Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Monday, August 31, 2015

HOTUBA YA MGOMBEA URAIS KUPITIA CHAMA CHA CHADEMA NA UKAWA MH. EDWARD NGOYAI LOWASSA YA KUZINDUA ILANI NA KAMPENI YA UCHAGUZI MKUU

Jangwani-Dar-es-Salaam, 29 AGOSTI 2015 Ndugu Wana Dar es salaam na Watanzania wenzangu Leo ni siku ya kihistoria. Baada ya miaka ishirini na tano tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe, vyama vya upinzani wa CHADEMA, CUF, NCCR na NLD umeungana chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi kupigania uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kuwa na mgombea mmoja katika ngazi zote. Miaka zaidi ya hamsini ya utawala wa serikali za CCM na waasisi wake, umekuwa utawala wa wachache walio hodhi madaraka na mali za nchi. Leo tunaanza safari ya uhakika ya kuleta mabadiliko ya kweli nchini. Mabadiliko yaletayo neema na kujenga upya mfumo wa uchumi, haki na sheria nchini. Mabadiliko ya kuimarisha huduma za jamii kama elimu, afya, maji na makazi. Mabadiliko ya kuondoa umaskini. Mabadiliko tunayatoahidi ni mabadiliko ya kurejesha matumaini kwa Watanzania kwa kubadili hali zao za maisha. Kila mwaka hali na ubora wa maisha ya Watanzania imeshuka wakati tunaambiwa kuwa pato laTaifa linakuwa. Lakini Watanzania wanachotaka siyo takwimu bali kuona kipato chao kinakua, shule, hospitali na barabara bora zinajengwa. Wanataka kupata maji safi na salama ya kunywa. Wanataka makazi bora. CHADEMA na UKAWA, tuna dhamira ya kuleta mabadiliko ya kweli ili kuona azma ya Watanzania tangu uhuru ya kuondoa umaskini, maradhi,na ujinga inahitimishwa. Ili tufanye hivyo tuahitaji tufanye mabadiliko ya fikra, uongozi, sera na utendaji. Leo Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi za ki-uchumi, kisiasa na kijamii. Changamoto hizi ni matokeo ya sera za utawala wa Chama kimoja wa miaka hamsini. Sote ni wahanga wa siasa na sera hizi. Miaka Hamsini ya CCM imetosha. Tunataka mabadiliko na siyo ahadi zile zile kila mwaka Tusidanganyike, CCM hawana jipya Chagueni UKAWA wenye dira ya kubadili maisha ya wananchi. Mimi ninauchukia umaskini na mimesimamia maendeleo kwa vitendo. Nilipokuwa Waziri Mkuu nilijaribu kubadili hali hii. Nilisimamia ujenzi wa shule za kata, Chuo Kikuu cha Dodoma. Nilihakikisha mikataba mibovu ya maji inavunjwa na sasa wananchi wa kanda ya ziwa wanapata maji safi. Ndugu watanzania CCM wanauliza tuna mpango gani wa kumaliza umaskini. Sisi hatuahidi tu. Tutatenda. Ilani yetu ni dira ya kuondoa umaskini kwa mikakati sahihi na siyo nadharia. Mkakati wa kuondoa umaskini si wa sekta kwa sekta bali wa sekta zote kwa pamoja. Ni ujumla wa utendaji na utekelezaji wa sera za kila sekta utakao leta maendeleo. Mkakati wangu na UKAWA wa kuondoa umaskini utakuwa na nguzo tano:- Kupunguza matumizi ya serikali na mashirika yake na kuimarisha utendaji na uwajibikaji. Kukuza pato la serikali kwa kudhibiti ukwepaji na misamaha ya kodi holela na kuhakikisha nchi inawekeza katika sekta muhimu na inapata gawio halisia kutoka wawekezaji Kukuza uchumi kwa sera na sheria endelevu ikiwa ni pamoja na kukuza biashara na uwekezaji hasa katika sekta za madini, kilimo, viwanda, ufugaji na uvuvi na kuondoa kodi kwa wanyonge. Kuimarisha huduma za umma kama elimu, afya, maji na makazi, na mazingira Kuimarisha utawala bora na mfumo wa haki na sheria chini ya Katiba ya Wananchi. Chini ya misingi hii na ili kufanikisha mkakati wa kuondoa umaskini, serikali yangu itafanya yafuatayo:- ELIMU BORA KWA KILA MTANZANIA Nimelisema hili huko nyuma. Nalisema tena leo. Elimu kwanza, Elimu kwanza, Elimu kwanza. Kwa hiyo mkakati wetu wa msingi utakuwa kutoa Elimu itatayogharamiwa na serikali kwa kila Mtanzania kutoka elimu ya msingi hadi Chuo Kikuu na pia:- Kuimarisha elimu ya teknolojia, ustadi na ufundi inayojenga uwezo wa kujiajiri na ushindani katika soko la ajira. Ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya elimu ikiwa ni pamoja na shule za Kata. Kusimamia ubora wa viwango vya elimu kote nchini. Kuimarisha taaluma na mitaala katika mashule. Kuondoa utoro darasani, na kuboresha afya za wanafunzi. Kuboresha maslahi na vitendea kazi kwa walimu ikiwa ni pamoja na nyumba, posho ya kufundishia, usafiri na zana za teknolojia. Kufuta michango ya maabara ya shule za kata AFYA Afya na tiba ya kila Mtanzania itagharamiwa kupitia bima za gharama nafuu na mifuko ya hifadhi ya jamii Tutaimarisha afya ya msingi pamoja na kinga kupunguza gharama za tiba. Serikali itahakikisha kuna uwiano na upatikanaji wa watumishi wa afya katika kada mbalimbali ili kuleta tija na huduma stahiki. Itaimarisha miundombinu ya afya pamoja na kujenga hospitali za kisasa ili kusogeza huduma za afya karibu na jamii na pia kuepukana na tiba za nje ya nchi. Tutarejea kwa lengo la kuboresha maslahi na vitendea kazi katika sekta ya Afya ikiwa ni pamoja na nyumba na usafiri. Tutathibiti ongezeko la gharama za huduma za afya bila kuathiri uendeshaji wa watoaji huduma za afya kama vile serikali na hospitali za sekta binafsi. ARDHI, MAJI NA KILIMO Tutaimarisha mfumo wa umiliki wa ardhi kwa Watanzania na kudhibiti migogoro ya ardhi hasa kati ya wakulima na wafugaji. Tutapima ardhi yote ya Tanzania na kumilikisha vijiji na wakulima kwa hati za serikali ili kuipa thamani. Tutaleta mapinduzi ya kilimo kwa kuimarisha elimu, ufundi na teknolojia ya kisasa na kumkomboa mkulima kutoka jembe la mkono. Tutasimamia kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa na kuunganisha sekta hizo na ya viwanda. Kuhakikisha kuwa wananchi wanatunza na kulinda vyanzo vya maji. Tutakuza kilimo cha umwagiliaji kwa kuwapa wakulima elimu na mikopo ya riba nafuu ya kuvuna maji na kujenga miundombinu husika. Tutaweka mazingira rafiki yatakayomhakikishia kwa kila Mtanzania kupata maji safi na salama. Kumaliza kero za maji nchini kutamkomboa mwanamke kutokana na adha ya kuchota maji kwa kichwa Nitafuta kodi zote za mazao na mifugo kwa wakulima na wafugaji. Tutasimamia kilimo cha biashara kinachozingatia maslahi ya nchi na ya Watanzania. Tutaanzisha programu maalum ya kufufua mazao asilia ya Tanzania hususan mkonge. Tutaanzisha Benki ya Maendelo ya Ufugaji na Uvuvi. MIUNDOMBINU Tutaboresha bandari zilizopo na kujenga mpya kama vitega uchumi vya Taifa ili kurejesha biashara tulizopoteza kwa bandari za nchi jirani. Tutajenga barabara nchini kwa kuzingatia ubora hasa zile za vijijini. Tutajenga reli ya kati kwa viwango vya kisasa Tutajenga shirika la Ndege la Taifa linalojiendesha kwa misingi ya faida. Tutajenga miundombinu ya kisasa na kuondosha misongamano ya magari hasa katika majiji ya Dar es salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha Tutaimarisha uzalishaji na usambazaji wa umeme vijijini ili kufikia zaidi ya asili mia sabini na tano ya Watanzania VIWANDA Tutaimarisha sekta ya viwanda kuwa mhimili wa uchumi kwa uzalishaji wa bidhaa na ajira endelevu Tutajenga viwanda vipya vya kusindika mazao ya kilimo, uvuvi na ufugaji. Tutahakikisha kuwa ndani ya miaka mitano mali ghafi zote za Tanzania zinasindikwa kabla ya kusafirishwa nje ili kuongeza mapato na ajira ya mamilioni ya vijana. Tutaanzisha Benki ya Ukuzaji wa Viwanda UCHUMI Tutabadili mfumo wa Uchumi wa nchi ili kuhakikisha kuwa mfumo wa uchumi wa Tanzania unakuwa ni wa soko-kijamii ambapo nguvu za soko zitatumikia jamii kwa serikali kuweka uwiano wa mapato unaohakikisha huduma za kijamii zinapatikana kwa ufanisi. Tutalinda sekta binafsi na bidhaa za ndani kwa kuwapa Watanzania upendeleo wa maksudi kwa kipindi cha mpito ili waimarike na waweze kuhimili ushindani. Tutawapa wafanyabiashara wetu upendeleo katika manunuzi ya serikali na kuwajengea mazingira mazuri ya biashara na kodi endelevu. Tutawawezesha Watanzania kupata mitaji ya biashara kwa masharti nafuu kabisa. Tutavutia uwekezaji na wawekezaji wenye tija. Kuweka udhibiti wa wahamiaji wasioleta tija wala maslahi kwa Taifa. Tutaimarisha sera ya ubia baina ya Serikali na Sekta binafsi kwenye maeneo muhimu ya kiuchumi na kibiashara. Pia, kuwawezesha Watanzania kuwekeza kwa njia ya ubia na wawekezaji wenye mitaji mikubwa bila kujali wanapotoka. Tutaimarisha usimamizi kwa kubadilisha mfumo wa Vyama vya Ushirika nchini ili utokane na uendeshwe na wakulima wenyewe ikiwa na pamoja na kuwawezesha kuboresha makazi kwa mpango wa kushirikiana kujenga nyumba bora Tutaanzisha na kuwezesha uanzishaji wa viwanda vidogovidogo vinavyotoa ajira kwa wingi kwa kuvihusisha na vyuo vya ufundi na benki maalum kwa lengo hilo. AJIRA Tutasimamia swala la ajira hasa kwa vijana kwa kukuza elimu ya ufundi ili waweze kujiajiri Tutazipa kipaumbele sekta zinazozalisha ajira kwa wingi hasa za viwanda, kilimo, ufugaji, uvuvi na utalii na kuzipa unafuu wa kodi ili zikue kwa haraka. Tutawapa wawekezaji wakubwa katika sekta hizi upendeleo maalum na viwango vya kodi nafuu. NISHATI NA MADINI Serikali itashiriki kikamilifu katika uzalishaji wa nishati Itatengeneza mazingara mazuri ya kisera yatakayovutia na kuwezesha ushiriki wa Watanzania na ubia kati yao na wageni. Serikali yangu itaupa uzalishaji mkubwa wa umeme wa maji kipaumbele namba moja, umeme wa makaa ya mawe kipaumbele namba mbili, umeme wa gesi asilia kipaumbele namba tatu na umeme wa urana kipaumbele namba nne. Serikali itatoa vipaumbele muhimu kwenye usambazaji wa huduma kubwa ya umeme sehemu za uzalishaji uliyolenga masoko ya ndani, ya nchi jirani na ya nchi za kigeni. Itapitia upya mikataba yote mikubwa ya nishati na madini ili kubaini iliyo mibovu na kuifanyia maboresho. Serikali yangu itatumia sehemu ya hisa zake kwenye raslimali kubwa ya gesi asilia iliyopatikana hapa nchini kama rehani kwenye kujichukulia mikopo kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya mabomba ya gesi. Serikali itatoza kodi na ada ndogo zaidi kwa wazawa wenye ubia kati yao na wageni kuliko zitakazotozwa kwa wageni wasiowekeza kwa kushirikisha wazawa. Serikali itasitisha utoaji wa misamaha ya kodi isiyo lazima kwenye sekta ya madini, na badala yake itawekeza kwenye kuongeza thamani ya raslimali zake za madini. Tutakuza nishati mbadala kutamkomboa mwanamke kutokana na adha ya kukata kuni MALIASILI NA UTALII Tutasimamia uvunaji na matumizi ya rasilimali za Taifa kwa manufaa ya kila Mtanzania wa kizazi hiki na kijacho Tutapiga vita ujangiri na kuimarisha utunzanji wa hifadhi za taifa na mazingira Tutachochea ujenzi wa miundombinu ya utalii nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mahoteli na kuimarisha mafunzo Tutaongeza idadi ya watalii kufikia milion mbili ifikapo 2020. UTAWALA BORA, ULINZI WA NCHI NA USALAMA WA RAIA Tutasimamia Katiba mpya inayolinda haki za msingi za wananchi na kuweka bayana mipaka ya madaraka ya serikali na viongozi, Bunge na Mahakama. Tutasimamia haki za raia na kuangalia upya sheria kandamizi ili wananchi kama Masheik wa Zanzibar hawasoti jela kwa sababu za kisiasa. Tutaimarisha mafunzo ya vyombo ya Polisi hasa wapelelezi na waongoza mashtaka ili wapate uwezo wa kusimamia utoaji wa haki. Tutavipa vyombo vyote vya ulinzi na usalama nyenzo na kuboresha mazingira yao ya kazi na maslahi UZALENDO, UTENDAJI NA UWAJIBIKAJI Tutajenga uzalendo ili kila Mtanzania aweze kutathmini mchango wake kwa taifa kila siku Tutaimarisha nidhamu, utendaji na uwajibikaji katika Sekta ya Umma Tutaimarisha mchango wa Wataalam wetu, wanawake na vijana katika kusimamia uchumi na kuwajengea mazingira stahiki ya kazi pamoja na mafao. Tutapiga vita rushwa na ubadhirifu katika sekta ya Umma na binafsi Tutadhibiti na kupunguza matumizi ya serikali ikiwa ni pamoja na kufuta safari za watumishi serikalini zisizokuwa muhimu pamoja na zile za Rais na kupiga marufuku matumizi ya mashangingi serikalini. Tutadhibiti deni la Taifa kwa kuanza na ukaguzi wa madeni ya serikali ili kuhakiki jinsi yalivyotumika Tutaimarisha uwazi na kuondoa usiri katika shughuli za serikali na kuweka bayana mikataba yote ya nchi ikiwa ni pamoja na ile ya mafuta, madini na gesi asilia KUKUZA PATO LA SERIKALI Tutadhibiti mapato kutokana na raslimali kwa kupitia upya viwango vya mirabaha kutokana na madini na gesi asilia ili kuhakikisha kuwa Tanzania inapata gawio stahiki. Serikali itaanzisha Wizara maalum itakayosimamia nishati ya gesi na mafuta. Tutaimarisha ofisi ya Msajili wa Hazina ili kusimamia vema uwekezaji wa Serikali katika mashirika na mapato yake. Tutahakikisha kuwa mashirika ya umma yanaendeshwa kwa misingi ya faida na uadilifu. Tutadhibiti ukwepaji kodi za ushuru wa forodha na kupiga marufuku misamaha ya kodi holela ili kuokoa mabilioni ya fedha yanayopotea kila wiki. Sambamba na hilo tutarahisisha utaratibu wa kulipa kodi ili kuondoa kero na mazingira ya rushwa. Kwa kudhibiti makusanyo ya kodi tutakusanya fedha za kugharimia huduma za msingi kama afya na elimu kikamilifu. KUIMARISHA MUUNGANO Tutaimarisha umoja, usalama na udugu wa Watanzania na Muungano kwa misingi ya haki na usawa WANAWAKE, WATOTO NA WAZEE Wanawake watapewa fursa na haki sawa katika elimu na uchumi ili waweze bila kuwezeshwa. Tutahakikisha wazazi wanapata fursa ya kuwa walezi na wafanyakazi kwa kuongeza urefu wa likizo ya uzazi Tutaimarisha elimu ya watoto hasa wasichana na kukuza fursa zao na kukomesha ndoa za watoto wadogo. Tutaongeza uwakilishi wa akina mama katika ngazi zote serikalini na mashirika yake kufikia asili mia hamsini ifikapo 2020. Wazee na wasiojiweza watapewa posho ya kujikimu inayokidhi mahitaji ya msingi itakayowawezesha kuishi kwa heshima na kulinda utu wao ndani ya familia na jamii zao. SANAA, UTAMADUNI NA MICHEZO Tutaendeleza na kuwezesha vipaji vya sanaa na michezo Tutarudisha viwanja vya michezo vilivyovamiwa Tutafuta kodi zote za vifaa vya michezo. Tutadhibiti viwango na maadili ya bidhaa za nje zinazoingizwa nchini na kuzitoza kodi halisia Tutajenga taasisi na vyuo vya kukuza michezo ili kuhakikisha kuwa ndani ya miaka mitano Tanzania inashiriki kwa ushindi katika mashindano ya kimataifa ya soka na riadha Tutalinda Hakimiliki za sanaa nchini Tutafuta kodi za sanaa kwa wasanii chipukizi ili kuwapa muda kwa kujijenga. SERA YA MAMBO YA NJE YENYE TIJA KWA TAIFA Tutakuza ushirikiano wa Kimataifa wenye tija na Ujirani mwema. Tutatetea haki za binadamu, usawa wa nchi na kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika diplomasia ya kimataifa. Tutakuza umoja na ushirikiano wa Umoja wa Afrika, Jumuia ya Afrika Mashariki, SADC na Umoja wa Mataifa. Tutaimarisha Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na kudai mabadiliko ya mfumo ili kuleta usawa wa nchi shiriki. Ndugu Watanzania Naomba nimalizie kwa kusema yafuatayo Natambua kuwa uongozi ni dhamana. Mkinichagua nitaienzi dhamana hiyo kwa utendaji uliotukuka. Nawaahidi Watanzania kuwa kwa uwezo, akili, uzoefu na nguvu zangu zote nitawatumikia. Nawaomba nanyi mniahidi jasho lenu na uwezo wenu wote ili kwa pamoja tuvuke. Tutajikomboa toka utawala wa CCM unaodumaza uchumi na maendeleo. Tutaanza safari ya uhakika kuondoa umaskini. Mabadiliko pia ni kuthamini utu na kukataa hadaa ya hongo ili kuuza haki yako ya kuchagua. Msikubali rubuni za uchaguzi kwa kupewa pesa au vitu. Rushwa ya uchaguzi ndiyo sera ya CCM. Ukikubali basi umeuza pia haki na sauti yako ya kuwalalamikia walio madarakani. Imetosha. Tukatae. Tulinde utu na haki zetu. Tuchague mabadiliko. Mabadiliko ni fikra. Ni kufikiri na kutenda tofauti. Hatuwezi kuendelea kufikiri na kutenda kama kwamba hatuna dharura ya maendeleo. Kwanza tuanze kwa kufanya mabadiliko na tujiamini kuwa sisi kama Taifa tunaweza. Tunaweza kujitegemea na kuleta maendeleo yetu wenyewe bila kutegemea wafadhili. Hii si ndoto. Nchi nyingi zimefanikiwa kuondoa umaskini katika kizazi kimoja. Tujifunze kutoka kwao. Tuwe taifa linalotumia raslimali zake kujiendeleza na siyo kuwanufaisha wageni na kuwafanya Watanzania watwana katika nchi yao. Inabidi tuache kuwa taifa ombaomba. Tuache kuukubali na kuvaa umaskini kama joho la fahari. Mabadiliko ya kweli hayawezi kuletwa na CCM. Tusitegemee kuwa leo wana jipya. Ndiyo maana ahadi walizotoa miaka thelathini iliyopita ndizo wametoa juzi. Tukatae hadaa. Miaka hamsini ya CCM imetosha. Tunaamani kwamba tutashinda kwa sababu Watanzania mpo nyuma yetu. Watanzania mmeamua kuleta mabadiliko. Kura yako ndiyo itakayokuwa mkombozi wako. Hakikisha unapiga na kuilinda kura yako. Wakati wa mabadiliko ni sasa. Mungu ibariki Tanzania. Asanteni sana Chanzo:Chadema Blog

MASPIKA WA MABUNGE DUNIANI WAKUTANA UMOJA WA MATAIFA

Na Mwandishi Maalum, New York Mkutano wa Nne unaowakutanisha Maspika 180 na Manaibu Spika 35 kutoka nchi 140, unaanza leo ( jumatatu) hapa Makao Mkuu ya Umoja wa Mataifa. Mkutano huu wa siku tatu na ambao umeandaliwa na Chama cha Mabunge Duniani ( IPU), utafunguliwa na Rais wa IPU Bw. Chowdhury Saber na Katibu Mkuu wa Umoja wa Matafa, Ban Ki Moon. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Ann Makinda anaongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu. Mkutano ambao Maspika wanatarajiwa kujadiliana kwa kina namna ya kukabiliana na changamoto za Amani, Demokrasia na Maendeleo kwa maono ya Kibunge. Mkutano wa Nne wa Maspika, ulitanguliwa na Mkutano wa Kumi wa Maspika wanawake, mkutano uliofanyika kwa siku mbili ( jumamosi na Jumapili). Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Ann Makinda ameshiriki kikamilifu na kuongoza baadhi ya mikutano. Mkutano wa Nne wa Maspika ni sehemu ya mfululizo wa mikutano ya Maspika hao na ambayo imekuwa ikifanyika kuelekea Mkutano wa Kilele wa Viongozi wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanyika wiki chache zijazo ambapo watapokea na kupitisha Ajenda Mpya za Maendeleo Endelevu baada ya 2015. Chanzo: CCM Blog

Maandamano yazuka nje ya bunge- Ukraine

Afisa mmoja wa polisi ameuawa na wengine zaidi ya mia moja kujeruhiwa nje ya jengo la bunge la Ukraine, baada ya wabunge wa nchi hiyo kuunga mkono mpango wa awali wa kuipa eneo linalothibitiwa na waasi Mashariki mwa nchi hiyo, mamlaka ya kijitawala. Waandamanaji waliwarushia mawe na mabomu ya petroli maafisa hao na kuna ripoti kuwa kulitokea mlipuko kati kati mwa waandamanaji hao. Maandamano hayo yalitokea muda mfupi baada ya wabunge kuidhinisha eneo la Donetsk na Luhansk ambayo yamo chini ya waasi wanaoungwa mkono na Urussi mamlaka zaidi. Mkataba wa amani wa kusitisha mapigano ungali unadumisha nchini humo. Mkataba wa amani wavunjwa Mpango huo ulioidhinishwa na wabunge na sehemu ya mkataba huo uliosainiwa mwezi Februari mjini Minsk. Wakati huu wa msimu wa joto mapigano kati ya wanajeshi wa Ukraine na waasi yameongezeka. Lakini pande hizo mbili ziliafikiana wiki iliyopita kusitisha mapigano hayo hiyo kesho, wakati wanafunzi watakapokuwa wakirejea shuleni. Licha ya kuwa mikataba kadhaa ya kusitisha mapigano yamekiukwa katika siku za hivi karibuni, afisa mmoja mwandamizi wa shirika la kimataifa la OSCE, nchini Ukraine, Alexander Hug, ameonya kuwa hakuna upande wowote katika mzozo huo umedumisha mkataba huo wa kusitishwa mapigano. Lakini muda mfupi baada ya wabunge 265, kuidhisha mswada huo wa ugatuzi katika bunge la nchi hiyo, maandamano nje ya bunge yakachacha. Chanzo:BBC Swahili

Thursday, August 13, 2015

Jimmy Carter asema ana kansa

Rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter ametangaza kuwa ana maradhi ya kansa. Carter mwenye umri wa miaka tisini ,na siku za hivi karibuni alifanyiwa upasuaji wa ini. Jimmy amesema kuwa imebainika kuwa ana kansa ambayo imekwisha sambaa katika baadhi ya sehemu za mwili wake. Ameongeza kuwa yupo katika mpango wa kuweka vizuri ratiba yake kwa lengo la kupata matibabu zaidi. Jimmy Carter toka aondoke madarakani ,amekua akijisughulisha na kazi za kuhudumia jamii duniani kote. Chanzo:BBC Swahili

Ban Ki moon afanya maamuzi magumu

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon, amesema amemfukuza mkuu wa kulinda amani toka UN nchini Afrika ya kati baada ya kutuhumiwa kuhusika na madai ya unyanyasaji wa watoto kingono. Bwana Ban amesema mwanadiplomasia wa Senegal Babacar Gaye angeachia ngazi kama mkuu wa ujumbe. Ban aliongeza kuwa alipatwa na hasira na aibu baada ya taarifa hizo za unyanyasaji wa ngono na ukandamizaji kwa watoto. Taasisi ya kutetea haki za binaadam Amnesty International imewatuhumu wanajeshi hao wa kulinda amani wa UN kwa kumbaka msichana wa miaka kumi na miwili na kumuua kijana na baba yake katika mji mkuu wa nchi hiyo Bangui, mapema mwezi huu. Uchunguzi pia unaendelea namna wanajeshi hao wa umoja wa mataifa kuhusika na madai ya unyanyasaji dhidi ya wanajeshi wa Ufaransa mwaka jana. Chanzo:BBC Swahili

Monday, August 10, 2015

JK, Magufuli waendelea kunguruma Kusini

Rais Jakaya Kikwete akiwa na Waziri wa Ujenzi na mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli jana aliendelea kuunguruma katika mikoa ya Kusini na kuzindua Kivuko cha MV Mafanikio cha Mtwara kilichogharimu Sh3.3 bilioni. Kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba watu 100 na magari sita kinamaliza kero iliyokuwa ikiwakabili wananchi wanaovuka kutoka Pwani ya Mtwara Mikindani kwenda Pwani ya Msangamkuu, kilizinduliwa siku moja baada ya kuzindua kipande cha barabara ya Ndundu-Somanga mkoani Lindi. Kuzinduliwa kwa kipande hicho cha barabara kumeifanya Serikali kukamilisha ujenzi wa miradi 13 mikubwa katika Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara. Vilevile, kwa kukamilisha kipande hicho cha barabara ambayo ni sehemu ya Barabara Kuu ya Dar es Salaam-Kibiti-Lindi hadi Mingoyo, kunaifanya Serikali kutumia Sh9 trilioni katika miaka 10 ya uongozi wa Rais Kikwete. Kilomita 60 za kipande cha Ndundu-Somanga ni sehemu pekee iliyokuwa imebakia kukamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami, ambayo imekuwa kero kwa wananchi wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara. Baada ya tukio hilo juzi, Rais Kikwete jana aligeukia kivuko hicho na kusema kuwapo kwake ni utekelezaji wa ahadi alizotoa kwa wananchi. Aidha aliwataka wananchi na wasafirishaji kuzingatia maadili ya kiwango cha uzito wa kivuko hicho. “Suala la kivuko lilikuwa kero kubwa sana na tuliliona hasa watu walipokuwa wakivuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine. Jambo muhimu ni kukitunza kivuko kwa kubeba watu na mizigo kwa kiwango kinachokubalika” alisema Rais Kikwete. Awali, Dk Magufuli akimkaribisha Rais Kikwete alisema watu wa Mtwara walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya kivuko. “Mheshimiwa Rais, wakati unaingia madarakani tulikuwa na vivuko 13, lakini kwa kipindi chako tumeongeza vivuko vingine 15 na kukamilisha idadi ya vivuko 28 vyenye uwezo wa kubeba tani tofauti tofauti, kikiwamo hiki cha Mtwara ambacho gharama yake ni Sh3.3 bilioni na tumekarabati vivuko vingine saba,” alisema Dk Magufuli. Akizungumzia viwango vya nauli vilivyopangwa, Dk Magufuli alisema ni Sh300 kwa mtu mzima, wanafunzi hawatatozwa, huku watoto na wanafunzi wasiovaa sare za shule watalipa Sh100. Kuhusu miradi mingine ya Kusini, Waziri Magufuli aliitaja kuwa ni Daraja la Umoja lililokamika ujenzi wake, ujenzi wa barabara za lami ya Songea-Namtumbo; Peramiho Junction-Mbinga, Masasi-Mangaka na usanifu wa kina kwa ajili ya ukarabati wa Barabara ya Mtwara-Mingoyo-Masasi yenye urefu wa kilomita 200, ambao umekamilika. Miradi mingine inayoendelea ni ujenzi kwa barabara za lami za Mangaka-Mtambaswala, Mangaka-Nakapanya, Nakapanya-Tunduru-Matemanga na Matemanga-Kilimasera yenye urefu wa kilomita 68.2. Waziri Magufuli aliitaja miradi mingine inayoendelea ya ujenzi wa kiwango cha lami ni barabara za Kilimasera-Namtumbo, upembuzi yakinifu wa barabara ya Mtwara-Newala-Masasi na kuwa zabuni tayari imetangazwa kwa ajili ya ujenzi sehemu ya barabara ya Mtwara-Mnivata. Madaraja 12 yajengwa Kama ilivyo kawaida yake kutaja bila kusoma popote miradi anayojengwa na Serikali, Dk Magufuli alisema Serikali katika kipindi hicho imejenga madaraja makubwa 12, ambayo ni Rusumo (Kagera), Umoja (Mtwara), Mwanhuzi (Simiyu), Kikwete (Kigoma), Nangoo (Mtwara), Ruhekei (Ruvuma), Mbutu (Tabora), Mwatisi (Morogoro), Ruvu (Pwani), (Nanganga (Mtwara), Maligisu (Mwanza) na daraja la waendao kwa miguu la Mabatini (Mwanza). Dk Magufuli pia alisema madaraja mengine madogo zaidi ya 7,200 yamejengwa na kukamilika katika kipindi cha uongozi wa Rais Kikwete, huku mengine makubwa saba yakiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi ambayo ni Kigamboni (Dar es Salaam), Kilombero (Morogoro), Kavuu (Katavi), Sibiti (Singida), Ruvu Chini (Pwani), Lukuledi 11, (Mtwara) na Kolo la Dodoma. Kana kwamba haitoshi, alisema kuna madaraja mengine makubwa ambayo yako katika maandalizi ya kujengwa. Ni pamoja na Momba, Mwiti, Simiyu, Wami, Ruhuhu, Daraja jipya la Salendar, Daraja jipya la Wami Chini, Pangani na daraja la wandeao kwa miguu la Furahisha.

Lowassa: CCM hodari wa kuiba kura

Mgombea wa urais kupitia Chadema, Edward Lowassa ameituhumu CCM kuwa ni hodari wa kuiba kura hivyo akawataka wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura ili hata sehemu ya kura hizo ikiibiwa, Ukawa ishinde kwa kishindo. Lowassa ambaye ni waziri mkuu wa zamani aliuambia umati wa wafuasi wa Ukawa uliojitokeza jana kumpokea katika ofisi za makao makuu ya CUF yaliyopo Buguruni kuwa ili kufanikisha ushindi wa kuwawezesha kuingia ikulu hawana budi kushikamana, kushawishiana kupiga kura kwa wingi na kuzilinda Oktoba 25. Kauli hiyo ya Lowassa ambaye amelelewa kisiasa na CCM tangu alipojiunga akiwa mdogo mwaka 1977, inaendeleza tuhuma ambazo hutolewa na vyama vya upinzani kuwa chama hicho huchakachua matokeo wakati wa uchaguzi. Hata hivyo, Lowassa hakuwa na vielelezo wala kuthibitisha kuhusu tuhuma hizo dhidi ya chama chake cha zamani. “Tukiwa na umoja, tukiwa na mshikamano tutawaondoa Jumapili asubuhi sana. Tutahitaji mshikamano, tatahitaji ushawishi wa kupiga kura tupate angalau asilimia 90 ili wakiiba asilimia 10 tuwasamehe,” alisema Lowassa katika hotuba yake iliyokuwa inakatishwa na kushangiliwa na na salamu ya CUF ya “Hakiii” na kujibiwa “kwa wote.” “Hodari sana wa kuiba CCM kura. Sasa tupate kura nyingi za kutosha hata wakiiba kura hausikii na kuna usemi wa Chadema unaosema ‘piga kura, linda kura’ na sisi CUF ni hodari sana wa mambo hayo.” Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipotafutwa kwa simu kuhusu madai hayo, alijibu kwa ujumbe wa maneno kuwa asingeweza kuzungumza bali atumiwe ujumbe, na alipotumiwa ujumbe huo hakujibu. Lubuva: Aeleze wanaibaje Akizungumzia madai hayo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji mstaafu, Damian Lubuva alisema Lowassa angeeleza jinsi wanavyoiba kura. “Ili kutoa majibu ya uhakika naomba tufanye utafiti wa kutosha juu ya tuhuma hizo, lazima tujue ni njia zipi watu wanaiba, vinginevyo nitaeleza kitu ambacho sina ufahamu nacho. Yeye (Lowassa) kama mtu aliyekuwa serikalini lazima ana ufahamu walikuwa wanaiba vipi, angeeleza.” Tume huwa inaendesha uchaguzi kwa mujibu wa taratibu na sheria na iwapo kuna mtu anasema kura zinaibwa ajitokeze aeleze kinagaubaga ili ofisi yake ifanye utafiti wa kina. “Naomba nieleweshwe kura huwa zinaibiwa vipi? Hii imekuwa ni hisia, wengine wanasema tutaibiwa kura zetu wakati upande mwingine unasema hawa wataleta fujo kwa visingizio vya kuibiwa kura,” alisema Jaji Lubuva. Lowassa ambaye alihamia Chadema siku 11 zilizopita na baadaye kuteuliwa kugombea urais kwa mwamvuli wa Ukawa kupitia Chadema, alisema safari ya Ikulu itafanikishwa kwa kupiga kura na siyo maandamano, hivyo Watanzania watunze shahada za kupigia kura. Hata hivyo, hakuendelea kueleza undani kuthibitisha ni namna gani CCM huiba kura. Kiongozi huyo aliyeonekana mwenye furaha, aliwataka wanawake nao kujitokeza kwa wingi siku ya upigaji wa kura huku wakiwa wameshapika vyakula majumbani mwao ili nao wapate fursa za kupiga na kulinda kura. Lowassa alisema ameingia Ukawa ili kuandika historia ya nchi kukuza uchumi na kuondoa umaskini na kutekeleza kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya “mabadiliko ya kweli yatapatikana nje ya CCM.” Ukawa kutoyumba Mbunge huyo wa Monduli anayemaliza muda wake, alisema Ukawa ipo imara haitayumbishwa kirahisi na wafitini, licha ya baadhi ya watu kujipitisha kwa viongozi wa juu na kutaka kuwarubuni ili umoja huo utetereke. “Wanakuja kupitisha hela na kuhongahonga lakini viongozi wapo imara…hawahongeki hawa! Wanapita na maneno kwenye magazeti ya ufukuzi ufukuzi, nawaambia muwapuuze,” alisema Lowassa bila kuwataja wahusika. Alisema kuna baadhi ya watu wanaleta propaganda kuwa Ukawa ikiingia madarakani nchi haitatawalika kiasi cha kuwatisha wafanyabiashara kukimbiza fedha zao nje ya nchi, jambo ambalo si la kweli. “Waongo wakubwa hao…nchi itatawalika kuliko awali, Ukawa ikiingia madarakani nchi itatulia tuli, wasiwadanganye mkimbize hela zenu..tupo imara,” alisema. Juma Duni afafanua Mgombea mwenza wa urais wa Ukawa, Juma Duni Haji alisema hajahamia Chadema kutafuta vyeo kwa kuwa ameondoka akiwa Makamu Mwenyekiti wa CUF na waziri katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na hatua yake hiyo ni kutimiza za kuing’oa CCM madarakani. “Ni vizuri mkaelewa kwamba tutafanya kosa kubwa tusipofika ikulu mwaka huu, tutahitaji kusubiri miaka 50 zaidi maana jamaa hawa wakija kutulia balaa yao ni mara 100 ya wanayoyafanya. Wanaoleta mabadiliko ni vijana siyo wazee,” alisema Duni Haji. Alisema Ukawa wanatakiwa kushirikiana kwa dhati na Watanzania kwa ujumla kwa kuwa mwaka huu ni wa mageuzi na kila mmoja ana wajibu wa kufanya kampeni ya kuiondoa CCM ili kutafuta hatima bora ya nchi. Kauli ya Mbowe Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuna nguvu nyingi zinatumika kuivunja Ukawa lakini umoja huo utabaki kuwa imara na kutimiza malengo yake ya kushika dola mwaka huu kwa nguvu za Mungu. Alisema vyama vya upinzani vimefanya siasa zao kwa shida kwa miaka 25 huku baadhi ya makada wakifungwa, kufukuzwa kazi, ndoa kuparaganyika, kufungwa au kufunguliwa kesi mahakamani lakini miezi minane iliyopita imekuwa migumu zaidi kutokana na baadhi ya watawala kupatwa na hofu baada ya Ukawa kujiimarisha. “Safari yetu imebaki kidogo tufike tunakoelekea. Sasa akitokea kiongozi mmoja wetu bila kujali ni wa chama gani akaona kwamba malengo yetu siyo ya muhimu kuliko fursa binafsi, huyo hatufai,” alisema Mbowe na kushangiliwa. Alisema maandamano ya leo kumsindika Lowassa kuchukua fomu yataanzia CUF na kupitia ofisi za Makao Makuu ya NCCR-Mageuzi Ilala hadi NEC kabla ya kurudi ofisi za Chadema Kinondoni. Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi aliwataka wafuasi wa Ukawa kujitokeza kwa wingi kumsindikiza mgombea wa urais kupitia umoja huo na ikiwezekana kila mfuasi apeleke watu 10. Mbatia amvaa JK Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema Ukawa itaendelea kuhubiri amani siku zote ili CCM na vyombo vya dola visipate sababu ya kuwatuhumu na kwamba Uchaguzi Mkuu utafanyika kwa amani. Alisema Rais Jakaya Kikwete alihubiri chuki dhidi ya wapinzani kwa kuwaita maadui siku alipozungumza na wafuasi wa CCM baada ya kumpokea mgombea wa urais kupitia chama hicho, Dk John Magufuli alipotoka kuchukua fomu za kuwania. “Sikuamini kama Rais Kikwete angesema maneno yale eti anawaambia wana-CCM wana mikakati ya kila aina ya kushinda na kwamba ‘msiogope kujihadhari na nguvu za adui’. Yaani sisi wapinzani ni adui? Ukianza kuwaita wenzio adui wakati wewe ni amiri jeshi mkuu, nchi hii unaipeleka wapi?” alihoji Mbatia. Malim Seif apongeza Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, aliwashukuru wafuasi wa Ukawa waliojitokeza kumpokea Lowassa wakati wa ziara ya kutembelea ofisi zao na kwamba moyo huo uendelee hadi Oktoba 25 siku ya kupiga kura. “Hakuna silaha kubwa kuliko umoja, ushirikiano na mshikimano. Tukishirikiana tukawa wa kweli wa nafsi zetu bila shaka Lowassa anasubiri kuapishwa tu na sisi Zanzibar tumeshamaliza kazi,” alisema Maalim Seif na kushangiliwa na umati wa wafuasi hao. Hali ilivyokuwa Mapema kabla ya Lowassa hajawasili Buguruni wafuasi wa CUF walianza kujikusanya taratibu saa 4 asubuhi kwa kuzunguka na ngoma barabara za Uhuru na za mitaa kuingia ofisi za chama hicho. Baadaye umati huo uliongezeka kiasi cha kufunga barabara ya Uhuru kwa muda wakati Lowassa anaingia saa 6:20 mchana na kupokelewa na Maalim Seif, Makaidi, Mbatia na viongozi waandamizi wa Ukawa. Idadi hiyo ya watu iliwapa kibarua maofisa usalama wa Ukawa walioonekana wakihaha kutengeneza njia ili viongozi hao wapite. Baada ya viongozi hao kuwahutubia wafuasi hao, waliingia katika ukumbi wa Mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi saa 7:15 mchana na kufanya mazungumza ya takriban saa moja na baadaye viongozi kutoka nje ya CUF kuondoka. Nafasi ya Lipumba Kikao cha Baraza Kuu kilijadili nafasi ya mwenyekiti iliyoachwa na Profesa Lipumba na suala hilo liliachiwa Mkutano Mkuu wa chama ambao utaitishwa baada ya miezi sita kwa kuwa ndio wenye uwezo wa kufanya uchaguzi huo kwa mujibu wa katiba ya CUF. Akitoa taarifa ya kikao hicho, Maalim Seif alisema Baraza Kuu limeunda kamati maalum ya watu watatu itakayofanya kazi na katibu mkuu kwa miezi sita kabla ya Mkutano Mkuu kukaa na kumchagua mwenyekiti na makamu wake, nafasi ambazo ziko wazi. Waliochaguliwa kwenye kamati hiyo ni Twaha Taslima ambaye ni mwenyekiti na wajumbe wawili ambao ni Aboubakary Khamis Bakary (Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar) na Sererina Mwijage (mbunge mstaafu wa viti maalumu. Chanzo:mwananchi.co.tz

Mpigania Haki za binaadamu Mexico auawa

Mtetezi mmoja wa haki za binaadam nchini Mexico aliyekuwa akizisaidia familia kuwapata ndugu zao waliopotea amekutwa amekufa baada ya kupigwa risasi mwishoni mwa wiki. Mwili wa Miguel Angel Jimenez Blanco ulikutwa katika taksi moja aliyokuwa akiimiliki karibu na nyumbani kwake (katika mji wa Xaltianguis) Kusini Magharibi mwa jimbo la Guerrero. Kwa tabia alikuwa na hulka ya kukasirishwa na kile alichokiona kama kutochukua hatua kwa mamlaka husika, Jemenez Blanco alisaidia utafutwaji katika eneo ambalo wanafunzi 43 walipotea karibu na mji wa Iguala mwaka uliopita,pia alifichua upoteaji wa mamia ya watu katika mji huo kunakosababishwa na magenge ya wahuni. Chanzo:BBC Swahili

Michael Brown akumbukwa

Huko Marekani,mamia ya watu walisimama kimya kwa muda wa dakika nne na nusu kwa pamoja mjini Ferguson ,missouri sehemu ambayo kijana asiye na hatia Michael Brown aliuwawa na polisi mmoja wa kizungu mwaka mmoja uliopita. Ishara hiyo inaashiria muda ambao mwili wake ulilala katikati ya barabara bila kupata msaada wowote. Njiwa wawili walipeperushwa hewani na watu waliandamana kimya kimya ili kutoa heshima kwa Michael Brown na wengine ambao walikufa katika mikono ya polisi. Mauaji hayo yalileta mjadala dhidi ya ubaguzi wa polisi nchini Marekani na ulimwenguni. Chanzo:BBC Swahili

Saturday, August 8, 2015

Dk Magufuli, Lowassa pambano la karne

Wakati zikiwa zimesalia siku 14 kabla ya kuanza kwa kampeni za urais, ubunge na udiwani, macho na masikio ya wengi yanaelekezwa kwa wagombea wawili kutoka vyama vikuu vya siasa, Dk John Magufuli wa CCM na Edward Lowassa wa Chadema, ambao uchambuzi wa gazeti hili unaonyesha wana mengi yanayoshabihiana. Wawili hao ni kati ya makada saba waliosimamishwa na vyama saba kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ambao inaelekea kuwa ndiyo watakaochuana vikali, hasa kutokana na ukweli kuwa Dk Magufuli anatoka chama tawala na Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu, anaungwa mkono na vyama vinne vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Wengine wanaowania urais ni Mchungaji Christopher Mtikila wa DP, Chifu Lutayosa Chemba (ADC), Macmillan Limo (TLP), Hashimu Rungwe (Chauma), Fahami Dovutwa (UPDP) na mgombea wa ACT Wazalendo ambaye bado hajateuliwa. Pamoja na kwamba katika siasa lolote linaweza kutokea, wagombea hao watano hawatazamiwi kuweka ushindani mkubwa zaidi ya ule wa Dk Magufuli na Lowassa. Dk Magufuli hakutarajiwa kupita kwenye mbio za urais ndani ya CCM, ambako Lowassa na vigogo wengine walikuwa wakipewa nafasi kubwa, lakini ushindi wake umemfanya awe mgombea wa chama chenye mtandao mkubwa nchini na hivyo mwanzoni kupewa nafasi kubwa ya kushinda. Hata hivyo, uamuzi wa Lowassa kujivua uanachama wa chama kilichomlea na kilichompa umaarufu mkubwa, umebadili upepo na sasa vita ya kuingia Ikulu Oktoba 25 inaonekana kuwa ya watu hao wawili. Gazeti la Mwananchi linaangalia sifa ambazo wawili hao wanashabihiana pamoja na tofauti zao, kwa kuzingatia maelezo ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa. Wote wamesomea ualimu Moja ya mambo ambayo wawili hao wanashabihiana ni kusomea ualimu, ingawa wa fani tofauti. Dk Magufuli, ambaye atakuwa akitimiza miaka 56 siku nne baada ya Uchaguzi Mkuu, ni mwalimu aliyejikita kwenye masomo ya kemia na hesabu. Alipata diploma ya ualimu mwaka 1982 kwenye Chuo cha Elimu Mkwawa, kabla ya kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alipata shahada yake ya kwanza, ya umahiri na ya uzamiri akijikita kwenye somo la kemia. Lowassa, ambaye Agosti 26 atakuwa akitimiza miaka 62, alisomea shahada ya ualimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1977, lakini shahada yake ya uzamili ilijikita kwenye masomo ya maendeleo ya jamii. Dk Magufuli alitumia taaluma yake kufundisha kemia na hesabu kwenye Shule ya Sekondari ya Sengerema, lakini Lowassa hakufundisha. Wote ni makini Pengine ni kutokana na maadili ya ualimu, wawili hao wamedhihirisha kuwa ni watu makini katika utendaji wao, jambo ambalo limekuwa likiwafanya watu wanaofanya kazi chini yao kuwa na wasiwasi kila wanapowapeleka taarifa. Dk Magufuli na Lowassa hutumia muda mwingi kujiridhisha na taarifa wanazopelekewa kabla ya kufanya uamuzi ambao wakati mwingine huonekana kama wamekurupuka. Mhandisi mmoja ambaye amewahi kufungiwa leseni na Magufuli aliiambia Mwananchi kuwa kosa moja kubwa alilofanya ni kumwandikia Dk Magufuli taarifa ndefu, lakini iliyojaa mambo yasiyo sahihi. Anasema kuwa aya hiyo ilikuwa ukurasa wa 20, lakini ndani ya muda mfupi Magufuli aliibaini na kibarua chake kiliota nyasi. Hali ni kama hiyo kwa Lowassa, ambaye akiwa Waziri Mkuu aliwahi kumtimua mkandarasi wa Wilaya Temeke kwa kushindwa kukagua ujenzi wa maghorofa ikiwemo la Chang’ombe Village lililoporomoka na kusababisha maafa ya mtu mmoja na wengine kadhaa kujeruhiwa mwaka 2006. Uchapakazi Mbali na umakini, wawili hao wamedhihirisha kuwa ni wachapakazi hodari katika wizara na taasisi walizopitia kiasi cha kujijengea jina kubwa kwa wananchi. Utendaji wa Dk Magufuli hauna shaka na ameshaeleza bayana kuwa hapendi wazembe na wasiowajibika sanjari, kama Lowassa ambaye hata siku ya kwanza alipoingia ofisini mwaka 2005 aliwataka wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuacha kufanya kazi kwa mazoea. Wakati Dk Magufuli alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wengi walidhani kuwa amemaliza kisiasa, lakini mbunge huyo wa Chato alifanya kazi kubwa ya kutambua fursa za kiuchumi zilizoko hasa kwenye uvuvi na akafanikiwa kuonyesha ni kiasi gani Serikali ilikuwa ikipoteza fedha. Wakati huo, Tanzania iliingia makubaliano na Afrika Kusini na nchi nyingine za ukanda huu kufanya doria kwa pamoja kwenye pwani ya Afrika Mashariki na juhudi hizo zilifanikiwa kunasa meli ya Tawaliq 1 iliyokuwa na samaki wenye thamani ya Sh20 bilioni. Uchapakazi wake umedhihirika hasa kwenye ujenzi wa barabara, akiwa amefanikiwa kuunganisha takriban mikoa yote ya Tanzania katikja kipindi alichokaa Wizara ya Ujenzi. Lowassa anaonekana zaidi katika kusimamia utekelezaji wa mradi wa maji ya Ziwa Victoria katika shughuli za maendeleo baada ya mpambano mkali dhidi ya Misri, ambayo ilikuwa na ukiritimba wa maji hayo kabla ya nchi tano kuungana na kusaini makubaliano ya matumizi ya maji hayo. Lowassa pia anajinadi na mafanikio ya ujenzi wa shule za kata, ambazo kwa kiasi kikubwa zimefanikisha watoto wengi kupata elimu kwa gharama nafuu, ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ambao aliufanya kwa kukutanisha mifuko ya hifadhi ya jamii na kuiamuru ichangia gharama za ujenzi. Jambo lingine walilonalo Dk Magufuli na Lowassa ni misimamo. Dk Magufuli ni kiongozi mwenye misimamo isiyotia shaka na siku zote husimamia anachokiamini, sanjari na Lowassa, ni mwenye misimo yake na itakumbukwa alipokuwa Waziri wa Maji na baadaye Waziri Mkuu alionyesha misimamo. Dk Magufuli alitofautiana hata na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati aliposimamia uendeshaji wa kivuko cha Kigamboni, na suala la kiwango cha mizigo inayobebwa na malori. Moja ya kauli zilizonukuliwa sana ni ile ya “asiyekuwa na nauli ya kulipia kivuko, apige mbizi”, ambayo ilitafsiriwa kuwa ya kutojali wananchi, lakini faida zake ndio zinamfanya aonekane kuwa msimamo wake ulilenga kunufaisha wananchi. Hali kadhalika Lowassa anajulikana kwa kusimamia uamuzi kama wa kubomoa maghorofa yaliyojengwa kinyume na sheria Masaki jijini Dar es Salaam. Msimamo wake pia kwenye suala la mkataba wa City Water iliyokuwa ikihusika na ugavi wa maji jijini Dar es Salaam ndio uliosababisha uvunjwe. Ufuatiliaji Lowassa na Dk Magufuli pia wanajulikana kwa kuwa wafuatiliaji wazuri kwa watu walio chini yao au wanaofanya kazi chini ya mamlaka zao. Dk Magufuli, ambaye anajulikana kwa kukariri tarehe, kiwango cha miradi, urefu wa barabara na kiwango cha fedha zilizotengwa kwenye miradi, hutumia talanta hiyo kufuatilia miradi mbalimbali na hasa muda wa kumalizika, hali inayomfanya kila mara atishia kuvunja mikataba na wakandarasi au kuivunja kabisa. Hilo pia limekuwa likifanywa na Lowassa, ambaye akiwa Waziri Mkuu alikuwa akihakikisha wakuu wa wilaya na mikoa wako sehemu zao za kazi na yeyote ambaye alitaka kutoka alitakiwa awe na kibali, kwa mujibu wa baadhi ya watu waliofanya kazi naye. Udhaifu Mbali na sifa hizo nzuri, wanasiasa hao wanashabihiana katika udhaifu, hasa uamuzi wa papo kwa papo ambao pia husababishwa na kiu yao ya kutaka kuona kazi inafanyika. Wote wawili hufanya uamuzi wa papo kwa pamo ambao wakati mwingine huwa na athari za kisheria. Uamuzi kama huo huwa na kadhia kwa wafanyakazi na makandarasi wanaopewa zabuni mbalimbali na Serikali. Hawaachi mfumo wa utendaji Udhaifu mwingine wa wawili hao ni hali ya kujituma wao bila ya kutengeneza mfumo ambao unaendeleza ufanisi na badala yake wanapoondoka, hali hubakia kama ilivyokuwa awali. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Dk Magufuli kwenye wizara alizopitia kama ya uvuvi na hali kadhalika kwa Lowassa. Pia wanatofautiana Tofauti kubwa kati ya Dk Magufuli na Lowassa ni mgombea huyo wa CCM kutokulia ndani ya chama na badala yake amekuwa kwenye nafasi za utendaji zaidi na uwaziri. Dk Magufuli amekuwa mwanachama wa CCM na mbunge, nafasi ambayo humuingiza kwenye kikao cha Halmashauri Kuu pekee. Lakini Lowassa ameshika nafasi mbalimbali kwenye chama kuanzia katibu wa mkoa hadi mjumbe wa vyombo vya juu vya CCM. Kauli za wachambuzi Baadhi ya wachambuzi na wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (Udsm) wamesema kwa nyakati tofauti kwamba wagombea hao wanaonekana kuwa na tofauti kubwa zinazoweza kufanikisha ushindi katika uchaguzi huo. Mohammed Bakari, ambaye ni mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema wagombea hao wanafanana katika kigezo cha utendaji kazi lakini kiuamuzi na uzoefu wanatofautiana. “Dk Magufuli ana uamuzi wa kukurupuka ila Lowassa ametulia,” alisema. “Kuhusu uzoefu pia Lowassa ni mzoefu kiuongozi kuliko Dk Magufuli.” Alisema suala la uadilifu siyo rahisi kupata kiongozi mwadilifu kwa wagombea hao na bila kuzitaja kashfa hizo, alisema wote wana kashfa. Aliongeza kwamba, Lowassa ni mgombea anayeweza kuleta mabadiliko kwa Taifa hili, lakini Dk Maghufuli hawezi kutokana na mfumo uliopo kwenye chama chake. Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa wa Udsm, Dk Alexander Makulilo pia anaona sifa hizo zinazolingana. Alisema wagombea hao wanafanana kwa utendaji mzuri wa kazi na uamuzi wa papo kwa hapo. Aidha, alisema Magufuli ni kiongozi anayeweza kuleta siasa mpya zisizokuwa na makundi. Alisema Lowassa ni mgombea anayekabiliwa na changamoto ya Richmond iliyomfanya ajiuzulu uwaziri mkuu, wakati Dk Magufuli hana kashfa kubwa iliyowahi kujadiliwa bungeni. “Lakini hali hiyo haiwezi kuwa changamoto kubwa kutokana na mwamko mkubwa wa kundi linalohitaji mabadiliko ya uongozi serikalini. Uchaguzi huu ninaufananisha na Zambia wakati chama cha UNIP kilipoondolewa madarakani kwa kuwa makundi ya kijamii yalikuwa yameamua kiondoke madarakani,” alisema. Kuhusu mfumo kuibeba CCM, Dk Makulilo alisema ni sehemu ya changamoto kubwa inayoweza kufanikisha ndoto za Lowassa kuingia madarakani. Chanzo:BBC Swahili

Friday, August 7, 2015

Wasifu wa Lowassa

Umoja usio rasmi wa vyama vinne vya upinzani nchini Tanzania unajulikana kwa jina la Katiba ya Wananchi (UKAWA), baada ya kusubiri kwa muda hatimaye umemtangaza Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa urais. Lowassa anagombea kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huku vyama vingine vitatu vikimuunga mkono. Hii inatokana na sheria za Tanzania ambayo haitambui umoja wa vyama. Kabla ya kujiengua chama Tawala chama cha Mapinduzi CCM, Edward Lowassa amekuwa mwanachama wa CCM kwa muda wa miaka 38, ambapo alijiunga na chama hicho mara tu baada ya kumaliza elimu yake ya chuo kikuu mwaka 1977. Hatua ya mwanasiasa huyo mashuhuri nchini Tanzania kuamua kujiunga na chama cha upinzani Chadema, ikiwa imebaki miezi mitatu tu kuelekea uchaguzi mkuu, kumebadilisha kabisa upepo wa kisiasa nchini Tanzania, na hasa uchaguzi mkuu ujao. Lowassa alikuwa Maziri Mkuu kati ya mwaka 2005 na 2008 kabla ya kujiuzuLu wadhifa huo kufuatia sakata la kashfa ya rushwa iliyohusisha kampuni ya kuzalisha umeme ya ki-Marekani Richmond Development Company LLC ya Houston Texas. Hata hivyo wakati anatangaza kuhamia kwake Chadema, Lowassa alikanusha katu katu kuhusika kwa namna yoyote na kashfa hiyo na kudai kuwa yeye alifuata tu amri kutoka kwa ‘wakubwa’ walio juu yake. “Kama kuna mtu yeyote mwenye ushahidi basi na aende mahakamani ama sivyo anyamaze” alisema Lowassa “Kama kuna mtu yeyote mwenye ushahidi basi na aende mahakamani ama sivyo anyamaze” alisema Lowassa Kuhama kwake kunamfanya Lowassa kuwa ndie kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu kabisa wa CCM kukihama chama hicho tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania mnamo mwaka 1992. Mwanajeshi wa zamani na aliyewahi kupigana wa vita kati ya Uganda na Tanzania mwaka 1978/79, Lowassa aliiambia hadhara kwamba akiwa kama mtu mwenye uchungu na nchi yake isingekuwa rahisi kubaki ndani ya CCM huku akiona chama hicho kimepoteza mwelekeo na sifa ya kuongoza nchi. Lowassa amekimbilia upinzani baada jina lake kukatwa wakati alipoomba kuwa mgombea urais kupitia chama tawala CCM katika uchaguzi mkuu ujao utakafanyika mwezi Oktoba mwaka huu. Wakati mchakato wa CCM wa kumtafuta mgombea wao wa urais ulipoanza, Lowassa ndiye aliyekuwa kinara wa wagombea wote 42. Kila kona aliyozunguka, mikutano yake ya hadhara ilivutia maelfu ya watu waliomuunga mkono. Wakati chama cha CCM kilimtaka kila mgombea apate sahihi za wadhamini 450 lakini Lowassa alipata sahihi za wadhamini zaidi ya 700,000. Hata hivyo mchujo wa chama ulipofanyika jina lake lilikatwa mapema kabla hata ya kupelekwa kwenye vikao vya vya juu vya chama hicho. Ambapo baadae Waziri wa Ujenzi John Pombe Magufuli ndiye aliyeibuka kidedea na kuwa mgombea kupitia chama tawala CCM. Lowassa ameushutumu mchakato CCM wa kutafuta mgombea urais akiuita kuwa ulijaa chuki na mizengwe dhidi yake, hali ambayo aliifananisha na ‘ubakaji wa demokrasia’ “Nitakuwa mnafki nikisema bado nina imani na CCM. CCM niliyoiona Dodoma si CCM niliyokulia”, alisema, na kuongeza “kama Watanzania hawapati maendeleo kupitia CCM basi wakayatafute nje ya CCM” Wakati sakala la Richmond lilipoibuka miaka michache tu iliyopita, Chadema ilimfanya limsakama Lowassa kuwa ni mmoja wa mafisadi wakubwa nchini. Lakini wakati chama hicho kinamkaribisha kuwa mwanachama wao, kiligeuka na kusema hakuna mtu msafi nchini na kwamba hawawezi kuacha kumpokea mwanasiasa mwenye mtaji mkubwa wa wafuasi kama Lowassa. Wakati akiwa Waziri Mkuu, Lowassa alisifika kama mchapakazi hodari na msimamiaji wa moja kwa moja wa shughuli za serikali. Bado anaendelea kufahamika kwa jina la utani la ‘mzee wa maamuzi magumu’. Je unamfahamu Edward Lowassa ni nani katika siasa za Tanzania ? Moja ya mafanikio makubwa ya uwaziri mkuu wake ni jitihada kubwa na mafanikio ya upatikanaji wa fedha za kujenga chuo kikuu cha Dodoma. Chuo hiki kikuu cha umma kilichopo katikati ya Tanzania kilianzishwa mwaka 2007. Lowassa ni mashuhuri pia kwa kusimamia mpango wa serikali uliofanikiwa wa ujenzi wa shule za kata ambazo uliiletea Tanzania sifa kubwa kwa kutoa fursa ya watoto wengi kupata nafasi shuleni. Mtoto wa Mzee Ngoyai Lowassa, ambaye aliwahi kuwa mtumishi wa serikali ya kikoloni, Lowassa ameanza harakati zake za kuwania urais tangu mwaka 1995 lakini inaarifiwa kwamba rais wa kwanza wa Tanzania Mwl Julius Nyerere alimkatalia kushika nafasi hiyo. Wafuasi wa Lowassa wamekuwa wakiyatupilia mbali madai hayo Ulipofika uchaguzi wa mwaka 2005, Lowassa hakutaka kuwania urais, lakini badala yake alimnadi rafiki yake wa siku nyingi Rais wa sasa Jakaya Kikwete ambaye alipata ushindi wa kishindo wa zaidi ya asilimia 80.

Tuesday, August 4, 2015

Chadema yamweka pembeni Dk Slaa

Baraza Kuu la Chadema limeridhia Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa apumzike wakati chama hicho kikiendelea na mchakato wa Uchaguzi Mkuu baada ya kiongozi huyo kutofautiana nao katika uamuzi wa kumkaribisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa. Baraza hilo jana lilipiga kura ya wazi huku likishauri kuwa endapo atafikiria kubadili uamuzi wake, atarejea kuendeleza safari ya chama hicho kuelekea Ikulu chini ya mwavuli wa Ukawa. Uamuzi huo ulifikiwa jana wakati wa kikao cha Baraza Kuu kilichofanyika hapa baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kueleza tofauti iliyojitokeza mwishoni mwa mchakato wa kumpokea Lowassa baina ya Dk Slaa na Kamati Kuu kiasi cha kumfanya Katibu Mkuu huyo kutohudhuria baadhi ya shughuli muhimu za chama. Mbowe alisema Kamati Kuu ilifanya vikao kadhaa kutafakari ujio wa Lowassa na mashauriano ya muda mrefu ambayo hayakuwa rahisi kufikia uamuzi wa pamoja. “Tulifanya mashauriano yaliyoambatana na hali ya kitafiti na tukaridhika pasipo shaka kwamba ujio wa Lowassa na wenzake katika chama hiki ni mpango wa Mungu ambao tunatakiwa tuunge mkono, utusadie kuwaunganisha wenzetu wa CUF, NLD na NCCR-Mageuzi na Watanzania wote kufikia malengo ya pamoja,” alisema. “Katika hatua zote hizo tulikuwa sambamba na Dk Slaa lakini katika dakika za mwisho akatofautina kidogo na Kamati Kuu.” Maelezo hayo ya Mbowe yanamaliza sintofahamu iliyokuwa imetanda kwa makada wa Chadema juu ya sababu za Dk Slaa kutoonekana kwenye hafla ya kumpokea Lowassa Julai 28, wakati wa kuchukua fomu za kugombea urais Julai 30, siku aliporudisha fomu Agosti Mosi na kwenye vikao vya Sekretarieti na Kamati Kuu juzi. Mbowe ambaye pia ni Kiongoni wa Upinzani Bungeni alisema: “Kwa hiyo tumekubaliana na Katibu Mkuu apumzike kwa muda na nina hakika kwa tabia na hulka za Dk Slaa… kwa sababu anajua tunampenda na yeye anakipenda chama hiki, tunamwombea kwa Mungu ampe nguvu na ujasiri wa kuona kwamba kauli ya wengi ni kauli ya Mungu. “Tutaendelea kuongea naye, bado nafasi yake ipo na kwa wengine wote wenye hofu ya aina hii na naomba niseme kuwa nafasi zetu za kiuongozi au kiuchaguzi ni dhamana, hakuna yeyote mwenye hatimiliki na nafasi mliyonayo ni kwa sababu ya watu, tukielewa hivyo wala hatuna ugomvi.” Huku akizungumza kwa hisia, Mbowe alisema kauli yake ni uamuzi wa vikao vya chama na kwamba hakuna ugomvi wowote na kiongozi huyo, hivyo makada na Watanzania waachane na uzushi wa mitandaoni akisema hofu kama ya Dk Slaa ipo pia kwa makada wengine na kwamba ilikuwa na mashiko na inayozungumzika, lakini wasingezuia matakwa safari ya mamilioni kwa “sababu ya matakwa ya Mbowe au Slaa... tunasema lazima tuendelee kwa sababu uchaguzi upo kesho.” Katika hotuba hiyo ya dakika 35, Mbowe alisema Dk Slaa ni kiongozi ambaye wanamheshimu, wanampenda na wataendelea kumpenda siku zote kwa sababu chama chao ni cha kujengana na siyo kubomoana. Ili kupitisha uamuzi huo, Mbowe aliwahoji wajumbe wa baraza hilo iwapo wanataka waendelee na kazi au wasubiri ili kila mmoja afanye uamuzi wake binafsi na kujibiwa “tuendelee…” Aliuliza swali hilo mara mbili na kuungwa mkono na wajumbe wote kwa sauti kubwa na alipowataka wajumbe wanaounga mkono uamuzi huo wasimame, walifanya hivyo na kuimba wimbo wa chama “Chadema, Chadema…people’s power.” Alisema amezungumza suala hilo mbele ya wanahabari ili kama kuhukumiwa, ahukumiwe kwa sababu wajibu wake akiwa kiongozi ni kusema ukweli daima. Aliwataka makada wa Chadema wawe na amani na kwamba chama hicho kipo salama na wanaofikiri kitameguka ni ndoto za mchana. “Wengine wakasema Lissu (Tundu) huyoo, wakahamia Mnyika (John), Mnyika alikuwa mgonjwa, huyoo… mtasema na Slaa amesharudisha na gari mtakuta Jumatatu huyooo, lakini kwa leo amepumzika mzee wangu,” alisema Mbowe na kushangiliwa. Mwenyekiti huyo aligusia moja ya ajenda ya mkutano wa Baraza Kuu kuwa ilikuwa ni kujadili ilani ya uchaguzi kabla ya kupitishwa leo na mkutano mkuu. Baada ya mkutano huo, kuanzia kesho kwa siku tatu mfululizo chama hicho kitakuwa na vikao vya Kamati Kuu kuteua majina ya wabunge na wawakilishi watakaosimamishwa na chama hicho. Hofu ya Lowassa Akizungumzia hofu iliyotanda baada ya Lowassa kujiunga na chama hicho, Mbowe alisema kila jambo jema mara nyingi hujitokeza likiwa na changamoto. Alisema baada ya kutambulishwa kwa Lowassa, hofu ilionekana kutanda ndani ya wajumbe wa Mkutano Mkuu na Baraza Kuu kwa kuhofia nafasi za uongozi na hatima ya chama hicho. “Lakini inawezekana hofu hiyo wameipata zaidi CCM, kwa kipigo ambacho wamekipata hakijawahi kutokea katika historia ya siasa nchini, hali hii inataka kufanana na kuondoka kwa Augustino Mrema lakini naweza kuilinganisha nguvu ile kwa asilimia 25 tu na nafasi ya kuondoka Lowassa.” Kuhusu madai ya kupokea mafisadi ndani ya chama, Mbowe alisema katika mazingira yoyote kwa mwanasiasa anayetafuta mbadala wa chama, lazima atakifikiria Chadema kwa sababu ni chama kilichojijengea msingi. Alisema ilikuwa ni lazima kwa chama kuweka mkakati wa kumpokea mwanasiasa yeyote atakayekuwa tayari kuingia. “Kwa mpango huohuo wa Mungu, leo yamejitokeza makundi yameingia ndani ya chama na miongoni mwao aliyekuwa anawika sana ni Lowassa... sasa katika siasa kuna kitu kinaitwa ‘game change’, yaani kwamba siasa zinaelekea mrengo huu halafu ghafla zinageuka na kuelekea mrengo mwingine, hiyo ndiyo ‘dynamism’ ya siasa. “Hatuwezi kufunga milango ya chama kwa kuhofia nafasi zetu za uongozi, eti nafasi ya mwenyekiti, udiwani itachukuliwa...je, tutakuwa tunajenga chama? “Hali hiyo ndiyo imekuwa sababu vyama vingi vilijisahau na kuendekeza masilahi binafsi wakasahau masilahi mapana ya chama. Kila mwanachama anaheshimika katika nafasi yake ndani ya chama. Kwa hivyo fursa iliyojitokeza usipoitumia utakuwa ni mwendawazimu.” Mwalimu abeba mikoba ya Dk Slaa Chama hicho kimemkaimisha Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu nafasi ya Dk Slaa na papo hapo, Mwalimu aliwaeleza wajumbe kuwa hotuba maalumu ya Katibu Mkuu itatolewa leo wakati wa mkutano mkuu. “Lazima mjue tunakwenda kuwa chama tawala, hivyo hakuna kiongozi mdogo wala hakuna mwanachama aliye mdogo ndani ya chama hiki, kila mwanachama mmoja atakuwa na thamani, hivyo mjilinde msije kunufaisha maadui zetu,” alisema Mwalimu. Msindai atua Chadema Mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM, Mgana Msindai jana alijiunga na Chadema na kutambulishwa katika mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho. Mgana, ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Iramba Mashariki (2000-2010) alitambulishwa pamoja na Mbunge wa Arumeru Magharibi (CCM), Goodluck Ole Medeye na ofisa mwandamizi wa chama hicho, Matson Chizii. Makada hao wa CCM jana usiku waliambatana katika kikao hicho na aliyewahi kuwa waziri mkuu Edward Lowassa. Habari zinasema kuna makada zaidi wa CCM wakaotambulisha katika mkutano mkuu wa Chadema leo. Chanzo:mwananchi.co.tz

Rais Nkurunziza aomba utulivu Burundi

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza ameomba utulivu baada ya wapiganaji waliovalia magwanda ya kijeshi kumuua mmoja ya majenerali walio na ushawishi mkubwa serikalini. Katika hotuba kwa taifa muda mchache tu baada ya shambulio hilo,Nkurunziza aliomba utulivu akisema kuwa kisasi kitamaliza kizazi chote. Hizi ni baadhi ya nukuu za hotuba hiyo. ''Burundi imempoteza mtumishi mkubwa ,jenerali Adolphe Nshimirimana alikuwa alifanya kazi kwa bidii.Natoa wito kwa idara ya usalama kuanzisha uchunguzi ndani ya wiki moja ili wahalifu watambuliwe na kushtakiwa.Nawataka raia wote wa Burundi kuwa watulivu na kuungana.'' Chanzo:BBC Swahili

YALIYOSEMWA NA MBOWE HII LEO WAKATI AKIFUNGUA MKUTANO WA BARAZA KUU CHADEMA

Mbowe-Tumekubaliana na Katibu Mkuu apumzike kwa muda, kwamba sis tuendelee na atakapokuwa tayari ataungana nasi mbele ya safari. Chama hiki hatukiendeshi kwa siri, tunakiendesha kwa mikakati. Tulilazimika kutumia kila mbinu halali ambayo inakiwezesha chama chetu kusaka matumaini na matarajio ya wananchi. Tuliridhika pasipo shaka kwamba ugeni wa Edward Lowassa katika chama chetu ni mpango wa Mungu. Umoja wetu ndio ushindi, fursa iliyojitokeza ni nadra. Mtikisiko huu umekuja kwa CCM kipindi ambacho Watanzania wanamatamanio ya mabadiliko. Hatuwezi kuwa chama cha kuendelea kuhubiri mabaya ya jana tukashindwa kuhubiri maendeleo ya kesho. Kipigo wanachopata CCM, hawajawahi kukipata tangu tuanze siasa za vyama vingi. Kila tunayeweza kumpokea kutoka vyama vilivyo nje ya UKAWA tutamchukua. Mungu ameamua kutumia chama chetu kujeruhi na kuangusha CCM. CHADEMA ni chama cha siasa, ni chama makini, chama makinI ni chama cha watu, chama kisichokuwa makini ni chama cha viongozi. Chanzo:frankleonald info

Monday, August 3, 2015

Binti wa Sokoine atwaa mikoba ya Lowassa

Binti wa Waziri mkuu wa zamani, Edward Sokoine, Namelock Sokoine ameshinda kura za maoni kugombea ubunge Jimbo la Monduli kupitia CCM huku mkwe wa Lowassa, Siyoi Sumari akishindwa Jimbo la Arumeru Mashariki. Namelock ambaye ni mbunge wa Viti Maalumu (CCM) alipata kura 29,582 akifuatiliwa na Loota Sanare aliyepata kura 8,809 na nafasi ya tatu, ilichukuliwa na Lolinyu Mkoosu aliyepata kura 235 na Payani Leyani akipata kura 226. Arumeru Mashariki: Sumari aliyewania jimbo hilo kwa mara ya kwanza baada kifo cha baba yake Jeremia Sumari na kushindwa na Joshua Nassari wa Chadema alipata kura kura 3,664 dhidi ya 12,071 za John Pallangyo. Mshindi wa tatu alikuwa ni William Sarakikya ambaye alipata kura 3,552 na wagombea hao waliwaacha mbali wapinzani wao wengine wanne. Arusha Mjini: Katika Jimbo la Arusha Mjini, mfanyabiashara Philemon Mollel ameshinda kwa kura 5,320, akifuatiliwa na mfanyabiashara mwingine Justine Nyari aliyepata kura 1,894 na nafasi ya tatu, ilichukuliwa na Moses Mwizarubi aliyepata kura 1,205. Karatu: Dk Willibrod Lorry alishinda baada ya kupata kura 17,711, Rajabu Malewa (911), John Dado (745) na Joshua Mwambo (67). Masele ambwaga Mlingwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Steven Masele amembwaga waziri mwingine wa zamani, Dk Charles Mlingwa baada ya kupata 70,900 dhidi ya 669 za mpinzani wake. Wagombea wengine Abdallah Seni alipata kura 391, Erasto Kwilasa (232), Hassan Athuman (164), Mussa Ngangala (116), Hatibu Malimi (69), Wille Mzava (65) na Tara Omari (43). Ushetu: Elias Kwandikwa (11,554) Isaya Sino (5,241) na Elfaidi Sikuli (2,007). Kahama Mjini: Jumanne Kishimba (9,754), Kintoki Godwin (433), Nkuba Charles (389), Bundala Maiko (284), Sazia Robert (257), Kapela Robert (135), Ngalawa Adamu (126), Luhende Jerard (106), Malele Charles (91), Tunge John kura (78), Mpangama Deogratias (57), Machunda Eliakimu (56), Masanja Andrew (48) na Kambarage Masusu (28). Msalala: Ezekiel Maige (11,575), Emmanuel Kipole (1,197), John Sukili (962), Nicholas Mabula (668), Maganza Mashala (597), John Lufunga (29) na Wankia Welema (14). Solwa: Mbali ya matokeo ya kata moja ambayo imerudia uchaguzi, Ahamed Salum alikuwa akiongoza kwa kura 17,485 akifuatiwa na Amos Mshandete (2,028), Cyprian Mhoja (1,586), Luhende Richard (1,273), Kasile Paul (637), Gabriel Shija (361), Renatus Chokala (357) na Hosea Somi (255). Kishapu: Kabla ya matokeo ya kata tatu, Suleiman Nchambi alikuwa akiongoza kwa kura 13,443, William Bonda (6,143), Kishiwa Kapale (500), Limbe Moris (393), Heke Bulugu (356) na Timoth Ndanya (193). Mawaziri watamba Kanda ya Ziwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani ameshinda kura za maoni Jimbo la Busega baada ya kupata kura 10,697 dhidi ya mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Dk Rafael Chegeni aliyepata kura 9,661. Buchosa: Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba ameibuka mshindi kwa kupata kura 26,368 dhidi ya Eston Majaliwa aliyepata 9,213. Misungwi: Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga ameibuka mshindi kwa kura 26,171, akimwangusha Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Jacob Shibiliti aliyepata kura 7,009. Shomari Chalamila alipata kura 1,840, Dk Makene Doshi (1,339), Cleophace Jerome (1,051). Ilemela: Mkuu wa Wilaya ya Iringa Angelina Mabula ameibuka mshindi katika Jimbo la Ilemela kwa kupata kura 6,324 mbele ya Barnabas Mathayo (3,562), John Buyamba (1,167) na wagombea wengine 16. Tabora Kaskazini: Almasi Maige (9,466), Shaffin Sumari (6,392) na Joseph Kidawa (5,965). Bariadi: Andrew Chenge (20,200), Masanja Kadogosa (2,986) na Cosmas Manula (270). Meatu: Salum Mbuzi (13,180), Oscar Maduhu (2,988), Romano Thomas (358) na Donard Jinasa (350). Itilima: Njallu Daudi (44,486), Simon Ngagani (2,759) na Danhi Makanga (814). Chanzo:mwananchi.co.tz

Mawaziri watano waanguka kura za maoni

Kishindo cha kura za maoni ndani ya CCM kimeendelea kuwakumba baadhi ya vigogo wa chama hicho baada ya jana mawaziri wengine watano kuanguka. Miongoni mwao ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe aliyekuwa akiwania kupitishwa tena kugombea tena ubunge wa Nachingwea. Chikawe ambaye pia alishindwa katika kinyang’anyiro cha urais kupitia chama hicho, alidondoshwa na Hassan Masala aliyepata kura 6,494 akifuatiwa naye akipata 5,128. Wagombea wengine ni Steven Nyoni (1,438), Amandus Chinguile (1,274), Fadhili Liwaka (1,171), Benito Ng’itu (797), Greyson Francis (671), Albert Mnali (763), Issa Mkalinga (466), Mustafa Malibiche (427) na Ali Namnjundu (319). Mbali ya Chikawe pia manaibu waziri wanne wameangushwa katika kura hizo. Hao ni Mahadhi Juma Maalim (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), Perera Ame Silima (Mambo ya Ndani), Amos Makala (Maji) na Saning’o ole Telele (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi). Mahadhi alianguka katika Jimbo la Paje, Zanzibar kwa kupata kura 1,785 huku Jaffar Sanya Jussa ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) Mkoa wa kusini akiibuka mshindi kwa kura 3,368. Silima aliyepata kura 1,218 katika Jimbo la Chumbuni alibwagwa na mpinzani wake, Ussi Pondeza aliyepata kura 1,952. Katika Jimbo la Mvomero, Suleiman Murad alishinda kwa kura 13,165 dhidi ya Makalla ambaye alikuwa anatetea jimbo hilo akipata 10,973. Ole Telele alipata kura 5, 126 huku William ole Nasha akiibuka mshindi kwa kura 23, 563 akifuatiwa na Elias Ngolisa aliyepata 11, 442 na Dk Eliamani Lalkaita 7,135. Matokeo hayo hayakujumlisha kura za matawi matano ambayo Katibu wa CCM Wilaya ya Ngorongoro, Elihudi Shemauya alisema hayawezi kubadili matokeo. Katika Jimbo la Uzini, Katibu wa Oganizesheni wa CCM, Muhammed Seif Khatib ameshindwa baada ya kupata kura 1,333 huku mpinzani wake Salum Mwinyi Rehani akiibuka kidedea kwa kura 1,521. Kigogo mwingine wa CCM, Nape Nnauye ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi, ameshinda kura hizo Jimbo la Mtama kwa kura 9,344 dhidi ya mpinzani wake Selemani Methew aliyepata kura 4,766. Jimbo la Chwaka mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 20, Yahya Kassim Issa aliangushwa baada ya kupata kura 1,572 dhidi ya mpinzani wake, Baguwanji Mensuriya Baguwanji aliyepata kura 1,951. Wakati mawaziri hao wakianguka, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alishinda katika jimbo jipya la Welezo huku Waziri wa Ulinzi, Hussein Mwinyi akishinda katika Jimbo la Kwahani. Aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM, Masauni Hamad Masauni ameshinda Jimbo la Kikwajuni kwa kura 2,222 dhidi ya mpinzani wake, Mussa Shaali Choum aliyepata kura 461. Katika Jimbo la Jang’ombe, Ali Hassan Omar ameibuka mshindi kwa kupata kura 879 dhidi ya mpinzani wake Abdullah Hussein Kombo (639). Aliyekuwa Waziri Kiongozi Zanzibar na waziri wa zamani wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha aliibuka mshindi katika Jimbo la Kijito Upele. Jimbo la Malindi Abdullah Juma Abdulla alishinda kwa kura 558 dhidi ya mpinzani wake, Kombo Mshenga Zubeir aliyepata kura 241. Jimbo hilo nafasi ya uwakilishi, Mohammed Ahmada Salum alishinda kwa kura 336 na dhidi ya Abdulrahman Hassan (271). Majimbo mengine Liwale: Faith Mitambo (7,238), Zainabu Kawawa (3,126). Ruangwa: Naibu Waziri (Tamisemi), Kassim Majaliwa (11,988), Bakari Nampenya (2,678). Kilwa Kaskazini: Murtaza Mangungu alishinda kwa kura 7,140. Kilwa Kusini: Hasanain Dewji ameshinda kwa kura 3,859. Lindi Mjini: Hassani Kunje (3,428) Mohamedi Ulthali (2,314). Jimbo la Mchinga: Said Mtanda ameshinda kwa kura 3,101, Riziki Lulida (2,217). Serengeti: Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Kebwe Steven Kebwe aliibuka mshindi kwa kura 29,268 akiwashinda, Dk James Wanyancha (5,980) na Mabenga Magonera (1,638). Nyamagana: Aliyekuwa Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula ameibuka mshindi kwa kura 9,553, Joseph Kahungwa (3,947) na Raphael Shilatu (894) na kufuatiwa na wenzao 17. Ukerewe: Christopher Nyandiga aliongoza kura 8,077, Gerald Robert (142), Laurent Munyu (197), Emmericiana Mkubulo (242), Bandoma Kabulule (414), Bigambo Mtamwega (477), Dk Elias Missana (648), Hezron Tungaraza (693), Dk Deogratias Makalius (727), John Mkungu (775), Osward Mwizalubi (1,098), Maliki Malupu (1,443), Deogratias Lyato (1,824), Sumbuko Chipanda (2,016) na Magesa Boniphace (2,552). Morogoro Mjini: Abdulaziz Abood amepata kura 20,094 na Simon Berege (429). Mikumi: Jonas Nkya alipata kura 947 ameshinda dhidi ya Abdulsalum Sas (544). Kilombero: Mbunge wa jimbo hilo, Abdul Mteketa alianguka baada ya kushika nafasi ya tatu kwa kupata kura 2,646 nyuma ya Abubakar Assenga aliyepata kura 6,629 na Abdul Liana 3,999. Mlimba: Godwin Kunamba ameshinda kwa kura 6,233 Dk Fredrick Sagamiko (2,203), Jane Mihanji (2,073). Gairo: Mbunge wa sasa, Ahmed Shabiby alishinda kwa kura 15,920 akifuatiwa na Omari Awadhi 886. Morogoro Kusini Mashariki: Omary Mgumba alishinda kwa kura 3,393 akifuatiwa na Jamila Taji (2,914) na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Dk Lucy Nkya (1,710). Msoma Vijijini: Profesa Sospeter Muhongo aliibuka mshindi kwa kura 30,431 waliofuatia ni Anthony Mtaka (3,457), Evarest Mganga (2,556), Profesa Edson Mjungu (898), Mafuru Mafuru (421), Wits Onyango (392) na Nelson Semba (186). Butiama: Nimrodi Mkono ameshinda kwa kupata kura 19,366, Chirstopher Siagi (2,457), Samweli Ndengo (745), Jacob Thomas (502), Mwita Wariuba (1,346), Moringe Magige (317), Godfrey Wandiba (303), Joseph Nyamboha (262) na Samweli Gunza (73). Musoma Mjini: Vedastus Mathayo alishinda kwa kura 6,691 akifuatiwa na Paul Kirigini (1,174), Dk Msuto Chirangi (1,082), Juma Mokili (681), Deus Mnasa (378), Nicodemus Nyamajeje (183), Emmanuel Mwita (155), Felix Mboje (131) na Zerulia Mneno (61). Kyela: Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe ameshinda kwa kupata kura 15,516, George Mwakalinga (4,905) na Martin Kipija (2,301). Njombe Kusini: Edward Mwalongo (3,870), Romanus Mayemba (2,153), Daniel Msemwa (1,976), Arnold Mtewele (1,136), Alfred Luvanda (978), Hassan Mkwawa (152), Vitalis Konga (76) na Mariano Nyigu (86). Makambako: Deo Sanga (7,643) Alimwimike Sahwi (499). Ludewa: Deo Filikunjombe kabla ya kata tatu alikuwa na kura18,290 akiwaacha Kapteni Jacob Mpangala (205) na Zephania Chaula (770). Wanging’ombe; Gerson Lwenge kabla ya kata tatu alikuwa na kura 11,322, Thomas Nyimbo (1,871), Yono Kevela (1,819), John Dugange (466), Richard Magenge (417), Abraham Chaula (382), Kennedy Mpumilwa (332), Hoseana Lunogelo (322), Malumbo Mangula (304), Nobchard Msigwa (216), Abel Badi (106) na Eston Ngilangwa (47). Kiteto: Mjumbe wa NEC, Emmanuel Papian ameshinda kwa kupata kura 40,636 mbunge aliyemaliza muda wake Benedict Ole Nangoro (21,461), Amina Said Mrisho (2,118), Ally Lugendo (287) na Joseph Mwaseba (250). Bunda Mjini: Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira ameshinda kwa kupata kura 6,429 dhidi ya kura 6,206 alizopata mshindani wake wa karibu, Robert Maboto. Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Christopher Sanya alipata kura1,140, Exavery Lugina (846), Simon Odunga (547), Magesa Mugeta (446), Peres Magiri (385) na Brian Bitta (263). Handeni na Bumbuli Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia January Makamba wameshinda katika mchakato wa kura za maoni katika majimbo ya Handeni na Bumbuli. Chanzo:mwananchi.co.tz

Sunday, August 2, 2015

MAONI YA DR LWAITAMA KUHUSU UKAWA

Historia inaonesha kuwa vipindi fulani katika mstakhabali wa nchi unalazimisha kupima nini ni janga zaidi ya jingine. Marehemu Samora Machel na Frelimo walikubali kutia saini Mkataba wa Nkomati wa ushirikiano na Makaburu kama mkakati wa kujinusuru na kutoa nafasi kukabiri janga kubwa kuliko zote wakati huo la kuondolewa serikali ya Frelimo na Renamo ikisaidiwa na Makaburu. Wakomunisti wa Afrika ya Kusini waliingia ubia na ANC ya mabweneyenye weusi ili kutokomeza kwanza ukaburu na mapambano na ubepari yaje baadaye. Katika Vita Kuu ya Dunia ya Pili wakomunisti walishirikiana na mabwenyenye wa mrengo wa kulia na kati kutokomeza janga kubwa zaidi wakati huo la ufashisti, yaani ubepari wa mrengo wa wa kulia kupitiliza. Hivyo hivyo mapambano ya kuleta uhuru wa Tanganyika yalivyo unganisha nguvu za mabwenyenye wazungu na waasia pamoja na zile za wakulima na wafanyakazi wa rangi zote kwa azimio lile la mkutano wa mkuu wa Tanu wa 1958 pale Tabora. Hivyo hivyo Mandela na ANC waliingia "urafiki wa mashaka" na De Clerk kiongozi wamakaburu ili kuondolewa ukaburu kuwe kwa amani ya "kula matapishi" ya kuwalaani huko nyuma kuwa ni wabaya wa Mwaafrika!! Mabadiriko ya haraka haraka yanayoendelea hapa Tanzania yenye lengo la kuondoa CCM madarakani kama chama dola kinachodumaza na kudhoofisha ushindani wa kisiasa miongoni mwa mabwenyenye watabaka tawala Tanzania ni mbadiliko yatayoleta neema kwa Watanzania wote. Ile tu CCM kudhoofishwa na kujiunga UKAWA kwa Lowasa ni kuvuja kwa pakacha ambayo ni nafuu ya mchukuzi.....Nikuondoa kizingiti kikuu cha kushamiri kwa demokrasia pana na maendeleo endelevu Tanzania ambacho ni kuhodhiwa na ukiritimba wa chama dola cha CCM kinachojinadi kama chama cha mrengo wa kushoto wakati ni chama cha mrengo wa kulia kama vyama vyote vya siasa Tanzania kwa sasa. Kumeguka kwa CCM-Mambo Leo kama taasisi ya kakundi kawana mtandao ulioingiza serikali ya sasa ya Tanzania madarakani mwaka 2005 ni faraja kwa wote wenye kuitakia mema nchi hii na ni kiashiria cha kukomaa kwa vuguvugu la ukombozi wa pili wa Tanzania utakao chukua sura ya demokrasia zaidi ilikuwa na na maendeleo endelevu zaidi yapatikane kupitia kupatikana nafasi chanya zaidi ya kupitishwa kwa Katiba Mpya kama ilivyopendekezwa ndani ya Rasimu ya Pili ya Tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Warioba. Kwa mara ya kwanza vyama vy siasa vya upinzani kiuhalisia ( tofauti na vile ambavyo vimebebwa na watawala wa sasa kwa lengo la kuua upinzani wa kisiasa kijanja kijanja kama ACT- Wazalendo) sasa vimeunganishwa na kupigania Katiba Mpya iliyotokana na maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Jaji Warioba ( UKAWA) badala ya kuunganishwa na kutaka kuondoa CCM madarakani pekee. Ghafla mwanasiasa mwenye nguvu nyingi ndani ya chama cha kifisadi cha CCM, mwanasiasa ambaye umaaarufu wake umetokana na kuongoza mtandao uliouweka utawala wa sasa wa CCM madarakani, Ndugu Edward Lowasa, amekasirishwa na kukatwa jina lake na aliodhani ni rafiki zake ndani ya CCM na kuamua kusema basi na lolote liwe kwa kujiunga na vuguvugu la kupigania katiba mpya!! Naye sasa kang'amua kuwa Katiba ya sasa na ile Pendekezwa ni za ovyo maana haziruhusu kuwepo mgombea huru bila mizengwe. Hasira za Lowasa zimezaa tunda zuri la kug'amua kuwa Watanzania wanaitaji mabadailiko kupitia Katiba Mpya iliyobebwa ndani ya Rasimu ya Pili ya Tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Warioba. Hasira hizi za mkizi ni furaha ya kunguru na ni busara kwa viongozi wa Chadema na UKAWA kwa ujumla kutoongopa "kula matapishi yao" kwa kumkaribisha Ndugu Lowasa ...huyu huyu waliomwita fisadi... kujiunga na UKAWA na kugombea urais. Nafasi ya kihistoria imejitokeza ya kukiondoa CCM madarakani kwa amani!! Sishangai wasaliti wa vuguvugu la kukiondoa CCM madarakani wanatushauri sisi Watanzania wenye shauku ya kuutumia upenyo huu wa mpasuko ndani ya CCM kukiondoa CCM madaraka!!!Eti tuombe radi kwa" kula matapishi yetu" wote tulio wahi kumwita Lowasa fisadi! Wao wanataka tuendelee kuvumilia kutawaliwa na CCM labda kwa miaka mitano au zaidi hivi mpaka chama kipya cha watakatifu kiitwacho ACT-Wazalendo kitakapo kuwa tayari kututawala badala ya CCM!! Sishangai kusikia ushauri huu kutoka kwa wasaliti hawa ambao kazi yao hata huko nyuma imekuwa nikuudhoofisha upinzani dhidi ya CCM na kukisaidia CCM kiendeleee kuwa madarakani!! Hawa jamaa ni wasomi sana na ni wajanja sana, ilo lazima kulikiri!!! Sitashanga kama haya ninayoyasema yatapigwa madogo na wasaliti hawa!! Historia itakapoandikwa baada ya UKAWA kupata viti vingi zaidi Bunge lijalo au hata kuuchua urais na kupata Katiba Mpya iliyobebwa ndani ya Rasimu ya Pili ya Tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Warioba itawapa hukumu yao stahiki, wajanja na welevu hawa! Bila shaka wanaoomba UKAWA ishindwe kupata viti vingi Bunge lijalo na iukose urais na hivyo tuendelee kutawaliwa na CCM na wao wapate viti vya kutosha kuwa viongozi wakuu wa eti upinzani muruwa wenye maadili ya Azimio la Arusha Tanzania!! Ni haki yao ya binadamu kuendelea na matumaini haya kama na sisi tulivyo na haki ya kuendelea na matumani yetu ya uwezakano wa ushindi mnono chini ya UKAWA dhidi ya ukiritimba wa chama kimoja chama dola cha CCM! Mwl. Lwaitama Chanzo:chadema blog

Watu milioni 1.6 wamdhamini Lowassa

Kada mpya wa Chadema, Edward Lowassa jana amerejesha fomu ya kuwania urais, huku akifanikiwa kupata wadhamini milioni 1.6, zaidi ya nusu ya kura za urais ambazo chama hicho kilipata kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2010. Naibu katibu mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu alisema idadi hiyo ya wadhamini inaashiria ushindi wa kishindo, kwa maelezo kuwa inakaribia idadi ya kura alizopigiwa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alipogombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Katika Uchaguzi huo, Dk Slaa alishika nafasi ya pili baada ya kupata kura 2,271,941 sawa na asilimia 26.34, huku Rais Jakaya Kikwete akipata kura 5,276,827 sawa na asilimia 61.17. Lowassa alipochukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwania urais kwa tiketi ya CCM, kabla ya kuhamia Chadema, alidhaminiwa na wanachama 870,000 nchi nzima. Dk Slaa, ambaye hajaonekana hadharani tangu Lowassa ajiunge Chadema, jana hakuwapo kwenye ofisi za chama hicho wakati mbunge huyo wa Monduli alipokuwa akirejesha fomu. Hakuna kiongozi aliyekuwa tayari kuzungumzia suala lake, lakini baadhi ya maofisa wa Chadema walisema wanaendelea kuchapa kazi. Kama ilivyokuwa juzi katika hafla fupi wakati Lowassa akichukua fomu, umati mkubwa ulifurika na kusababisha Mtaa wa Ufipa uliopo Wilaya ya Kinondoni kufungwa, watu walijazana tena na safari hii umati huo ukiwa umebeba mabango ya kumsifu Waziri Mkuu huyo wa zamani. Katika hafla ya jana, makamu mwenyekiti wa Chadema-Bara, Profesa Abdallah Safari alieleza jinsi Chadema ilivyojipanga kuchukua nchi na siyo kushinda ubunge na udiwani pekee na kwamba Lowassa amebakiza hatua mbili tu kuingia Ikulu, jambo walilodai kuwa limeichanganya CCM. Wakati Lowassa ambaye alitangaza rasmi kujiondoa CCM na kujiunga na Chadema Julai 28 mwaka huu akisubiri kupitishwa na Mkutano Mkuu wa chama hicho utakaofanyika Agosti 4, habari za ndani zinaeleza kuwa vigogo kadhaa wa CCM watatambulishwa katika mkutano huo. Habari hizo zinaeleza watakaotambulishwa siku hiyo ni wenyeviti wa CCM wa mikoa, wilaya na waliokuwa wabunge wa chama hicho ambao wanamuunga mkono Lowassa. Jana Lowassa, aliyekuwa amevaa shati jeupe na suruali nyeusi na aliyekuwa katika gari aina ya Toyota Land Cruiser VX, alifika makao makuu ya Chadema saa 9:35 alasiri akiwa pamoja na familia yake na alipokewa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali. Baadhi ya ujumbe huo ni “Chini ya Lowassa umaskini haupo”, “Kwa Lowassa hata maskini atapata ajira” na “Kingunge Ngombare-Mwiru karibu Ukawa”. Kingunge ni kada mkongwe wa CCM na anamuunga mkono Lowassa. Mbali na kubeba mabango, watu hao walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kumsifu Lowassa na kushangilia pale ilipokuwa ikitajwa mikakati ya chama hicho kushika dola. Kura milioni 1.6 Akieleza taratibu na kanuni za kudhamini mgombea urais, mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaira alisema mgombea urais anatakiwa kudhaminiwa na wanachama wasiopungua 200. “Naamini fomu za Lowassa zitakuwa na idadi hiyo ya wadhamini. Ila baada ya mgombea kuchukua fomu jioni yake wanachama wa Chadema, wapenzi na Watanzania walifurika katika ofisi za Kanda, mikoa na majimbo nchi nzima wakiomba kumdhamini,” alisema Kigaira. Alisema wanachama hao walidhani fomu hizo zimepelekwa kila mkoa, kutokana na kuepuka kuwanyima fursa hiyo chama hicho kilipeleka fomu ili wanachama wamdhamini na kupewa masharti kuwa lazima wawe wamejiandikisha kupiga kura, wataje namba zao za simu. Huku akionyesha fomu chache za wadhamini kutoka mikoa mbalimbali nchini, Kigaira alitaja idadi ya watu waliomdhamini Lowassa katika mikoa yote 32 kuwa ni 1,662,397. Akizungumzia udhamini wa wanachama Mwalimu alisema: “Lowassa alitakiwa azunguke mikoani kusaka wadhamini ila siku zilikuwa zimebaki mbili. Tuliwataka wanachama wanaotaka kumdhamini (Lowassa) wafike makao makuu, siku uliyochukua fomu. Wanachama 700 walikuja kukudhamini.” Alisema kitendo hicho kiliiibua malalamiko kutoka kwa wanachama wa mikoa mbalimbali nchini, hivyo kuagizwa fomu za udhamini zipelekwe mikoani. Safari ya Lowassa haitavurugwa Katika maelezo yake, Mwalimu alisema CCM inafanya vikao ili kuivuruga Chadema, lakini akasema kuwa hilo halitafanikiwa na hakuna wa kuivuruga safari ya Lowassa. “Tunajua kuna mikakati na vikao vinavyoendelea kwa nia ya kumzuia Lowassa katika safari hii ya Chadema na Ukawa, lakini tunawaambia Lowassa kuja Chadema ni mpango wa Mungu. Hatujamuokota barabara, ni Mungu amemuongoza kuja chama chetu kwa sababu Mungu ameshakiandikia neema chama hiki kutokana na falsafa inazokisimamia tangu kuanzishwa kwake.” “Njama zozote za kishetani, kihafidhina na kifedhuli zitalegea na kupotezwa. Lowassa amebakiza hatua mbili, ya kwanza ni kumaliza mchakato wa ndani ya chama kupitia Mkutano Mkuu na hatua ya pili ni kuapishwa.” Mwalimu alisema Chadema inaunga mkono kauli ya Lowassa ya kuuchukia umaskini, kwamba nchi imeshindwa kupata maendeleo kutokana na kuongozwa na viongozi wa CCM wenye fikra za kimaskini, za kuamini ili uwe kiongozi lazima uwe maskini. Alisema baada ya Lowassa kupitishwa na Mkutano Mkuu chama hicho, atazunguka mikoa mbalimbali nchini kuanzia Dar es Salaam Agosti 9. Lengo ni kuchukua nchi “Kuna watu walidhani Lowassa hawezi kurejesha fomu. Safari ya kuelekea uchaguzi mkuu imefikia hatua muhimu. Kinachofuata ni Kamati Kuu kupitisha fomu hizi. Naamini hakuna pingamizi lolote maana mpaka sasa hakuna aliyejitokeza kuchukua fomu za kugombea urais kupitia Chadema na Ukawa,” alisema Profesa Safari. Alisema wapo wanaosema mwaka huu wapinzani wataambulia wabunge na madiwani tu siyo rais, jambo alilodai kuwa si kweli na kwamba lengo lao ni kushinda kiti cha urais. “Wazanzibari wana msemo wao kwamba goli unafungwa, lakini chenga twawala. Sisi chenga tutapiga na magoli tutafunga,” alisema. Vigogo CCM Habari za ndani kutoka chama hicho zinaeleza kuwa vigogo wa CCM watatambulishwa kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu wa chama hicho, wakiwemo wabunge mashuhuri. “Siku ya mkutano mkuu watatambulisha wabunge na viongozi wa CCM. Ni wengi na wengine watawashangaza watu kwa kweli kwa sababu si watu wanaotarajiwa kuihama CCM, “ alisema mpashaji habari wetu. Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye ndiye anayeambatana na Lowassa na amehudhuria hafla zote za uchukuaji na urejeshaji fomu, mara zote akiulizwa amekuwa akijibu kuwa ni mshauri wa mbunge huyo wa Monduli wa masuala ya kupambana na rushwa. Chizii agoma kuzungumza Naye kada mkongwe wa CCM, Matson Chizii ambaye naye amekuwa bega kwa bega na Lowassa tangu ahamie Chadema, alipoulizwa kama amehamia katika chama hicho kikuu cha upinzani nchini alisema hana cha kujibu, kusisitiza kuwa atajibu suala hilo siku mbili zijazo. Chanzo:mwananchi.co.tz

Mauzauza kura za maoni CCM

Mauzauza jana yalitawala mchakato wa kura za maoni kwa ajili ya kupata wagombea ubunge na udiwani kwa tiketi ya CCM kutokana na kuwapo kwa vitendo vya rushwa, vurugu, kura kuchomwa moto, makada kukamatwa, wanachama kutoruhusiwa kupiga kura na kugundulika kwa karatsi zilizokwishapigwa kura. Kwenye baadhi ya maeneo kazi hiyo iliahirishwa hadi leo kutokana na vifaa kuchelewa na pia tatizo la kugundulika kwa shahada ambazo zimeshapigwa kura zikiwa ndani ya maboksi. Lakini matukio yaliyotawala kura za maoni ni makada kukamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kugawa fedha au kuchapisha karatasi bandia za kupigia kura. Dar es Salaam Wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, Takukuru inawashikilia wagombea sita kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa wajumbe ili wachaguliwe kwenye kura za maoni. Makamu mkuu wa Takukuru wilayani Kinondoni, Denis Manumbu aliwataja waliokamatwa kuwa ni katibu wa kata ya Kibamba, Denisi Kalela, katibu wa itikadi, Babu Kimanyo, diwani wa viti maalumu wa Goba, Rehema Luhanja, Wengine ni mwenyekiti kata ya Goba, Pili Mustafa, mgombea udiwani, Msigani Mwasha na Eliasi Nawera ambaye anagombea ubunge Jimbo la Kawe. Alisema kuwa Kalela, na Kimanyo walikamatwa juzi saa 4:00 usiku maeneo ya Kibamba CCM, huku Mustafa na Luhanja wakikamatwa maeneo ya Goba Kati na Kawe. “Walikamatwa wakiwa wanatoa rushwa na wengine walikamatwa wakiwa na kiasi cha pesa ambazo bado walikuwa wanazigawa huku wengine wakiwashawishi wajumbe kupokea rushwa,” alieleza Manumbu. Manumbu alisema katika kipindi hiki cha uchaguzi ofisi yao inafanya kazi saa 24 ikipokea taarifa zote zinazohusu rushwa. Kondoa Lakini hali ilikuwa mbaya wilayani Kondoa, Dodoma ambako CCM ililazimika kuchoma moto makasha sita ya kupigia kura baada ya kubainika kuwa baadhi ya wanachama walitumia kadi ya CCM pekee bila ya kitambulisho cha kupigia kura. Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Shaaban Kissu, mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Othman Gora na kamanda wa polisi wa wilaya, Nyantora walikubaliana kuchomwa moto baada ya kubaini tatizo hilo. Hatua hiyo, inatokana na wanachama kuanzisha zogo kuwa vitambulisho vya kura havikutumika kabla ya uamuzi huo kufikiwa. Tayari zaidi ya wanachama 200 walikuwa wamepiga kura hizo. Maboksi hayo yalichomwa mbele ya kituo cha kupigia kura cha Ubembeni na kushuhudiwa na wananchi, wananchama wa CCM, polisi na uongozi wa CCM. Baada ya kuyachoma, Kissu alitangaza kuahirishwa kwa uchaguzi huo baada ya dosari hiyo na kwamba utarudiwa leo. Baadaye kamanda wa polisi wa wilaya aliamrisha watu wote kutawanyika eneo hilo hadi leo. Awali kulitokea vurugu baada ya baadhi ya wanachama kunyakua sanduku lililokuwa na kura na kutaka kukimbia nalo kwa tuhuma kuwa mawakala hawakuwa wakitenda haki kwa wapiga kura Mbeya Kashfa ya matumizi ya rushwa pia ilijitokeza mkoani Mbeya ambako mgombea udiwani mmoja kulalamikiwa kwa madai ya kuwakodisha wanafunzi wampigie kura kwa malipo ya Sh2,000 kwa kila mmoja. Mgombea huyo wa udiwani wa Kata ya Mbalizi Road analalamikiwa pia alikwenda kwenye kilabu za pombe kuwatafuta watu wanaotaka kumpigia kura ili awanunulie kinywaji. Miongoni mwa walalamikaji ni Ally Salum na Aziza Mbika wa eneo la Sabasaba ambao walisema walimwona mgombea huyo akitoa fedha na pombe kwa vijana mbalimbali . Msimamizi wa uchaguzi wa Kituo cha Meta, Ndoni Mwakalukwa alikiri kupokea malalamiko ingawa hakushuhudia utoaji wa fedha hizo na kwamba atayazungumza baada ya kumaliza kazi ya upigaji kura. Vituo vingine, vikiwamo vya Kata za Ruanda na Sinde, vilikosa wanachama wa kupiga kura na badala yake walifika mmoja mmoja kila baada ya saa kupita. Wasimamizi wa uchaguzi maeneo hayo walikuwa na kazi ngumu ya kuwaita watu waliokuwa wakipita wakiwaomba wakapige kura kama ni wanachama wa CCM. “Tatizo ni kwamba vituo vya kupigia kura havijawekewa alama yoyote, hivyo wanachama wengi hawajui,’’ alisema msimamizi wa kituo cha Soweto, Ambakisye Kitunga. Lindi Rushwa pia ilijitokeza kwenye Jimbo la Mchinga (CCM) ambako mbunge wa viti maalumu, Fatuma Mikidadi alikamatwa na Takukuru kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa wafanyakazi wa taasisi hiyo waliomkamata kwa tuhuma za hongo. Habari zinasema kuwa mgombea huyo alikutwa na wafanyakazi wa Takukuru akitoa rushwa kwa wanachama wa Kata ya Mchinga. Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo, Mikidadi alikasirika akisema: “Uongo, uongo, huu ni uzushi kabisa.” Alipoulizwa kwa nini anafikiri wamemsingizia, alisema: “sijui hawa wanasingizia singizia tu, uongo.” Hata hivyo, kamanda wa Takukuru wa mkoa wa Lindi, Steven Chami alisema Fatuma alikamatwa saa 5:00 usiku Kata ya Mchinga akigawa fedha kwa wanachama. Chami alisema akiwa ofisi za Takukuru baada ya mahojiano, mtuhumiwa huyo alitoa tena Sh780,000 kwa ajili ya kuwahonga maofisa hao ili wasiendelee na suala hilo. Alisema kutokana na kitendo hicho, Takukuru itamfikisha mahakamani muda wowote baada ya mwanasheria kutafsiri na kubainisha tuhuma zake. Wakati huohuo, kamanda huyo alisema mgombea ubunge wa Jimbo la Lindi Mjini, Mohamedi Utali alishikiliwa kwa muda wa saa kadha kwa mahojiano na Takukuru baada ya kukutwa na Sh4milioni saa 8:30 usiku akiwa Kata ya Mbanja. Chami alisema kukamatwa kwa mgombea huyo kulitokana na ushirikiano baina ya wananchi na taasisi hiyo. Shinyanga Mjini Shinyanga, katibu wa Kata ya Mjini Shinyanga, Ramadhani Majani amenusurika kipigo baada ya kukamatwa usiku wa kuamkia jana akiwa ofisini kwake na mmoja wa wagombea udiwani na ubunge katika Jimbo la Shinyanga Mjini. Mashuhuda wa tukio hilo waliwaeleza waandishi wa habari jana kwamba Majani alikutwa na kadhia hiyo baada ya watu waliotilia shaka nyendo zake kwa kitendo chake cha kuongozana na mmoja wa wagombea nyakati za usiku kuingia ofisini na hivyo kuhisi kuna jambo lisilokuwa la kawaida walilopanga kufanya. Walisema waliamua kuwapigia simu wagombea wengine waliokwenda ofisi hizo na kumkuta mgombea mmoja (jina limehifadhiwa) akiwa anaongea naye, hata hivyo walishituka ghafla baada ya kuona kundi la wana-CCM wakijongea ofisini hapo. “Sisi tulipigiwa simu usiku saa 4:45 na baadhi ya watu wanaoishi jirani na ofisi yetu ya kata kwamba wamemuona katibu kata wetu akiwa na mgombea udiwani pamoja na wapambe wake. Walidai inavyoelekea walikuwa wakipanga mikakati mibovu ya kutaka kuiba kura,” alisema Rashidi Abdalah. “Taarifa hizo zilitushangaza sana. tuliamua kuchukua gari na kwenda katika eneo la ofisi na kweli tulimkuta katibu kata akiwa na mgombea (anamtaja jina) wakiwa nje ya ofisi za CCM wakitaka kuingia ndani, ghafla walipotuona mgombea na wapambe wake walikimbia na katibu kata aliingia ofisini na kuufunga mlango,” alieleza aliongeza. Abdalah alidai kitendo cha Majani kukimbilia ofisini kilisababisha baadhi ya watu kushikwa na hasira na kutishia kuvunja mlango ili kumtoa nje na kumshushia kipigo, lakini mgombea mwingine alimsihi ajisalimishe na kufanikiwa kutuliza ghasia. Majani alikiri kutaka kupigwa na kundi la wana-CCM na kwamba ni kweli muda huo wa usiku alikuwa ofisini akifanya kazi ya kugonga muhuri kwenye karatasi za kupigia kura japo hakuweza kufafanua kitendo cha mmoja wa wagombea kuwa katika maeneo hayo nyakati hizo za usiku. “Nilikuwa naendelea na kazi zangu lakini baadaye nilishangaa watu wanakuja na fimbo wakidai niko na mgombea ilibidi nijifungie ofisini kwangu,” alisema Majani. Handeni Hali ya sintofahamu ilitanda kwenye tawi la Bomani, Kata ya Vibaoni wakati zaidi ya wanachama 60 walipogoma kupigia kura wagombea udiwani kwa maelezo kuwa hawawafahamu kwa kuwa hawakufika eneo hilo kujinadi na badala yake kuamua kupiga kura ya wagombea ubunge. Wakizungumza jana wakati wa kuwasubiri wagombea, wanachama hao walisema kuwa walikutana kuanzia saa 9:00 alasiri kwa ajili ya kuwasubiri, lakini hawakutokea hadi saa 12:00 jioni, kitu ambacho walidai kuwa ni dharau. Mwenyekiti wa mtaa wa Bomani, John Mohamed alisema kuwa walikubaliana kukutana na madiwani hao kwa mara ya kwanza, lakini akidi ya wanachama haikutimia ikawabidi kuahirisha kikao hicho hadi jana lakini kitu cha ajabu wagombea hao hawakutokea hadi jioni. Arusha Sakata la karatasi bandia za kupigia kura pia liliibuka mkoani Arusha, ambako viongozi wawili wa CCM walikamatwa kwa tuhuma hizo. Waliokamatwa ni katibu wa Kata ya Mjini Kati, Ally Meku na mwenyekiti wa Mtaa wa Bondeni, Yakub Shaban. Katibu wa Wilaya ya Arusha, Feruz Bano alisema: “Ni kweli wamekamatwa, lakini tunafuatilia kujua kosa lao kwa kuwa hawana ofisi, hivyo walikuwa wanapeleka karatasi hizo kwenye chumba cha kupigia kura kidogo kidogo,” alisema. Dodoma Rafu iligubika uchaguzi huo mkoani Dodoma ambako baadhi ya wanachama walikamatwa na shahada bandia, huku vurugu zikiripotiwa maeneo kadhaa. Waliokamatwa na tuhuma kuwa walikuwa na shahada bandia ni katibu wa vijana Tawi la Chang’ombe, Nasra Salum akiwa na shahada 20 za kupigia kura, 20 za udiwani, Bakari Fundikira (za ubunge), na David Malolle. Mwingine aliyekamatwa kwa tuhuma hizo ni Faisi Mussa ambaye CCM imeeleza alikutwa na shahada 15 bandia. Aidha, baadhi ya kata zilishindwa kufanya uchaguzi kutokana sababu mbalimbali ikiwemo kuchelewa kwa vifaa na karatasi za kupigia kura kuwa na makosa. Miongoni mwa kata zilizoshindwa kufanya uchaguzi huo ni Tambukareli na Kilimani mjini Dodoma. Katibu wa CCM wa mkoa, Albert Mgumba alisema kata ambazo hazijafanya uchaguzi, kazi hiyo itafanyika leo kabla ya saa 4:00 asubuhi. Kuhusu makada waliokamatwa, katibu huyo alisema jambo hilo waulizwe makatibu wa wilaya kwa kuwa ndiyo wasimamizi wa uchaguzi huo. Katika hatua nyingine, vurugu zimetokea katika tawi la Mji Mpya lililoko Kata ya Uhuru kutokana na baadhi ya wanachama kudai kuna mamluki wameingia kupiga kura. “Asubuhi walikuja watu kutoka Tawi la Uhuru wakidai kuwa kuna mamluki wanataka kupiga kura kwenye tawi letu, lakini baada ya viongozi kufika tulirekebisha na zoezi likaendelea kwa amani na utulivu,” alisema msimamizi wa kituo hicho, Mariam Jumbe. Bukoba Hali ilikuwa tofauti mkoa Kagera ambako uchaguzi huo majina ya wanachama waliofariki dunia yalikuwapo kwenye orodha ya wapiga kura Jimbo la Nkenge huku kukiwa na hofu ya kuanguka kwa vigogo. Hali hiyo ilitokea katika vituo vya Mutemba na Igayaza. Hata hivyo, katibu wa CCM wa Wilaya ya Missenyi, Mwajuma Mboha alisema kujulikana kwa majina hayo, ni matunda ya uwepo wa mawakala katika uchaguzi huo. Pia kumekuwa na tatizo la kukosekana kwa majina ya baadhi ya watu waliofika kupigakura. Katika kata hiyo ya Nsunga kulikuwa na watu saba waliolalamikia kutoorodheshwa. Mtwara Kukosekana kwa majina katika orodha ya wapigakura pia ilijitokeza kwenye Manispaa ya Mtwara Mindindani. Wakiongea na Mwananchi, Shangani Aisha Ismail na Salima Nassoro wa Tawi la Vigaeni walisema wanashangazwa na kitendo cha uongozi wa CCM kuwapa kadi za chama bila kuweka majina yao katika daftari la wapigakura. “Sisi tumepewa kadi tunazo mikononi hatujui kama nyingine zimesajiliwa au la. Nyingine tumezilipia na majina yetu hayapo. Kuna kadi nyingine za mwaka 2000 hadi mwaka 1950 zipo na majina yao yapo na sisi majina yetu hayapo kuna nini hapa?” alihoji Aisha Katibu wa itikadi na uenezi wa wilaya, Mohamed Watanga alikiri kuwapo na tatizo hilo, akieleza kuwa wanalitafutia ufumbuzi. Njombe Pia mkoani Njombe, wanachama walishindwa kupigakura kutokana na kadi zao za uanachama kuonekana kuwa zilikatwa baada ya Julai 15, siku ambayo CCM ilifunga kazi ya kuandikisha wanachama wapya. Msimamizi wa uchaguzi wa kituo cha Mpechi, Sarah Nyandoa alisema licha ya uchaguzi kufanyika kwa amani, alikiri kuwapo kwa wanachama waliokuwa na kazi walizopata baada ya Julai 15. “Ni kweli kuna baadhi ya watu wanakuja na kadi zao zilizochukuliwa baada ya Julai 18, lakini tumewarudisha baada ya kuwaelimisha wameridhika,” alisema Nyadoa. Pwani Mchakato kura za maoni umeingia dosari katika vituo kadhaa baada ya baadhi ya wanachama kukatwa majina yao kwenye daftari la orodha ya wanachama wa chama hicho. Mbali ya kuwepo majina yaliyokatwa, pia baadhi ya wanachama walikutwa wakipiga kura kwa kutumia stakabadhi ya malipo ya wanachama maarufu badala ya kutumia kadi ya uanachama wa CCM. Kasoro hizo zilisababisha vurugu kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura mjini Kibaha na kumlazimu mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini, Maulid Bundala kusitisha uchaguzi huo kwenye vituo kadhaa vilivyokua na kasoro. Bundala alisema jana mchana kuwa vituo vilivyofutiwa kufanya uchaguzi ni Morning Star na Machinjioni vilivyoko Kata ya Tangini mjini Kibaha. Uchaguzi huo utarudiwa leo. Alipoulizwa sababu za kuwepo tofauti ya idadi ya majina yaliyomo kwenye daftari la uanachama na idadi ya wenye kadi za chama eneo hilo, alisema wamebaini kasoro hiyo imesababishwa na baadhi ya mabalozi kutowasajili kwenye daftari la chama la wapigakura. Katika hatua nyingine, baadhi ya wanachama waliokuwa wakipiga kura Kibaha Mjini wamelalamikia kuwepo rafu katika mchakato wa upigaji kura wakisema baadhi ya matawi yaliweka orodha kubwa ya wanachama wanaoruhusiwa kupiga kura ikilinganishwa na idadi ya awali iliyobandikwa kwenye kuta za ofisi za matawi yao. Tarime Mjini Tarime mkoa wa Mara, uchaguzi ulilazimika kuahirishwa hadi leo baada ya kukamatwa kwa karatasi bandia za kupigia zilizokuwa zimeshawekewa alama ya ndiyo kwa wagombea wa ubunge Jimbo la Tarime, na Tarime Mjini. habari kutoka ndani ya CCM zinasema kuwa karatasi hizo zinazoendelea kukusanywa, zilitengenezwa na mmoja wa viongozi wa wilaya, Bernard Nyerembe ambaye amekamatwa na kufikishwa Takukuru kwa mahojiano zaidi. Habari hizo zinasema kuwa karatasi hizo zilikuwa zichanganywe na karatasi halali baada ya wanachama kupiga kura za maoni. Mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Rashid Bogomba alithibitisha kukamatwa kwa karatasi hizo jana asubuhi. Alisema kwa Jimbo la Tarime, kura hizo zimekamatiwa katika vijiji vya Nyamwaga, Masanga na Nyamongo na kwa Jimbo la Tarime Mjini zimekamatwa Mtaa wa Bomani, Magena na Romori. Bogomba alisema kutokana na kukamatwa kwa karatasi hizo, uchaguzi umeahirishwa. Kamanda wa polisi wa Tarime/Rorya, Benadict Mambosasa pia alithibitisha kukamatwa kwa Nyerembe na kwamba amepelekwa Takukuru kuhojiwa. Alisema Nyerembe alikamatwa akiwa ofisi ya CCM ya wilaya baada ya wanachama kumtuhumu kuwa alikuwa na karatasi zilizokwishapigwa kura kwa ajili ya wagombea wawili wa majimbo hayo. Mwananchi ilipomtafuta Nyambari Nyangwine anayetetea ubunge wa Tarime, na Waziri Gaudensia Kabaka (Tarime Mjini) wote wwalikanusha kuhusika na kudai hizo ni njama zilizopikwa dhidi yao. Makada wengine wanaowania ubunge wa Tarime ni Christopher Kangoye ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Arusha, Nyambari Nyangwine (mbunge), Pius Marwa, John Gimunta, Maseke Muhono, Lucas Mwita, Paul Matongo na Charles Machage. Kwa jimbo jipya la Tarime Mjini wanaogombea ni Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, Maico Kembaki, Philipo Nyirabu, Jonathani Machango, Ditu Manko na Brito Burure. Chanzo:mwananchi.co.tz

Mwandani wa rais wa Burundi auawa

Mamlaka nchini Burundi inasema kuwa jenerali Adolphe Nshimirimana ameuawa. Imeripotiwa kuwa alifariki katika shambulizi la roketi katika gari lake kaskazini mwa mji mkuu wa Bujumbura. Jenerali Adolphe Nshimirimana alikuwa rafiki wa karibu wa rais Pierre Nkurunziza. Hata baada ya kuondolewa kama afisa wa idara ya ujasusi mwezi Novemba mwaka jana alikuwa akionekana na wengi kama mwenye ushawishi mkubwa nchini humo. Alishtumiwa kwa kusimamia oparesheni za kukabiliana na waandamanaji baada ya rais Pierre Nkurunziza kutangaza kwamba atawania muhula wa tatu mbali na kuhusika pakubwa katika kuzima jaribio la mapinduzi dhidi ya rais huyo. Kwa sasa wengi wana hofu ya hatua itakayochukuliwa na wafuasi wa Nshimirimana. Chanzo:BBC Swahili

NYALANDU AJIVUNIA MAFANIKIO MAKUBWA SINGIDA KASKAZINI

KATIBU CCM Mkoa wa Singida, Mary Maziku, amesema mchakato wa kampeni kwa wagombea wanaowania ubunge katika Jimbo la Singida Kaskazini, unaendelea vizuri. Pia, amesema changamoto zilizojitokeza ikiwemo baadhi ya wagombea kulalamika kufanyiwa rafu, yamepatiwa na yataendelea kupatiwa ufumbuzi kwa njia halali za vikao. Aliyasema hayo jana muda mfupi baada ya kufanya kikao na wagombea wanaowania ubunge kwenye jimbo hilo, ambalo linaongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu. Jana, Mary alifanya kikao na wagombea hao ambapo masuala mbalimbali yalijadiliwa ikiwemo malalamiko miongoni mwa wagombea. Jimbo hilo mbali na Nyalandu, pia linawaniwa na Amos Makiya, Justin Monko, Michael Mpombo, Sabasaba Manase, Yohana Sintoo, Mungwe Athumani na Aron Mbogho. Katika mkutano huo ambao uliisha kwa wagombea wote kuunga na kutaka kufanyike kampeni za kistaarabu. Awali, Mary alisema kuwa baadhi ya wagombea walikuwa wakilalamika kuchezewa rafu, ambapo baadhi walimlalamikia Nyalandu, ambaye pia aliwalalamikia wagombea wenzake kufanya kampeni chafu dhidi yake ikiwemo kuandaa watu kumzomea kwenye mikutano. “Kulikuwa na malalamiko miongoni mwa wagombea na ndio sababu tumeitana hapa ili kuzungumza ili kufikia mwafaka na kuendelea na kampeni. Kila mmoja amezunguza na ni mambo madogo ambayo hayana madhara katika mchakato,” alisema Mary na kuongeza kuwa: Nyalandu alilalamika wenzake kuandaa vijana wa kumzomea kwenye mikutano ili ashindwe kujieleza, jambo ambalo tumelizungumza pia. “Baada ya kupitia malalamiko hayo na mengine mengi kwa pamoja tumekubaliana yote hayo yanatokana na joto kali la uchaguzi wa mwaka huu na hayajavunja kanuni zetu”. Mary alisema kuwa wagombea wote wamekubaliana kuwa malalamiko hayo yamekwisha na wanasonga mbele na kampeni kwa ajili ya kuomba ridhaa ya wana-CCM na kukitanguliza Chama kwanza katika kila kitu. Alipoulizwa na waandishi wa habari, Nyalandu alisema malalamiko yaliyotolewa na wagombea wenzake ni dalili za kuashiria kushindwa. Alisema miaka yote amekuwa akiendesha kampeni za kistaarabu ndani na nje ya Chama na kwamba, anatambua kanuni na taratibu za CCM. “Nitumie fursa hii kuwaasa wanasiasa wenzangu kuacha vitendo vya rushwa, kupakana matoke, uzushi na uongo uliopitiliza. Tufanye siasa safi kwa maslahi ya wapigakura wetu na CCM kwa sababu kununua watu ili wanizomee bila sababu ya msingi ni kosa. “Najivunia kazi kubwa niliyoifanya kwa wananchi wangu na jimbo langu na ndio sababu ninasimama tena kuomba ridhaa ya wananchi ili niendelee kuwatumikia,” alisema Nyalandu.

Saturday, August 1, 2015

Kufa au kupona wagombea CCM

Leo ni kufa au kupona kwa makada wa CCM wanaowania ubunge wakati wanachama wa chama hicho tawala watakapopiga kura wilayani kuchagua wagombea kwenye majimbo yao baada ya wiki kadhaa za vikumbo zilizojumuisha kurushiana ngumi, tuhuma za rushwa, malumbano na migomo. Uchaguzi Mkuu umepangwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu. Katika upigaji kura leo, wanachama watakuwa na kazi ngumu kuamua kuhusu makada waliogeukia ubunge baada ya kukosa urais, mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Nne inayoondoka madarakani, waliotemwa mwaka 2010 wanaowania kurejea bungeni, wakuu wa wilaya ambao wameingia kwa wingi kwenye mbio hizo, na pia wabunge wanaomaliza muda wao ambao ama walikidhi mahitaji yao au kutofanya kazi ipasavyo. Mchakato huo wa kura ya maoni unafanyika baada ya kumalizika kwa siku 10 za wagombea hao kujinadi kwa makada wenzao katika kata mbalimbali za majimbo wanayotaka kugombea, huku baadhi wakijitoa kutokana na kushindwa kulipa fedha kama mchango wao wa safari za kampeni. Mchakato wa kura za maoni, utafuatiwa na vikao vya kamati za siasa za wilaya na mikoa wakati kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kitafanyika kwa siku mbili kuanzia Agosti 11 kwa ajili ya uteuzi wa wagombea rasmi wa ubunge na udiwani wa CCM. Gazeti hili linakuchambulia maeneo matano yatakayozua mjadala mkali mara baada ya matokeo ya kura ya maoni kutangazwa, pamoja na kilichojitokea wakati wa kampeni za wagombea hao. Wagombea urais waliojitosa ubunge Macho ya wana-CCM na wananchi wengine yatakuwa yakielekezwa kwa makada wa CCM walioanguka kwenye mbio za urais na ambao wamegeukia ubunge, ambao ni pamoja na Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi), Lazaro Nyalandu (Singida Kaskazini) na mwanasiasa mkongwe ambaye kwa sasa ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira. Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye alijiuzulu kutokana na kashfa ya escrow, lakini anataka kurejea bungeni kuwakilisha jimbo la Musoma Vijijini. Pia yumo January Makamba wa Bumbuli mkoani Tanga, William Ngeleja (Sengerema), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe (Nachingwea), Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani (Busega) na Waziri wa Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe anayerudi Kyela mkoani Mbeya na Balozi Augustine Maiga anayewania Iringa Mjini. Majimbo yenye mchuano mkali Nzega Vijijini Moja kati ya majimbo yenye upinzani mkali kwa sasa ni jimbo la Nzega Vijijini kutokana na uwepo wa makada wawili wa chama hicho, Lucas Selelii na Dk Hamisi Kigwangalla. Katika uchaguzi uliopita wa 2010, makada hao walivaana lakini wote wakaangushwa na Hussein Bashe aliyeibuka wa kwanza akifuatiwa na Selelii, lakini Halmashauri Kuu ya CCM ikamchukua Dk Kigwangalla aliyekuwa mshindi wa tatu. Mgawanyo wa majimbo uliofanywa hivi karibuni na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), umefanya mpambano huo uwe wa makada hao, baada ya kumwachia Bashe jimbo la Nzega Mjini. Iringa Mjini Jimbo jingine lenye mchuano mkali ni Iringa Mjini ambako Balozi Augustine Mahiga aliyekwama katika harakati za kuwania urais kupitia CCM, atapambana na makada wengine kuwania kupata tiketi ya kulikomboa jimbo hilo kutoka Chadema. Makada wengine kati ya 12 wanaowania kiti hicho ni Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Frederick Mwakalebela, mwenyekiti wa CCM wa mkoa, Jesca Msambatavangu na katibu mwenezi wa CCM mkoa wa Iringa, Dk Yahya Msigwa. Kundi lingine ambalo huenda likaleta upinzani katika uchaguzi huo linamjumuisha mjumbe wa NEC wa Iringa Mjini, Mahamoud Madenge, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Falles Kibassa na mwandishi wa habari, Frank Kibiki. Wengine wanaowania Iringa Mjini ni Peter Mwanilwa, Frank Kibiki, Michael Mlowe, Nuru Hepautwa, Adestino Mwilinge na Adani Kiponda. Jimbo la Mkalama Jimbo la Mkalama linaongoza kwa kuombwa na makada 16 wakiongozwa na mwenyekiti wa mkoa wa Singida, Mgana Msindai, Profesa Shaaban Aman Mbogho, Nakey Samwel Sule, Orgenes Emmanuel, Joseph Mbasha na Allan Joseph Kiula. Wengine wanaowania jimbo hilo ni Emmanuel Mkumbo, Dk Kissui Stephen Kissui, William Makali, Kyuza Kitundu, Dk Charles Mgana, Salome Mwambu, Francis Mtinga, Dk George Mkoma na Lameck Itungi. Jimbo la Kalenga Mchuano mkali pia upo, Kalenga linalowaniwa na mbunge wa sasa, Godfrey Mgimwa na Jackson Kiswaga, na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro na mbunge wa zamani wa jimbo hilo, George Mlawa. Jimbo la Mwanga Mshikemshike mwingine unatarajiwa kuibuka katika Jimbo la Mwanga ambako Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe anapambana tena na hasimu wake mkubwa katika kiti hicho, Joseph Thadayo. Maeneo yaliyotokea tafrani Wakati baadhi wakikabiliana na upinzani mkali, makada wengine watakuwa wakihangaika kushawishi wapigakura baada ya kukumbana na hali ngumu kwenye kampeni. Baadhi yao ni mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka, Harrison Mwakyembe (Kyela) na Assumpter Mshama (Nkenge). Profesa Tibaijuka Profesa Tibaijuka anayewania jimbo hilo kwa mara ya pili, alishushwa jukwaani kwa kuzomewa na wananchi wake katika kata ya Nshamba wilayani Muleba na tafrani hiyo kudumu kwa dakika kadhaa na kusababisha wagombea wengine kulazimika kuondoka. Kwa mara ya kwanza alizomewa Juni 8, wakati wa ziara ya katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwenye kata hiyo hiyo kutokana na kutajwa kwenye kashfa ya escrow na kushindwa kutekeleza ahadi ya kuwajengea barabara ya lami. Mwakyembe Hasira za wananchi pia zilimkumba mbunge wa Kyela, Harrison Mwakyembe kwenye moja ya mikutano yake baada ya wananchi kupiga kelele kutotaka kumsikiliza. Profesa Maghembe Hali kama hiyo ilimkuta Profesa Maghembe kwenye jimbo lake la Mwanga wakati akijinadi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kisangara. “Kidumu Chama cha Mapinduzi. Kisangara saafii,” alisalimia Profesa Maghembe na kuitikiwa na sauti za “ondoka ondoka, tumekuchoka sasa, nenda kapumzike huna jipya, waachie wenzio”. Profesa Maghembe alipoulizwa na gazeti hili jana kuhusu kadhia hiyo, alisema vijana waliomzomea walikodishwa na kupewa pombe katika baa ya jirani ili tu kujaribu kuchafua hali ya hewa. Profesa Maghembe anachuana tena na mshindani wake wa 2010, Joseph Tadayo na wagombea wengine ambao ni Karia Magaro, Baraka Lolila, Ramadhani Mahuna, Japhar Mghamba na Miniel Kidali. Naibu Spika Ndugai Wakati Maghembe akikumbana na hasira za wananchi, Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai alishindwa kuzuia hasira zake wakati maneno ya mgombea mwenzake yaliposababisha amvamie na kujikuta akihojiwa na polisi. Ndugai alihojiwa na polisi kwa tuhuma za kumshambulia mgombea mwenzake, Dk Joseph Chilongani kwenye mkutano wa kampeni akimtuhumu kurekodi tukio la kutaka kumpiga mgombea mwingine aliyekuwa akijieleza na kuponda uongozi unaomaliza muda wake. Hata kama atapita leo, suala lake linatarajiwa kuwa moja ya hoja kwenye kikao cha Halmashauri Kuu. Mwigulu Nchemba Hali kama hiyo ipo kwa mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba anayetetea jimbo lake akipambana vikali na katibu mkuu wa zamani wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, pamoja na Juma Hassan Kilimba anayerudi na Amon Gyuda. Nchemba amekumbana na tafrani baada ya kuhojiwa na Takukuru kwa tuhuma za rushwa. Baadhi ya wagombea wanaowania pamoja naye walishtaki kuwa mwenzao anafanya vitendo ambavyo walivihusisha na rushwa na hivyo Takukuru kuchukua hatua. Lusinde ‘Kibajaji’ Ushindani mkubwa katika jimbo la Mtera unaonekana kuwa baina ya mbunge anayemaliza muda wake, Livingstone Lusinde ‘Kibajaji’ na mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Samuel Malecela. Lusinde pia amekuwa akikumbana na kadhia hiyo baada ya wananchi kumzomea wakati akieleza sera zake kwenye kijiji cha Nkwenda wilayani Chamwino. Baada ya zomeazomea hiyo, mbunge huyo anadaiwa kuagiza kikundi cha vijana kuwashambulia wananchi ambao walikuwa wakimpiga kelele kumzomea. Venance Mwamoto Kada mwingine anayewania kurejea bungeni ni mwanasoka wa zamani, Venance Mwamoto ambaye amerejea Jimbo la Kilolo kupambana na mbunge wa sasa Profesa Peter Msolla. Wanahabari wapambana Wakati wanahabari wakikumbana na makada wa fani nyingine kwenye mbio hizo, Jimbo la Chemba linakutanisha wanahabari wawili, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia ambaye atavaana na mhariri kutoka gazeti la Mtanzania, Khamis Nkyota anayelitaka jimbo hilo kwa udi na uvumba. Tayari Nkamia ameshalalamikia bungeni harakati za mwanahabari mwenzake kwenye jimbo hilo. Manyoni Magharibi Hali ushindani inayotokana na makada wengi kujitokeza pia ipo kwenye Jimbo la Manyoni Magharibi ambako John Lwanji, mbunge anayemaliza muda wake, anakabwa koo na binamu yake Eliphas Emmanuel Lwanji. Wengine ni Jamal Kuwingwa, Jane Likuda, Mohamed Makwaya, Yahaya Masare, Athumani Masasi, Yohana Msita, Moshi Mmanywa, Adimini Msokwa, Dk Mwanga Mkayagwa, Rashidi Saidi na Francis Shaaban. Mbeya Mjini Hali kama hiyo pia ipo Mbeya Mjini ambako Charles Mwakipesile aliyepambana na mbunge wa sasa Joseph Mbilinyi mwaka 2010, atakuwa akipambana na Stephen Mwakwenda, Nwaka Mwakisu, Aggrey Mwasanguti na Mchungaji Jackson Numbi Wengine ni Ibrahim Mbembela, Fatma Ismail , Shambwe Shitambala, Solomon Swila, James Mwampondele, Ulimboka Mwakilili, Samuel Mwaisume, Eliud Mwaiteleke, Michael Mbuza Aman Kajuna na Shadrack Mwakombe. Singida Kaskazini Lazaro Nyalandu atakuwa na kazi ya kuzuia kazi ya Amos Makiya, Justin Monko, Michael Mpombo, Sabasaba Manase, Yahana Sinton, Mugwe na Aaron Mgogho. Jimbo la Nanyumbu Mgombea wa jimbo la Nanyumbu Dastani Mkapa yupo katika wakati mgumu kutokana na mgombea mpinzani wake William Dua kuonekana ana kasi ya kuchukua Jimbo hilo. Jimbo la Ndanda Mgombea wa jimbo jipya la Ndanda, Mariam Kasembe alijikuta akitoa machozi baada ya wananchi wa jumbo hilo kuuliza maswali kwa mgombea huyo na kushindwa kuyatolea majibu. Jimbo la Newala Mbunge wa jimbo hilo, George Mkuchika ana wakati mgumu kurudi katika nafasi hiyo kutokana na ushindani uliopo kuwa mkubwa ukilinganisha na uchanguzi wa 2010. Chanzo:mwananchi.co.tz