielimu, kiafya, kimiundombinu, kiutendani na kiutawala na kueleza kuwa
dhana hizo zinatekelezwa kwa vitendo na serikali ya Awamu ya saba
inayoongozwa na Dkt. Shein.
“ Sote ni mashahidi kuwa serikali
zilizopita zimefanya kadri zilivyojaaliwa hata katika Mfumo wa Serikali
ya Umoja wa kitaifa, tulishuhudia baadhi ya viongozi wa upinzani ndani
ya mfumo huo walikuwa wakishutumu na kulaumu serikali ambayo na wao
walikuwa ni washirika wa kufanya maamuzi jambo ambao katika siasa za
kimaendeleo halina mashiko.”, alisema Waziri Ali ambaye pia ni Waziri
asiyekuwa na wizara maalum wa SMZ na kumsifu Rais wa Zanzibar Dkt. Shein
kwa kufananisha utendaji na busara zake kuwa ni sawa na za Mzee Karume
kwani bila ya kujali Dkt. Shein aliteuwa vyama vitano vya upinzani
kuingia katika serikali yake kwa lengo la kutengeneza umoja na utaifa wa
kwa kweli na kuondosha ubaguzi wa itikadi za kisiasa.
Naye Dkt. Moses John amesema kazi
iliyobaki baada ya Mzee Karume kuacha misingi imara ya kuleta uhuru wa
nchi, vijana wanatakiwa kusoma kwa bidii ili wapate ujuzi na utaalamu wa
kuendesha nchi kisomi kulingana na wakati uliopo sasa ili kuenzi fikra
za mashujaa hao kwa vitendo.
Viongozi mbali mbali wa kitaifa
wameudhuria maadhimisho hayo wakiwemo Makamo wa Rais wa jamhuri ya
muungano wa Tanzania mh. Samia Suluhu Hassan aliyemwakilisha Rais Dkt.
John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa, Makamo wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, waziri waziri wa mambo ya
nje na ushirikiano wa afrika mashariki, Balozi dkt. augustine mahiga,
Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali
ya mapinduzi Zanzibar Said Hassan Said na viongozi wengine mawaziri,
manaibu waziri, makatibu wakuu na wakurugenzi.
Pia Viongozi wengine ni Mke wa aliyekuwa
Rais wa Kwanza wa Zanzibar Mama Fatma Karume, Rais Mstaafu wa Awamu ya
Pili ya jamhuri Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya sita wa
SMZ Aman Abeid Karumr, Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwena Mwema Shein,
Makamo wa Rais mstaafu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt. Mohamed
Gharib bilal, Spika wa Baraza la wawakilishi Zanzibar Zubeir Ali
Maulid, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdallah Juma Abdallah,
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi Bi. Waride
Bakari Jabu.
Kwa upande wa viongozi wa dini na
mabalozi kutoka nchi mbali mbali walioudhuria ni pamoja na Mufti Mkuu wa
Zanzibar Shein Saleh Omar Kaabi, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Othman
Hassan Ngwali, Askofu wa Kanisa Katoliki Zanzibar Augostino Shao, Balozi
mdogo wa msumbiji Jorge augusto, mwakilishi wa balozi mdogo wa China
Cheng Kun, Balozi mdogo wa Oman na Mwakilishi wa shirika la kimaifa la
UNICEF Tanzania.
Hitima hiyo ilikamilishwa na dua za
Viongozi wa madhehebu mbali mbali ya dini yaliyopo nchini baada ya
kuzuru kaburi la Mzee Karume ambapo kwa upande wa dini ya kiislamu
aliyesoma dua ni Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi
ambapo madhehebu ya Kikiristo aliyesoma ni Askofu wa Kanisa katoliki
Augostino Shao sambamba pia dhehebu la kihindi nao walisoma dua hiyo ya
kuwaombea mashujaa hao.
Maadhimisho hayo ya siku ya mashujaa
uadhimishwa kila ifikapo April 7 ya Kila mwaka, ambayo ndio siku
aliyouliwa Mzee Karume na wapinga maendeleo, Mungu azilazu roho za
mashujaa wote walioipigania Zanzibar mahala pema peponi Amin.
Na Mjengwa Blog
No comments
Post a Comment