Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Monday, March 31, 2014

Bunge la Katiba kuanza kazi rasmi leo

Wabunge wakiwa Bungeni mjini Dodoma 
Na Mussa Juma, Mwananchi
Dodoma. Wakati Bunge la Katiba leo linaanza kujadili sura mbili za Rasimu ya Katiba ambazo zitalenga Muundo wa Muungano, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umewataka wajumbe wake kutokuondoka Dodoma hadi kumaliza kujadili sura hizo.
Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge iliyotangazwa Ijumaa iliyopita na makamu mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Saluhu, leo wajumbe wataanza kujadili sura ya Kwanza ya Rasimu ambayo inahusu Jina, mipaka, alama, lugha na Tunu za Taifa.
Sura ya sita, inahusu muundo wa Muungano, vyombo vya utendaji na mamlaka ya Serikali, nchi washirika na uhusiano wa nchi washirika.
Katibu wa Bunge la Katiba, Yahya Hamis Hamad alisema utaratibu wa kujadili rasimu kwa kuanza na sura hizo umetolewa na Kamati ya Uongozi kwa kuzingatia kanuni ya 58 ya Bunge la Katiba.
Kanuni hiyo ya 58 (3) inasema kamati ya uongozi itakuwa na majukumu ambayo ni “(a) kujadili na kuamua mambo yote yanayohusu uendeshaji bora wa shughuli za BungeMaalumu na kamati zake.
“(b) kujadili na kupanga ratiba ya utekelezaji wa shughuli za Bunge na (c) kujadili na kufanya uamuzi kuhusu masuala yatakayohitaji usuluhishi na maridhiano”.
Tamko la Ukawa
Mjumbe wa Bunge hilo, John Mnyika akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, alisema kuanzia leo Bunge litaanza kujadili muundo wa Muungano ambao alisema ndiyo moyo ya Rasimu ya Katiba hivyo wajumbe wote wa Ukawa watashiriki.
“Tumewaomba wajumbe kutokuondoka wakati wa kujadili sura hizi mbili kwani ndiyo roho ya rasimu na tunaonya ikifikia hatua CCM wakachakachua, tutachukua maamuzi (uamuzi) mazito na kwa gharama zozote,” alisema Mnyika.
Mnyika alisema tayari wamepata taarifa kuwa wajumbe kutoka CCM wataingia na mapendekezo yao na yatapigiwa kura kwa kujua wao wapo wengi pamoja na uteuzi wa wajumbe 201 walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete .
Hata hivyo alisema wakati wa kupitisha vifungu vya rasimu hiyo ni wazi kuwa CCM haina theluthi mbili kwa Zanzibar na kama wakipeleka mapendekezo ya kutaka kuvunja sheria na kanuni kwa masilahi yao hawatakubali.
Mnyika alisema licha ya Mwenyekiti wa Kamati ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kueleza upungufu wa mfumo wa Serikali mbili na hivyo kupendekeza Serikali tatu ambayo ni maoni ya wananchi, bado CCM inashinikiza na kutetea msimamo wao.
Mnyika alionyesha waraka aliodai wa siri wa CCM kuhusu jinsi ya kupinga mapendekezo ya Sura ya Kwanza na ya sita katika rasimu hiyo.
Alionya kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya kupitisha sura katika rasimu, ni lazima ipatikane theluthi mbili kwa upande wa Tanzania Bara na kwa Zanzibar.
Tamko hilo la Ukawa limekuja siku chache baada ya wajumbe wake kadhaa, akiwapo Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema kutangaza nia ya kuondoka Dodoma, akipinga mwenendo wa Bunge hilo hasa upigaji wa kura za wazi na siri kwa wakati mmoja.
Lema alidai kwa mazingira yaliyojengwa bungeni amepoteza imani ya kupatikana kwa Katiba ya wananchi.

Israel:Ehud Olmert alipokea hongo

Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Ehud Olmert amepatikana na hatia ya kupokea hongo.
Ehud Olmert ana kosa la kupokea hongo katika sakata inayohusu kipande cha ardhi
Mahakama moja ya Mji wa Tel Aviv alimpata na hatia kiongozi huyo wa zamani katika ksahfa iliyotokea wakati akiwa Meya wa mji huo mkuu.
Kadhalika Mahakama imesema kesi hiyo imefichua utawala uliokuwa fisadi na ambao uliendeleza ufisadi mkubwa katika kipindi cha miaka mingi.Inaarifiwa hongo ilitolewa na kupokelewa katika uuzaji wa kipande cha ardhi ili kuharakisha ujenzi wa nyumba za kifahari.
Sakata hiyo iliyojuliakana kama 'Holy Land' iliyohusisha kipande cha ardhi mjini Tel Aviv ilipelekea Bw. Olmert mwenye umri wa miaka 68 kujiuzulu kama Waziri MKuu mwaka 2008.
Hii ndio mara ya kwanza Waziri Mkuu wa Israel amepatikana na hatia ya Hongo. Duru zinasema kuwa hukumu hii huenda ikawa mwisho wa ndoto ya kisiasa ya bw. Olmert.
Kwa muda mrefu Olmert alikana kufanya makosa yoyote na pia tuhuma sawa na hii dhidi yake zilitupiliwa mbali na mahakama mbali mbali.

Warioba amshukia Prof Shivji

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na waandishi wa gazeti hili, nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 
Na Raymond Kaminyoge, Mwananchi
Dar es Salaam. Mjadala wa Mabadiliko ya Katiba jana ulihamia nje ya Bunge wakati Jaji Joseph Warioba alipomchambua mhadhiri maarufu nchini, Profesa Issa Shivji akimueleza kuwa si mkweli bali mpotoshaji wa Rasimu ya Katiba.
Jaji Warioba, ambaye ni mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, pia amemtuhumu Profesa Shivji kuwa ndiye mwanzilishi wa chokochoko za Zanzibar za kudai serikali tatu, jambo ambalo sasa analigeuka kutokana na kuona hali imekuwa mbaya.
Kauli ya Warioba imekuja baada ya Profesa Shivji kuichambua Rasimu ya Katiba jana asubuhi kwenye Kongamano la Vijana lililoandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo lililokuwa na dhima ya Vijana Katika Kuimarisha na Kuendeleza Muungano Baada ya Miaka 50. Tamasha hilo lilifanyika kwenye hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza jijini Dar es salaam.
Akiwasilisha mada kwenye kongamano hilo, Profesa Shivji alisema katika kujadili Muungano, wananchi hawana budi kuzingatia mambo mawili ambayo ni nchi zinazozungumziwa kwenye Rasimu kuwa ni Zanzibar, Tanganyika au Tanzania, ambayo alisema haina mamlaka katika pande hizo mbili za Muungano.
Pia alisema suala la maadili kwa viongozi halina budi kuangalia kuwa linazungumzia maadili ya viongozi wa Zanzibar, Tanganyika au Tanzania na kwamba rasimu inazungumzia viongozi wa Tanzania ambao hawana mamlaka kwa Tanganyika na Zanzibar.
Katika majumuisho yake, Profesa Shivji, ambaye aliikosoa Rasimu kuwa haiwakilishi matakwa ya Watanzania kwa kuangalia sampuli zilizotumika, alisema kwamba wajumbe wa Tume ya Jaji Warioba walikuwa na nia njema.
Lakini Shivji akaenda mbali zaidi kwa kusema “the road to hell is paved in good intention,” akimaanisha kuwa njia ya kuzimu imetengenezwa kwa nia njema.
Akijibu hoja hizo, Jaji Warioba alisema Profesa Shivji amegeuka maandishi yake yaliyokuwa yanachochea utaifa wa Zanzibar na sasa anaona Tanganyika ndiyo hatari kwa Muungano.
“Shivji ni msomi na mimi najua anaelewa matumizi ya takwimu,” alisema Jaji Warioba, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakati alipozungumza na gazeti hili nyumbani kwake jana jioni.
“Nasema hapa, Shivji akiwa msomi, amekuwa intellectually dishonest (si mkweli kiusomi). Anapotosha kwa makusudi.”
Jaji warioba alisema Shivji ndiye amekuwa chanzo cha uchochezi wa kitaifa Zanzibar kupitia maandishi yake. Alisema waliokuwa wanadai serikali tatu kwa muda mrefu walikuwa wananchi wa Zanzibar.


“Shivji alikuwa anasema Tanganyika imejificha kwenye Muungano ili inufaike. Kwa hiyo anasema Tanganyika iwe wazi isijifiche,” alisema Jaji Warioba.
“Na Shivji amechochea hilo… wote wale waliokuwa wanamnukuu walikuwa wanatoa hayo kwenye maandishi yake na kwamba mpaka leo hii kuna watu wa Zanzibar wanaamini Muungano huu si halali kisheria kutokana na Shivji ambaye alisema Baraza la Mapinduzi halikuridhia articles (ibara) za Muungano.”
Alipoulizwa jana usiku kuhusu tuhuma hizo za uchochezi na chanzo cha hisia za utaifa wa Uzanzibari na Utanganyika, Profesa Shivji alisema hawezi kujibu tuhuma hizo kwa kuwa hajamsikia Jaji Warioba akizungumzia hilo.
“Hey, amezungumza lini?” alihoji. “Siwezi kujibu kwa kuwa sijamsikiliza mwenyewe.”
Lakini Jaji Warioba alisema watu walitumia msingi huo kudai utaifa wa Zanzibar na kusisitiza kuwa Shivji amesababisha hisia za utaifa na kwamba haya yanayoendelea sasa yanatokana uchochezi huo.
“Hata kabla ya sisi kuanza mchakato huu, Shivji alikwenda Zanzibar akazungumza na Baraza la Wawakilishi na akawaambia issue kwa Zanzibar ni self determination (kujitambua), Sasa leo anaona kama hatari ni Tanganyika, lakini yeye ndio amechochea nationalism (utaifa),” alisema Jaji Warioba.
Kuhusu takwimu, Jaji Warioba alisema mara ya kwanza Profesa Shivji alizungumzia takwimu za Zanzibar kuhusu muundo wa Muungano akisema kuwa waliozungumzia suala hilo walikuwa 47,000, huku watu 27,000 wakitoka Tanzania Bara na 19,000 kutoka Zanzibar.
 “Safari hii ametaja zile za Tanzania Bara na kusema hiyo ni figure (namba) ndogo sana ukilinganisha na watu 300,000 waliotoa maoni,” alisema Warioba.
Alisema Tume ilitumia takwimu zinatokana na watu waliozungumzia suala ambalo wameliwekea asilimia na si kwa ujumla na ndio maana anaona Profesa Shivji anataka kupotosha kwa makusudi.
Warioba alimuelezea Profesa Shivji kuwa sasa ameamua kueneza propaganda za serikali mbili kwa kuponda Rasimu ya Katiba ambayo inaonyesha kuwa muundo wa serikali tatu ndio unaoifaa Tanzani kwa sasa.
Aidha, Warioba alisema msimamo wa Profesa Shivji ni kwamba Zanzibar haikukosea kubadilisha Katiba mwaka 2010.
“ Nimeshangazwa na Shivji kusema kwamba kitendo cha Zanzibar kubadili Katiba yao kuwa ‘Zanzibar ni Nchi’ halikuwa jambo la ajabu,” alisema Warioba.
Alisema Shivji ni msomi ambaye anafahamu kitendo cha kubadilisha Katiba kilikuwa na madhara makubwa katika muundo wa Muungano.
“Nadhani mnakumbuka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipoulizwa Bungeni kama Zanzibar ni nchi au siyo nchi, alijibu kuwa Zanzibar siyo nchi, vurugu zake mnakumbuka,” alisema.
Alisema lakini msomi kama Shivji haoni kama suala hilo la ‘Zanzibar ni nchi’ lina madhara makubwa katika mstakabali wa taifa letu.
Jaji Warioba alisema kama serikali tatu hazitakiwi, basi kinachotakiwa kufanywa ni kwa Zanzibar kubadili Katiba yake ili iseme kwamba Zanzibar ni sehemu ya Muungano, vinginevyo haiwezekani.
“Maana kama ni kusahihisha, ni lazima kwanza Katiba ya Zanzibar itumie maneno yale yale yaliyo kwenye Katiba ya Muungano. Yaani Zanzibar iwe sehemu ya nchi. Zanzibar wakubali hilo,” alisema.
“Zanzibar wakubali Rais wa Muungano ana madaraka nchi nzima maana mabadiliko ya 2010 yamemuondolea Rais wa Jamhuri ya Muungano madaraka yake.”
Akitoa mfano wa mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Jaji Warioba alisema amekuwa akidai takwimu hazionyeshi uhalisia wa maoni ya wananchi.
“Kwa mfano, Jimbo la Simanjiro linakuwa na watu 100,000 lakini waliojiandikisha kupiga kura ni watu 20,000 na waliopiga kura ni watu 15,000. Hii ina maana ushindi wake utakuwa katika watu waliopiga kura na siyo idadi ya watu wa Simanjiro,” alisema Warioba

Waumini Uganda wamshukuru Museveni

Raia wa Uganda kutoka dini mbali mbali hii leo wamekusanyika katika uwanja wa Kololo mjini Kampala kwa maombi maalum na kutoa shukurani kwa Rais Yoweri Museveni kwa kutia saini mswaada wa sheria unaozuia mapenzi ya jinsia moja.
Rais Museveni aliidhinisha sheria ya adhabu kali kwa Mashoga nchini Uganda mwezi Februari
Viongozi wa dini mbalimbali wakristo na waislamu wamehimiza waumini wao kujitokeza kwa wingi katika ibaada hiyo maalum.
Rais Museveni aliidhinisha sheria hiyo ambayo raia wengi wa Uganda wameipigia debe sana.Hii ni mara ya kwanza viongozi wa dini mbali mbali nchini Uganda kujitokeza kwa pamoja na kuandaa Ibaada maalum ya kumshukuru Rais Museveni na kuliombea taifa kuepuka vitendo vya ushoga.
Ibaada hiyo maalum inafanyika uwanja wa uhuru wa Kololo mjini Kampala, baada ya karibu mwezi mmoja na nusu tangu rais Yoweri Museveni kuiidhinisha
Tangu Rais Museveni kuidhinisha sheria hiyo kumekuwa na shinikizo kubwa kutoka kwa mataifa ya Magharibi yakimtaka kubadili msimo wake, huku baadhi ya mataifa yakipunguza msaada kwa Uganda.
Lakini raia wengi wa Uganda walimsifu Rais Museveni kwa hatua yake.

Musharraf ashitakiwa kwa uhaini Pakistan

Parvez Musharraf mtawala wa zamani wa kijeshi Pakistan
Mahakama moja nchini Pakistan imemsomea mashitaka ya uhaini mtawala wa zamani wa kijeshi Pervez Musharraf, ikiwa ni mara ya kwanza kwa mkuu wa majeshi nchini humo kushitakiwa.
Bwana Musharraf anatuhumiwa kusitisha katiba kinyume cha sheria na kutangaza utawala wa sheria mwakai 2007.
Bwana Musharraf alikuwa rais wa Pakistan tangu mwaka 2001 hadi 2008, alikuwa mmoja wa watawala wa Pakistan waliokaa madarakani kwa muda mrefu.Amekana mashitaka na daima amedai kuwa mashitaka dhidi yake yana msukumo wa kisiasa. Atakabiliwa na adhabu ya kifo iwapo atapatikana na hatia.
Alikwenda kuishi uhamishoni mwaka 2008, na kurejea Pakistan mwezi Marchi 2013.
Alikuwa na matumaini ya kukiongoza chama chake katika uchaguzi, lakini alikosa sifa ya kugombea na kujikuta akikabiliwa na mashitaka yanayomhusisha na uvunjaji wa sheria akiwa madarakani.
Musharraf mwenye umri wa miaka 70 amekuwa hospitali tangu mwanzoni mwa mwaka huu na taarifa zinasema anatibiwa ugonjwa wa shinikizo la damu.
Wafuasi wa Bwana Musharraf wamefanya maandamano katika mji wa Karachi wakitaka hukumu ya haki itendeke. Jaji amemsomea Bwana Musharraf mashitaka matano.
Amekana mashitaka yote lakini pia aliiambia mahakama mchango wake kwa nchi ya Pakistan na kuhoji vipi aitwe msaliti, akisema yeye ni mzalendo.
"Naitwa msaliti, Nimekuwa mkuu wa majeshi kwa miaka tisa na nimelitumikia jeshi hili kwa miaka 45. Nimepigana vita viwili na huu ni 'usaliti'?" Shirika la Habari la Ufaransa, AFP, limemkariri askisema.

Sunday, March 30, 2014

Ukawa sasa yapania kufanya ziara nchi nzima

Viongozi wa vyama vya CUF, Chadema na NCCR-mageuzi wakiwa mkutanoni siku za hivi karibuni. Picha na Maktaba 
Na Julius Mathias, Mwananchi
Dar es Salaam. Muungano wa Vyama vya Upinzani (Ukawa) nje ya Bunge la Mabadiliko ya Katiba (BMK), unajiandaa kuzunguka nchi nzima kufanya kampeni ya kuelimisha umma juu ya ukiukwaji wa haki na kanuni za Bunge hilo unaofanywa na chama tawala.
Wakitoa tamko la pamoja kwa waandishi wa habari jana, Makatibu Wakuu wa Vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, Dar es Salaam walisema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimekuwa kikijihusisha na vitendo vingi vinavyokiuka kanuni za upatikanaji wa Katiba Mpya ikiwamo utoaji wa rushwa kwa baadhi ya wajumbe.
“Ukawa-nje tumepata taarifa ya kutolewa kwa ahadi za vyeo baada ya Bunge kwa baadhi ya wajumbe ili kuunga hoja sera za CCM,” sehemu ya tamko ilieleza kupitia kwa Dk. Willbrod Slaa.
Ukawa-nje, wanasema kuwa hata hotuba ya Rais licha ya kuonekana kuipinga rasimu iliyosomwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba iliweka wazi dhamira ya CCM kupitisha mapendekezo yao.
Katibu Mkuu wa Chadema alimpongeza Profesa Ibrahim Lipumba kwa ujasiri wake wa kukataa uongozi ndani ya BMK, ingawa kuna posho za ziada kwa kuwepo katika nafasi hiyo.
“Wingi wa wana-CCM ndani ya Bunge isiwe hoja ya kuvuruga utaratibu mzima na wanatakiwa wajue kuwa Watanzania walio nje ni wengi zaidi yao,” alisema Dk. Slaa.
Naye Mkurugenzi wa Habari wa CUF (Taifa), Abdul Kambaya alisema kuwa wajumbe wa Ukawa waliunga mkono uchaguzi wa Samuel Sitta kuliongoza Bunge hilo kutokana na uwezo wake aliounyesha wakati akiwa Spika wa Bunge lililopita, lakini isiwe sababu ya CCM kutumia fursa hiyo kama faida kwao.
“Uongozi wote wa juu wa bunge umeshikwa na watawala ambao hawawezi kuzalisha katiba nzuri ya wananchi,” alisema Kambaya.
Wajumbe hao pia walieleza kuwa utungaji wa Katiba ni suala la hoja, ushawishi, mijadala huru, maafikiano na maridhiano. Kwa kuwa mpaka sasa taifa limeshatumia zaidi ya Sh81 bilioni katika mchakato huo ni vyema kanuni zikazingatiwa.
Ukawa-nje wanaanza ziara yao leo katika Jiji la Mwanza kuhamasisha wananchi kuwa makini na mwenendo wa BMK. Ziara hizo zinaweza zikawakosa wenyeviti wa vyama hivyo, ambao nao ni Wajumbe wa BMK wanaoendelea na vikao mjini Dodoma.

Wajumbe wa Bunge Maalum wasusia Bunge

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Esther Bulaya ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) akipiga kura ya siri juzi wakati Bunge hilo lilipokuwa likipitisha utaratibu wa kupiga kura za aina mbili ya siri na wazi. Picha na Salim Shao 
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dodoma/Dar. Wakati Bunge Maalumu la Katiba linatarajia kuanza kujadili Rasimu ya Katiba kesho, baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo wameanza kuondoka bungeni, kupinga mwenendo wa Bunge hilo.
Hatua hiyo ya wabunge hao inakuja wakati Bunge Maalumu la Katiba juzi lilipitisha azimio la kutumia kura ya siri na wazi katika kuamua vifungu vya rasimu.
Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samia Saluhu alisema baada ya kupitishwa kwa utaratibu wa kupiga kura za siri na wazi katika Bunge hilo, kuanzia Jumatatu wataanza kujadili sura ya kwanza na sita ambayo inahusu Muundo wa Muungano.
Katika sura ya kwanza, mambo ambayo yanatakiwa kujadiliwa ni Jina, Mipaka, Alama, Lugha na Tunu za Taifa wakati sura ya sita mambo ambayo yanapaswa kujadiliwa ni Muundo wa Muungano.
Lema atangaza kurudi jimboni Arusha
Mjumbe wa Bunge hilo, Godbless Lema alisema anakusudia kuondoka bungeni, kutokana na kutoridhishwa na maridhiano ya kupiga kura za siri na wazi katika kufikia uamuzi katika Bunge hilo.
Akizungumza na Mwananchi jana, Lema alisema hakubaliani na utaratibu uliopitishwa, kwani unalenga kulazimisha kila jambo ambalo chama tawala kinalitaka lipitishwe.
“Huu utaratibu wa kura kupigwa kwa wazi na siri katika kitu kimoja, haupo sehemu yoyote duniani. Sasa sisi kukubali ni kuwasaliti wananchi, kwani hata Dodoma tunaandaa rasimu ya Katiba ya wananchi wote siyo ya CCM pekee,” alisema Lema.
Alisema pia hakubaliani na utaratibu wa kujadili rasimu ya Katiba, ambao umetolewa na Kamati ya Uongozi kwa kuanza na sura ya kwanza na ya sita, kwani vinalenga kufumua Rasimu ya Jaji Warioba.
“Hapa CCM wanataka kulazimisha Serikali mbili kwa kujadili kwanza vifungu hivi, kama vitapita basi watakuwa na uwezo wa kubadili rasimu yote kitu ambacho mimi siwezi kukaa kwenye Bunge hili na kusaliti wananchi waliotoa maoni kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba,” alisema Lema.
Jussa atabiri Bunge kuvunjika.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mjimkongwe, Ismail Jussa, alisema uchaguzi wa vifungu hivyo ambavyo ndivyo vinabeba Rasimu ya Katiba, vinaashiria kuvunjika kwa Bunge hilo katika hatua za awali.
“CCM msimamo wao ni Serikali mbili na sisi ni Serikali tatu na tunaanza kujadili vipengele vinavyobeba Katiba na hakuna atakayekubali kuachia msimamo wake na hapo ndipo Bunge litakapovunjika,” alisema.
Kuhusu utaratibu wa kupiga kura za wazi na siri, Jussa alisema utaratibu huo utaleta mgawanyiko mkubwa, kwa sababu ya msimamo wa CCM ni kura za wazi na hivyo hakuna mjumbe wa chama hicho atakayethubutu kupiga kura ya siri.
Mnyika
Naye mjumbe mwengine wa Bunge hilo, John Mnyika, alisema, CCM ina mpango wa kubadili rasimu kutoka Muungano wa Serikali tatu kuwa wa Serikali mbili ili kufanikisha msimamo wao na maelekezo ya Rais kwenye hotuba yake bungeni.
Mnyika alieleza kuwa kwa mazingira hayo, Ukawa unahitajika kutetea maoni ya wananchi na kwamba CCM wakiendelea na njama zao wakati wa kujadili sura ya kwanza na ya sita, itawalazimu kurudi kwa wananchi ambao ndiyo wenye nchi.
“Hatua ya kurejea kwa wananchi inatarajiwa kuchukuliwa kabla ya kuendelea na sura zingine mbili za Rasimu ya Pili ya Katiba,” alisema Mnyika.
Mnyika alisema mpango huu ulianza kwa wajumbe wa Bunge Maalumu kutoka CCM wakati wa kujadili rasimu ya kanuni waliwasilisha majedwali ya marekebisho kutaka ibara zipangwe mbili mbili zinazofanana.
Katibu wa Bunge
Hata hivyo, Katibu wa Bunge Yahya Khamis Hamad akizungumzia kuondoka kwa baadhi ya wabunge alisema, suala hilo amelipata jana kupitia Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge lakini si msimamo wa kundi.
“Taarifa hii tulipata kwenye kamati, lakini tukaulizana kama kuna kundi linataka kuondoka, ikabainika hakuna kundi.”
Kuhusu uamuzi wa kuanza kujadili sura ya rasimu ya kwanza na sita alisema tayari yalifikiwa na Kamati ya Uongozi na kwamba kwa mujibu wa kanuni ya 58 kifungu kidogo cha tatu, Kamati ya Uongozi ndiyo yenye jukumu la kupanga utaratibu wa kujadiliwa rasimu.
Kuhusu CCM kuwa na rasimu yake
Akizungumzia taarifa kuwa CCM ina rasimu yake ambayo ndiyo wanataka ijadiliwe alisema hakuna suala hilo.
“Mimi binafsi sijalisikia hilo na sitegemei kuwapo, kwani wajumbe watajadili rasimu iliyo mbele yao ambayo ni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema Hamad.
Wasomi
Wasomi nchini wamesema mfumo wa kupiga kura ya wazi na siri uliopitishwa na Bunge Maalumu la Katiba, hautapunguza nguvu ya mijadala katika Bunge hilo katika vipengele muhimu ikiwa ni pamoja na aina ya muundo wa Serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wasomi hao walisema kuwa badala yake mfumo huo utawalazimisha baadhi ya wajumbe wasiokubaliana na misimamo ya vyama vyao kupiga aina ya kura wasiyoitaka.
Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho alisema mjadala mkali unatarajiwa kuendelea bungeni hasa katika hoja ya aina ya muundo wa Serikali, kwa kuwa hotuba ya Rais Jakaya Kikwete iliashiria kutotaka muundo wa Serikali tatu.
Profesa Shumbosho alisema kuwa kuna baadhi ya wajumbe wa CCM hawakubaliani na muundo wa Serikali mbili, lakini watalazimika kupiga kura ya wazi ili kukiridhisha chama chao.
“Kuna watu hawana ujasiri. Ndani ya CCM wapo wanaopenda Serikali tatu lakini wanaogopa,” alisema Profesa Shumbusho.
Pia, alisema kuwa kwa namna hali inayoonekana kuendelea bungeni, kuna dalili kuwa maoni ya rasimu ya CCM kuhusu Katiba ndiyo yatakayopita na hivyo kurudisha mambo mengi yaliyopo katika Katiba ya sasa.
Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Gaudence Mpangala alisema kuwa upigaji kura wa wazi au siri hautazuia wajumbe kuendelea na misimamo yao na kwamba badala yake mjadala utakuwa mkali zaidi kuliko ilivyokuwa awali.
Alisema ingawa yapo baadhi ya mambo ambayo wajumbe wanaweza kukubaliana bila kupiga kura, suala la Muungano litakuwa na mvutano kwa kuwa tayari hotuba ya Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na Rais Kikwete bungeni, zimeshaleta ‘msuguano’.
“Mjadala utakuwa mkali, suala lenyewe tu limeanza kuwa kali tangu mwanzo. Warioba alieleza Serikali tatu, Rais Kikwete akapinga,” alisema Profesa Mpangala.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria, Hamad Salim alisema suala la kupiga kura ya siri au wazi limechukua muda mrefu kujadiliwa bila sababu za msingi.
Akifafanua, Salim alisema kuwa wanaotaka kura ya wazi wanajenga hoja kuwa wanataka masuala yote yawe wazi kwa wananchi, lakini wanashindwa kusema ni lini walipewa maoni hayo na wananchi.
“Sikubaliani na kura ya wazi, hawakutumwa na wananchi, walitakiwa kuridi kwao na kuwauliza aina gani ya kura wanataka,” alisema Salim na kuongeza:
“Kwa muda mrefu upigaji kura ulikuwa wa siri, sasa imekuwaje leo wanataka kura ya wazi?”
Sendeka
Mjumbe wa Bunge hilo, Christopha Ole Sendeka alisema matokeo ya kura za kupitisha kanuni ya 37 na 38 ya upigaji kura yamewashangaza Ukawa, lakini muhimu kwao ni kukaa bungeni na kujenga hoja.
“Matokeo ya jana (juzi) yamewakatisha tamaa kwa ushindi wa idadi nzuri ya kura, walidhani CCM haina theluthi mbili, lakini licha ya wabunge wengi hatohudhuria tumeshinda,” alisema Sendeka.
Alisema wingi wa CCM siyo ndani ya Bunge tu, kwani hata nje wengi wanakiunga mkono chama hicho.
“Vizuri wangekaa tu kwani CCM inaweza kupitisha mambo kwa kura nyingi zaidi, lakini wakiwepo tunaweza kufikia maridhiano katika baadhi ya mambo,” alisema Sendeka.
Umoja wabunge Wanawake
Naye Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wabunge, (TWP), Suzan Lyimo alisema utaratibu wa kura za wazi na siri utaleta vurugu na utekelezaji wake ni mgumu.
“Utaratibu huu ni mgumu kutekelezeka sasa sijui wanaopiga kura za wazi watakaa upande wao na wale wa siri upande wao, lakini ni mgumu kutekelezeka na hakuna nchi ambayo umeshawahi kutumika,” alisema.
Akizungumza na vyombo vya habari kwa niaba ya wabunge wanawake kutoka vyama vya upinzani, Suzan Lyimo alisema hotuba ya Rais Jakaya Kikwete imeleta madhara makubwa kwa wananchi hasa wale ambao hawana itakadi za vyama.
“Hotuba hiyo imeleta mpasuko mkubwa miongoni mwa Watanzania..., sisi kama wajumbe wa Bunge hili tunawahakikishia wananchi kwamba tutajadili Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayotokana na maoni ya wananchi,” alisema.
Kwa upande wake, Sabrina Sungura alisema mchakato huo wa Katiba unaweza usifike mwisho na kwamba mtu wa kwanza wa kulaumiwa ni Rais Kikwete ambaye alitoa hotuba ya kuwagawa wabunge.
“Tulipaswa kuambiwa kuwa Rais anatumia nafasi yake kama sehemu ya Bunge kuleta maoni yake na si kulizindua Bunge kama tulivyoambiwa katika ratiba,” alisema.
Naye Moza Abeid ametaka kurekebishwa upungufu uliojitokeza katika mchakato wa Katiba ili wananchi waweze kupata Katiba waitakayo.
Mussa Juma,Sharon Sauwa na Edith Majura, Goodluck Eliona.

Wamisri wanaomtusi El-Sisi waonywa

Wizara ya mambo ya ndani ya nchi ya Misri imesema kuwa inachunguza maneno yanayoandikwa kwenye mitandao ya kijamii yakiwa na kitambulisho, yaani "hashtag", yanayomtusi waziri wa ulinzi aliyestaafu ili kugombea urais, Field Marshall Abd-el-Fattah el-Sisi.
Wafuasi wamebeba picha ya El-Sisi
Heshtegi hiyo ambayo tafsiri yake ni "mpigie kura kuwadi", imesambazwa kwenye Twitter zaidi ya mara 100-milioni na imependwa na watu zaidi ya 40,000 kwenye Facebook.
Inaarifiwa kuwa wizara ya mambo ya ndani ya Misri imesema itawakamata watu wanaoitumia sana heshtegi hiyo.
Maneno hayo piya yamekuwa yakichorwa kwenye kuta za mjini Cairo chini ya mabiramu ya picha za Bwana Sisi.
Field Marshall E-Sisi aliipindua serikali iliyochaguliwa kwa njia za kidemokrasi ya Mohamed Morsi wa Muslim Brotherhood mwezi Julai mwaka jana.

Wanane wauawa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Vikosi vya Umoja wa Afrika nchini Jamhuri ya afrika ya kati vinasema kuwa watu wanane wameuawa na vikosi vya Chad katika mji mkuu wa Bangi.
Vyombo vya habari hatahivyo vimeiweka idadi hiyo kuwa juu zaidi.
Vikosi hivyo ambavyo vilikuwa vimewasili mjini humo ili kuwatorosha raia wa Chad wanaoishi nchini humo vinadaiwa kuwafyatulia risasi wakaazi wanaoishi katika maeneo ya wakristo ya mji wa Bangi.
Chad imeshtumiwa kwa kuwaunga mkono waasi wa kiislamu wa seleka ambao mwaka uliopita waliipindua serikali.
Taifa hilo la Jamhuri ya afrika ya kati limekumbwa na ghasia za kidini tangu kupinduliwa kwa rais Franswa Bozize.

Jamaa wa abiria wataka ukweli Malaysia

Jamaa kama 30 wa abiria wa Uchina waliotoweka na ndege ya Malaysia wamesafiri hadi Kualu Lumpur, mji mkuu wa Malaysia, kuwahimiza wakuu wajibu maswali yao.
Jamaa wa abiria wa ndege ya Malaysia iliyopotea
Walitoa bango katika uwanja wa ndege wakisema wanataka ushahidi na ukweli kuhusu nini kimesibu ndege hiyo.
Wanataka wakuu wa Malaysia waombe msamaha kwa kusema kuwa ndege hiyo imepotea katika Bahari Hindi na kwa kuchelewa kutoa habari hizo.
Mwandishi wa BBC amesema kuwa kuwasili kwao kulizua hali ya wasiwasi na familia hizo zilipewa ulinzi mkali na watu wa Malaysia waliojitolea, na hivyo kuwa vigumu kwa waandishi wa habari kuwafikia.

Saturday, March 29, 2014

MIAKA 30 YA NDOA YA MWALIMU CHRISTOPHER NA DIANA MWAKASEGE

Hatimaye Mwalimu Christopher na Diana Mwakasege  wamefikisha miaka 30 ya ndoa yao. Ambapo kulikuwa na tafrija fupi ya kusherehekea tendo hilo iliyofanyika jijini Arusha wiki iliyopita ambayo ilihudhuriwa na mkuu wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini Askofu dkt Alex Gehaz Malasusa, familia ya mwalimu Mwakasege, ndugu, jamaa pamoja na marafiki. Mungu aendelee kuwainua watumishi hawa ambao wamekuwa baraka kwa taifa letu la Tanzania. Tunawapongeza sana na kuwatakia maisha marefu zaidi ya ndoa pamoja na baraka zitokazo kwa Mungu ziambatane pamoja nanyi siku zote mkazidi kupata maarifa zaidi katika kuwahudumia watu wake.

Picha za tukio ambazo GK imefanikiwa kuzipata.
Mwalimu Mwakasege, mkewe pamoja na mtoto wao wa kiume.
Waalikwa wakiwapokea kwa shangwe maharusi. ©christian criminology
Mwalimu Christopher na Diana Mwakasege.
Habari na Gospel Kitaa

Kura mchanganyiko Bunge la Katiba

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Profesa Abdul Shariff (kulia) akipiga kura ya siri wakati Bunge hilo jana lilipokuwa likipitisha utaratibu wa kupiga kura za aina mbili (siri na wazi). Picha na Silvan Kiwale . 
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dodoma.Wajumbe wa Kamati ya Maridhiano jana walinusuru Bunge Maalumu la Katiba kuvunjika, baada ya kukubaliana kutumika kwa utaratibu wa upigaji kura wa wazi na siri kama ilivyopendekezwa na Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge.
Wajumbe hao walitangaza uamuzi huo bungeni kutokana na makubaliano yaliyofikiwa katika kamati ndogo ya maridhiano iliyofanyika jana asubuhi baada ya kushindwa kuafikiana katika kikao cha awali kilichofanyika juzi kuanzia saa 3:00 usiku hadi usiku wa manane ili kunusuru kukwama kwa Bunge hilo.
Kabla ya uamuzi huo, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta alisema juzi usiku walikutana hadi usiku wa manane baada ya hapo, walikabidhi kamati ndogo yenye mchanganyiko wa wajumbe kutoka Kamati ya Kanuni na Kamati ya Maridhiano.
“Baada ya kukamilisha kazi, wajumbe wa kamati ndogo watatoa taarifa hapa ambao ni John Mnyika, Profesa Ibrahimu Lipumba, Vual Ali Vual na Askofu Donald Mtetemela,”alisema Sitta.
Akitoa taarifa ya maridhiano hayo, kwa niaba Freeman Mbowe, Mjumbe John Mnyika alisema, alianza kwa kunukuu kitabu kilichoandikwa na Mwalimu Nyerere, mwaka 1962 chenye ujumbe mahususi kwa Chama cha TANU akisema ujumbe huo kwa sasa ni sahihi kwa watu wengi na taasisi ikiwamo CCM.
Mnyika pia alisema Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) hawana nia yoyote ya kuvuruga mchakato wa katiba kama ambavyo imeelezwa katika siku za karibuni na viongozi, kwani wazo la kutaka Katiba Mpya imekuwa ni kilio chao cha muda mrefu.
Naye Profesa Lipumba alisema suala ambalo tumekuwa tukisimamia kwa muda mrefu suala ambalo lina utata, kati ambao wanapenda kura za uwazi na wale wa siri.
Alisema: “Tuliletewa mchanganyiko wa uwazi na siri, lakini maana yake ni kura ya uwazi, wenzetu wamekuwa na msimamo mkali hata hili la kufanya uamuzi ilikuwa tufanye kwa siri, lakini hata hivyo hawakukubali.”
“Tulifanya uamuzi ili tusonge mbele, basi tulipendekeza upigaji kura wa kuamua tupige kura kwa mfumo wa siri, lakini pia wenzetu walikataa,”alisema Profesa Lipumba.
Alisema kwa kuzingatia kutokwama kwa zoezi la kuanza kujadili rasimu, wameamua kukubali kutokubaliana.
“Ili kusonga mbele tunahitaji kusonga mbele tuanze kujadili Katiba, natoa wito kwa wenzangu wa chama tawala kwa kuwa mpo wengi mnadhamana kubwa, ni vyema mkawa na utaratibu wa kuwasikiliza wachache,” alisema.
Mjumbe Vuai Ali Vuai alisema, wamefikia maridhiano hayo, ili kuwezesha kuendelea na mchakato wa katiba mpya kwani kila upande uliendelea kutetea msimamo wake hata katika kikao cha maridhiano.
“Yapo mambo yalijitokeza kwenye kamati ambayo ni mengi, tulidhani hapa tunakuja kueleza yale ambayo tunakubaliana kulikuwa na hoja nyingi kuwa CCM hatutaki kuendeleza mchakato, lakini nilisema CCM tutakuwa wa mwisho kusitisha mchakato wa Katiba,” alisema.
Alisema kwa mustakabali wa taifa waliamua kupitisha uamuzi wa kukubali kura za siri na wazi kwa pamoja.
Naye Askofu Mtelemela aliomba wajumbe kukubali maridhiano ambayo, wamefikia ili kuweza kusonga mbele katika kuanza kujadili mchakato wa Katiba.
Askofu Mtetemela alisema baada ya majadiliano, wamekubaliana kurudi kwenye azimio la Kamati ili kuruhusu kuendelea na kazi ya kujadili rasimu ya Katiba.
“Jambo zuri ambalo limejitokeza sote tuna nia njema kwa ajili ya Bunge hili maalumu kuhakikisha mchakato wa kupatikana Katiba Mpya haukwami,” alisema.
Alisema kwa siku 40 sasa wamekuwa wakijadili suala moja tu la kanuni, kazi ambayo inasubiriwa ya kujadili rasimu ya Katiba.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge
Baada ya taarifa hiyo ya Kamati ya Maridhiano, Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge, Pandu Ameir Kificho, pamoja na wajumbe wa kamati hiyo, Profesa Costa Mahalu na William Ole Nasha, walitoa ufafanuzi wa kisheria kuhusiana na kanuni hizo.
Hata hivyo, kwa pamoja walieleza kuwa uamuzi wa utekelezaji ya kanuni ya 37 na 38 yaliyokuwa ya yameachwa kama kiporo, yakikamilika kutawezesha kuendelea na mchakato ya Katiba.
Baada ya kamati kuridhia makubaliano hayo, zoezi la upigaji kura kuhusu uamuzi wa awali kama kura zipigwe kwa mfumo uliopendekezwa wa kura za siri na wazi ulianza.
Matokeo ya kura
Akitangaza matokeo haya, Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu alisema idadi ya wajumbe waliokuwa katika ukumbi ilikuwa 511, waliopiga kura walikuwa 509.
Alisema waliopiga kura ya wazi walikuwa 438 kati yao 351 walipiga kura ya ndiyo na 87 walipiga kura ya hapana.
Suluhu alisema waliopiga kura ya siri walikuwa wajumbe 71, kati yao 25 walipiga kura ya ndiyo huku wajumbe 46 wakipiga kura ya hapana.
Alisema jumla ya wajumbe waliopiga kura ya ndiyo ni 376 na waliopiga kura ya hapana walikuwa wajumbe 133. Katika matokeo hayo wajumbe wawili hawakupiga kura ingawa waliokuwamo bungeni.
Kutokana na matokeo hayo Bunge hilo sasa litatumia utaratibu wa kupiga kura ya wazi na siri kwenye uamuzi wake katika kupitisha vifungu vya rasimu.
Mjumbe awananga wenzake
Mjumbe wa Bunge la Katiba, Paul Gekul amewashambulia wabunge wa Katiba wanaotoka kundi la CCM kuwa ni wanafiki wanaojipendekeza kwa sauti, lakini matendo yao hayaendani nao.
Gekul alisema kitendo cha wabunge hao kulazimisha kupiga kura za wazi ili wasikike na wapiga kura wao ni sawa na unafiki kwa kuwa katika majimbo yao hakuna maendeleo.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hivi juzi tulitoka katika Jimbo la Uchaguzi la Kalenga (Iringa) kati ya kata 17 ni kata tatu ndizo zenye umeme, leo hii wanaposema wanataka kura ya wazi siyo haki,” alisema Gekul.
Alipinga kauli za wabunge kuwa wapinzani ndiyo wanaotaka kupinga na kuvuruga mchakato wa Katiba kwa kusema wao ndiyo waliokuwa wa kwanza kuomba Katiba Mpya hivyo hawatakuwa tayari kuvuruga utaratibu huo.
Katika mchango wake mbunge huyo ambao ulionekana kujikita zaidi kwenye vijembe badala ya hoja ya kura za siri au wazi, alisema hakuna chochote ambacho viongozi wa CCM wamefanya kwa kipindi cha miaka 50.
Alitolea mfano wa majiji na miji mikubwa ambayo yanaongozwa na wabunge wa Chadema kuwa wanataka kura ya siri ili watafute mwafaka wa maendeleo ya nchi yao.
Wabunge CCM wajilipua
Wabunge wa watatu wa Chama Cha Mapinduzi, Mjumbe Kangi Lugola, Deo Filikunjombe na Ester Bulaya, kwa mara nyingine jana walijilipua kwa kukataa pendekezo la chama chao kuhusu upigaji wa kura wa aina mbili.
Filikunjombe alitoa kauli ya hapana kuonyesha anapinga kauli ya kupiga kura za ndiyo kwa wanaotaka na hapana kwa wanaotaka pendekezo lililokuwa limetolewa na Kamati ya Kanuni ambalo ndilo lililoungwa mkono na wajumbe wote wa CCM.
Hii siyo mara ya kwanza kwa Filikunjombe kwenda kinyume na msimamo wa chama chake, mwaka juzi alikataa kuunga mkono bajeti ya Serikali na hata katika mapendekezo mengi hupingana na wenzake kwa misimamo.
Filikunjombe
Filikunjombe akizungumza na gazeti hili alisema aliamua kupiga kura ya hapana kwa sababu ni uamuzi ambao hauna msimamo.
Walitakiwa kupitisha upigaji kura ama uwe wa wazi au wa siri.
Alisema yeye angekuwa mwenyekiti angetumia falsafa ya kidemokrasia ya kusikiliza maoni ya pande zote hasa wale wachache kusikiliza hoja zao kwa makini.
Mjumbe huyo alisema katika Bunge hili wanaotaka kura za wazi wapo wenge, ila hoja zao ni dhaifu na kwamba wanaotaka kura za siri ni wachache lakini hoja zao ni nzito na zina mashiko.
Awali wabunge wengi walionekana kupingana na uamuzi wa chama chao, lakini jana wengi waliamua kutoka nje bila ya kueleza misimamo yao hadharani.
Waliokuwa wamejipambanua kuwa wangepinga ni pamoja na mbunge wa Kahama James Lembeli, Ester Bulaya, Kangi Lugola na Mohamed Keissy.
Hata hivyo, muda mfupi jana kabla ya kuanza upigaji wa kura, ni Lembeli pekee ambaye hakuwapo katika Viwanja vya Bunge, lakini wajumbe wengine Keissy aliunga mkono kwa kauli ya ndiyo, huku Ester Bulaya alipiga kura ya siri na Lugola alisema alipiga kura ya wazi akisema hapana.
Wakati wabunge hao wakipinga, wabunge wengine kutoka vyama vya upinzani waliunga mkono azimio hilo kitendo kilichoibua mshangao mkubwa bungeni.
Waliounga mkono ni Augustine Mrema (TLP), Hamad Rashid Mohamed (CUF), Kuga Mziray (APPT), Fahmy Dovutwa (UPDP), huku John Shibuda aliomba karatasi apelekwe mahali alipo ili kupiga kura ya siri kwa sababu alisema anaumwa mguu.
Hata hivyo, wabunge wa upinzani walitofautiana wengine waliamua kupiga kura ya wazi kwa kusema hapana na wengine waliamua kupiga kura ya siri.
Moja wa wajumbe ambao hawakupiga kura ni Godbless Lema ambaye alisema hakupiga kura kwa sababu uamuzi wa Bunge hilo kutumia kura ya wazi na siri kwa pamoja hauna tija.

Mussa Juma, Habel Chidawali, Sharon Sauwa, Editha Majura na Beatrice Moses, Dar es Salaam.

Kanisa lafunga kuombea Bunge la Katiba

“Kwa hali ilivyo sasa bungeni, tusitegemee kupata Katiba au ikipatikana inaweza kutokidhi matakwa ya wananchi kwa sababu tayari wanaoitengeneza wamegawanywa. Tunamwomba Mungu aingilie kati.” Lucas Mwakalonge 
Na Editha Majura, Mwananchi
Dodoma. Kanisa la Makole Pentekoste Holyness la mjini hapa, linafanya maombi maalumu ya kuliombea Bunge Maalumu la Katiba baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa Bunge hilo.
Maombi hayo yaliyoanza Jumatatu, yanatarajiwa kumalizika Jumapili ijayo kwa waumini kugawanyika makundi, kila moja linaomba kwa kufunga kwa siku moja kabla ya kujumuika pamoja kanisani, Jumapili kuomba kwa pamoja.
“Kificho (aliyekuwa mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo) aliliongoza bila kanuni ingawa kulikuwa na mvutano haukuwa mkubwa na alipochaguliwa Sitta kuwa mwenyekiti wa kudumu wananchi wengi tulifurahi,” Mchungaji Kiongozi Asajile Mwandiga alisema na kuongeza.
“Kwa tulivyomfahamu uwezo wake wa kuongoza, kwa mfano Bunge la Tanzania la 9, tuliamini tungepata Katiba bora lakini imekuwa kinyume, anaegemea upande wa chama chake kwa uwazi kabisa.”
Mch. Mwandiga alisema hali hiyo iliwakatisha tamaa, lakini kwa kuwa wanaamini katika Mungu, sasa wanaongoza Kanisa kuomba msaada wake ili abadilishe mioyo ya wanaopindisha mambo.
Naye Mchungaji kiongozi msaidizi wa kanisa hilo, Lucas Mwakalonge, alisema tofauti na Bunge kuamua mambo kwa mtindo wa wengi wape, wao wanaoamini katika Mungu.
Mwakalonge alitaja sababu nyingine za maombi hayo kuwa ni mivutano ya mara kwa mara bungeni kiasi cha vikao kuvunjika na mgawanyiko wa Wabunge wa Bunge Maalumu.
Mchungaji huyo aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maktaba na Tafiti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano hadi alipostaafu mwaka 2011, alisema ili kufikia uamuzi wa kutoa Katiba bora ni lazima kuwe na umoja miongoni mwa wanaoiunda na kuiandika.
“Kwa hali ilivyo sasa bungeni, tusitegemee kupata Katiba au ikipatikana inaweza kutokidhi matakwa ya wananchi kwa sababu tayari wanaoitengeneza wamegawanywa. Tunamuomba Mungu aingilie kati,” alieleza.
Mbali na hayo, Mwakalonge alisema wanataka uwezo wa Mungu uzuie mambo yasiyompendeza kuingizwa kwenye Katiba, akitoa mfano wa sura ya 4 inayohusu Haki za Binadamu, kwamba kusiwe na utetezi wa mashoga na wasagaji.
“Kuna mambo hakika hayapaswi kuingizwa kwenye katiba yetu, tunamuomba Mungu apitishie mbali wale wote wanaotaka kuifanya katiba hii kama mchezo wa kuigiza,” alisema

Friday, March 28, 2014

WAZIRI MKUU AONGOZA MAMIA KUAGA MWILI WA MAREHEMU TUPPA

Viongozi Dini wakiongoza ibada ya kuuaga mwili wa Marehemu John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara na hapo awali aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma,aliefariki ghafa siku kadhaa zilizopita.
Waziri Mkuu,Mh. Mizengo Pinda akitoa heshima za mwisho kwa Mwili wa Marehemu John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara na hapo awali aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma,aliefariki ghafa siku kadhaa zilizopita.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,Balozi Seif Ali Idd akitoa heshima za mwisho kwa Mwili wa Marehemu John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Waziri Mkuu Mstaafu,Mh. Edward Lowassa akitoa heshima za mwisho kwa Mwili wa Marehemu John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu wa Bunge),Mh. William Lukuvi akitoa heshima za mwisho kwa Mwili wa Marehemu John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Mh. Rehema Nchimbi akitoa heshima za mwisho kwa Mwili wa Marehemu John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.
Jeneza lenye mwili wa Marehemu John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara likiwa uwanja wa Nyerere mjini Dodoma wakati wa ibada ya kuuaga.
Viongozi mbali mbali wa Vyama na Serikali wakiwa kwenye Ibada ya Kuaga mwili wa Marehemu John Gabriel Tupa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.
 
 
 
 

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameongoza viongozi mbalimbali na mamia ya wakazi wa Mkoa wa Dodoma kuuaga mwili wa aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Mara ambaye alifariki dunia ghafla Machi 25, 2014 akiwa ziarani wilayani Tarime.

Shughuli ya kuuaga rasmi mwili wa marehemu John Gabriel Tuppa kwa wakazi wa mji wa Dodoma ilifanyika leo mchana (Ijumaa, Machi 28, 2014) kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere ambako ibada ya kumwombea marehemu ilifanyika. Baadaye mchana, mwili wake ulisafirishwa kwenda wilayani Kilosa, mkoani Morogoro kwa mazishi.

Akizungumza na waombolezaji hao kabla ya kutoa heshima za mwisho, Padri Chesco Msaga ambaye aliongoza ibada hiyo, alisema Mungu aliwaumba wanadamu ili wampende na wamtumikie na kwamba marehemu Tuppa alilitimiza jambo hilo vilivyo.

Alisema wakati wa uhai wake, Bw. Tuppa alipenda haki na popote alipokwenda alitetea haki za wanyonge. “Sote ni mashahidi wa jinsi alivyopenda watu na jinsi alivyowatumikia watu. Alikuwa mnyenyekevu, aliwasikiliza wengine na alithamini michango ya wengine. Na sisi tunapaswa kuiga hilo,” alisema.

Naye Dk. Right Mmbaga, akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Baraza la Wazee la Dodoma Mjini alisema: “Wale watumishi ambao bado wako kazini na walipata nafasi ya kufanya kazi na Bw. Tuppa, wajifunze kutoka kwake na wafuate nyayo zake kama njia ya kumuenzi.”

Naye Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Mwigulu Nchemba, akitoa salamu kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM, alisema Chama cha Mapinduzi kimempoteza kamisaa makini sana aliyekuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), Bw. William Lukuvi aliwaasa wakazi wa Dodoma kuenzi mambo ambayo Bw. Tuppa aliwafanyia wakati akiwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma hata kama walikuwa hawayaoni.

“Alikuwa na upeo wa kufanya kazi kwa spidi lakini kwa utulivu. Wakati tumeanza naye kazi hapa Dodoma mwaka 2006, kulikuwa na shule sita tu za sekondari lakini katika kipindi cha miaka miwili alifanikisha kusimamia ujenzi wa shule za sekondari 30,” alisema Bw. Lukuvi ambaye wakati huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa Makanisa ya mkoa wa Dodoma, Askofu Dk. Yohana Masinga alisema viongozi hawajui kwamba wakishateuliwa, wao ni watumishi wa Mungu kwa sababu wanawaongoza watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu..

Akinukuu neno la Mungu kutoka kitabu cha Waebrania sura ya 13 aya ya 7, linalosema wakumbukeni waliokuwa wakiwaongoza, ichunguzeni miisho ya mwenendo wao na iigeni imani yao, Askofu Masinga aliwataka wote waige mfano wa utendaji kazi wa Bw. Tuppa.

“John Tuppa alikuwa ni mtendaji na kanisa limempoteza mtu makini. Ninawaomba viongozi wa nchi hii waige mfano wa John Tuppa. John Tuppa awe ni mfano kwao, na wafanye hivyo kwa ukombozi wa nchi yetu,” alisema.

Bw. Tuppa anatarajiwa kuzikwa kesho (Jumamosi, Machi 29, 2014) wilayani Kilosa. Alizaliwa Januari mosi, 1950. Amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya za Chunya, Mwanga, Bukoba, Muleba na Dodoma kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara  mwaka 2011. Ameacha mke na watoto watano.

Chanzo:http://www.2jiachie.com/