Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Tuesday, December 31, 2013

Katiba kutumika Uchaguzi 2015

Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi akisalimiana na viongozi wa vyama vya siasa waliohudhuria sherehe za makabidhiano ya rasimu ya pili ya katika jijini Dar es Salaam jana.Rais Kikwete aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kujadiliana na kukubaliana juu ya rasimu hiyo kwa ajili ya maslahi ya Taifa ili nchi ipate katiba mpya. Picha na Silvan Kiwale 
Na Waandishi Wetu,Mwananchi
Dar es Salaam.Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya, imeelekeza kipindi cha mpito ambacho pamoja na mambo mengine, kitaandaa mazingira ya Katiba hiyo kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
“Kufanya maandalizi na kuendesha Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kuzingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 2014 na kufanya maandalizi ya mambo yote muhimu kwa ajili ya utekelezaji bora wa masharti ya kikatiba yaliyomo kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 2014,” inasema sehemu ya rasimu hiyo.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba pia imependekeza kipindi cha mpito cha miaka minne kuanzia tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba Mpya ili sheria zilizopo ziweze kubadilishwa.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema jana kwamba katika kipindi hicho cha mpito utakuwa ni muda wa kutungwa kwa Katiba ya Tanganyika. Warioba alisema pia katika kipindi hicho, utakuwa ni muda wa mgawanyo wa rasilimali baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali za nchi washirika.
“Katika kipindi hicho pia utakuwa ni muda wa kufanya maandalizi na kuendesha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kuzingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 2014,” alisema.
Warioba alisema katika kipindi hicho, Katiba ya Zanzibar itafanyiwa marekebisho ili kuwiana na masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 2014.
 Maoni ya Muungano kutengeneza Katiba ya Tanganyika
Sehemu ya Rasimu ya Katiba ya Muungano, imependekeza kuwa maoni yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, yanaweza kutumika kutengeneza Katiba ya Tanganyika.
Raymond Kaminyoge, Elias Msuya na Fredy Azzah

JK ateua IGP mpya

Kamishna wa Polisi, Ernest Mangu,PICHA|MAKTABA 
Na Mwandishi Wetu,Mwananchi
Dar es Salaam.Rais Jakaya Kikwete amemteua Kamishna wa Polisi, Ernest Mangu kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini.
Taarifa iliyotolewa jana usiku na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ilisema kuwa Kamishna Mangu anachukua nafasi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini aliyestaafu, Saidi Mwema.
Kabla ya uteuzi wake unaoanza kesho, Januari Mosi, 2014, Kamishna Mangu alikuwa Mkurugenzi wa Inteligensia ya Jinai (Director of Criminal Intelligence) katika jeshi hilo la Polisi. Pia taarifa hiyo ilisema kuwa Rais Kikwete amemteua Kamishna Abdulrahman Kaniki kuwa Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi, ambayo ni nafasi mpya katika muundo wa sasa wa Jeshi la Polisi.
Kabla ya uteuzi wake, Kamishna Kaniki alikuwa Kamishna wa Uchunguzi wa Kijinai (Commissioner for Forensic Investigations). Taarifa hizi zilitufikia wakati tukienda mtamboni.

TAMASHA KUBWA LA KUANZA MWAKA NA BWANA PTA SABASABA

Kwa habari zilizoenea mjini, ni kwamba kila mtu jijini anapanga kufika kwenye ibada ya kuanza mwaka na Bwana kwenye kanisa la EAGT City Centre chini ya Mchungaji Florian Katunzi, ambapo kutakuwa na tamasha kubwa sana la changizo kwa ajili ya ujenzi wa kanisa kubwa zaidi ya ukumbi wa Sabasaba ambao unatumika kwa hivi sasa.

Waimbaji nio wengi, na ni sahihi kusema karibia waimbaji wote Dar watakuwepo siku hiyo, kuanzia walichapwa kwenye karatasi za matangazo hadi wale ambao hawajaainishwa, ikiwemo Upendo Nkone, Masanja Mkandamizaji, Beatrice Mwaipaja, Christina Mbilinyi, Anne Annie, na wengineo wengi. Yote haya ni kuanzia saa nane mchana na kuendelea kwa kiingilio cha 5,000 kwa watoto, 10,000, 20,000 na 50,000.

Karibu uchangie huduma ya Neno la Mungu isonge mbele, na pia upate huduma ya maombezi kutoka kwa mtumishi wa Mungu, Florian Katunzi, by Power, by Force.

UTABIRI WA TB JOSHUA JUU YA KIONGOZI AFRIKA MASHARIKI KUTEKWA WATIMIA

Nabii TB Joshua
Hatimaye utabiri uliotabiriwa na mtume TB Joshua wa Nigeria mwezi Octoba mwaka huu juu ya kiongozi mkuu wa moja ya nchi za Afrika mashariki kutekwa huku akikataa kutaja jina la nchi hiyo ila akisema iko karibu na Kenya zaidi ya kuwataka watu kufunga na kuomba juu ya nchi hiyo. Hatimaye utabiri huo umetimia kwa kiongozi wa Sudan ya kusini ambako kuna mapigano kwasasa. 

Kiongozi huyo amezungumzia juu ya utabiri wake huo katika ibada ya jumapili iliyopita kanisani kwake SCOAN nchini Nigeria ambapo Rais wa Sudan ya kusini alituma ujumbe wa watu wawili na barua ya shukrani kwa nabii huyo kwa utabiri wake juu ya taifa hilo ambapo akamuomba nabii huyo kuliombea taifa lake kuwepo mapatano na kuahidi kufika SCOAN mambo yatakapotulia. Tazama video chini kwa maelezo zaidi.

Serikali ya Tanganyika yaibuliwa katika Rasimu ya pili

Jambo jingine jipya ni kupunguzwa kwa madaraka ya uteuzi ya Rais kwa kuweka vyombo vya kupendekeza majina ya watu wa kuteuliwa na baadhi ya vyeo kuhitaji kuthibitishwa na Bunge.PICHA|MAKTABA 
Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Dar es Salaam.Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa Rasimu ya Pili ya Katiba ikiwa na mambo sita mpya, huku ikiendelea kupendekeza Muungano wa Serikali tatu na kurejea kwa nchi ya Tanganyika.
Rasimu hiyo ya Pili ambayo imetolewa miezi saba baada ya Rasimu ya Kwanza, ilikabidhiwa jana kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba katika hafla iliyofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam. Akizungumza kabla ya kukabidhi rasimu hiyo, Jaji Warioba alisema ina Ibara 271, tofauti na ile ya kwanza iliyokuwa na Ibara 240.
Alisema ripoti ya rasimu hiyo pia ina maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko ya Katiba, sera, sheria na utekelezaji maoni ya Mabaraza ya Katiba, takwimu za ukusanyaji wa maoni ya wananchi, makala za utafiti kuhusu mabadiliko ya Katiba na viambatanisho vya ripoti ya mabadiliko ya Katiba.
Mambo mapya
Maeneo yaliyofanyiwa marekebisho baada ya mchakato wa Mabaraza ya Katiba yaliyokutana kuanzia Julai 12 hadi Septemba 2 mwaka huu ni kuongezwa kwa vipengele kuhusu haki za binadamu.
Miongoni mwao ni haki ya kutoa na kupata habari. Pia imetaja haki za makundi maalumu yakiwamo ya watoto, vijana, wazee, walemavu na wanawake.
Kuhusu uraia, Jaji Warioba alisema imependekezwa uraia wa Tanzania kuwa mmoja tu na kutambuliwa kwa uraia wa kuzaliwa na wa kujiandikisha wa nchi moja. Alisema imependekeza pia kutoa fursa kwa uraia wa nchi mbili.
Jambo jingine jipya ni kupunguzwa kwa madaraka ya uteuzi ya Rais kwa kuweka vyombo vya kupendekeza majina ya watu wa kuteuliwa na baadhi ya vyeo kuhitaji kuthibitishwa na Bunge.
Aidha, alisema rasimu hiyo imependekeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iwe taasisi inayojitegemea badala ya kuwa sehemu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kama ilivyokuwa katika Rasimu ya Kwanza.
“Rasimu inapendekeza kuwepo na Jeshi moja la polisi na Idara moja ya Usalama kwa taifa zima, siyo kama tulivyokuwa imependekezwa katika rasimu ya kwanza kwamba kila upande unaweza kuanzisha jeshi lake la polisi,” alisema.
Muungano
Akizungumzia Muungano na jinsi Tume ilivyofanya uchambuzi wa pendekezo lake la Serikali tatu alisema: “Katika Rasimu ya Kwanza tulieleza kuwa kuendelea kwa Serikali mbili kulihitaji ukarabati mkubwa ambao tuliona hautawezekana.
“Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilieleza Tume itaongozwa na msingi mkuu wa kitaifa na maadili ya jamii ya kuhifadhi na kudumisha mambo kadhaa muhimu, moja ya mambo hayo ilikuwa ni kuwapo kwa Jamhuri ya Muungano. Tume ilianza kazi kwa madhumuni ya kupata maoni ya kuboresha Muungano.”
Alisema watu wengi walizungumzia Muungano, lakini wengi wao walijikita katika muundo wake. Kwa Tanzania Bara, wananchi zaidi ya 39,000 walitoa maoni yao kuhusu muungano, kati yao 27,000 walizungumzia muundo wake. Kwa upande wa Zanzibar, kati ya wananchi 38,000 waliotoa maoni 19,000 walizungumzia muundo wa Muungano.
“Tanzania Bara asilimia 13 walitaka Serikali moja, asilimia 24 walipendekeza Serikali mbili, asilimia 61 walipendekeza Serikali tatu. Kwa upande wa Zanzibar, asilimia 34 walipendekeza Serikali mbili na asilimia 60 walipendekeza Muungano wa mkataba na watu 25 sawa na asilimia 0.1 walitaka Serikali moja,” alisema.
Alisema vyama vya siasa, taasisi za kidini, asasi za kiraia na baadhi ya taasisi za Serikali zilipendekeza muundo wa Serikali tatu, huku akitolea mfano wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Baraza la Katiba Ofisi ya Waziri Mkuu na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Malalamiko Muungano
Alisema kila upande wa Muungano una malalamiko mengi kuhusu muundo na kwamba tume hiyo imeorodhesha malalamiko 10 kwa upande wa Zanzibar na manane kwa upande wa Tanzania Bara.
Alisema kwa upande wa Zanzibar, malalamiko matatu makubwa ni Serikali ya Tanganyika kuvaa koti la Serikali ya Muungano ambalo linaisaidia zaidi Tanganyika kuliko Zanzibar na kuifanya Tanganyika kuwa Tanzania.
Pili, mambo ya Muungano kuongezeka na kuathiri madaraka na kuishusha hadhi Zanzibar na tatu ni kumuondoa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Alisema kwa Tanzania Bara, malalamiko makubwa ni Zanzibar kuwa nchi huru yenye bendera yake, wimbo wa taifa, serikali yake na imebadili Katiba yake ili ijitambue kama nchi, wakati Tanzania Bara imepoteza utambulisho wake. Katiba ya Jamhuri inasema Tanzania ni nchi moja lakini Katiba ya Zanzibar inasema ni nchi mbili.
Pili, Zanzibar imebadili Katiba yake na kuchukua madaraka ya Jamhuri ya Muungano, kuelekeza sheria za Muungano zinazopitishwa na Bunge la Muungano zipelekwe kwanza kwenye Baraza la Wawakilishi kabla ya kutumika.
Tatu, wananchi wa Tanzania bara kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi Zanzibar, wakati wenzao wana haki hiyo Tanzania bara.
Muundo wa Muungano
Alisema katika kuchambua malalamiko ya Zanzibar, Tume imebaini kuwa muundo wa Muungano wa Serikali mbili umeifanya Serikali ya Muungano kushughulikia zaidi mambo ya Tanzania bara, hasa maendeleo na uchumi.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1977, Serikali ya Muungano ina mamlaka ya kusimamia mambo ya Muungano na yasiyo na muungano kwa upande wa bara... “Kwa msingi huo, Serikali ya Muungano inashughulikia sana kilimo, elimu, afya, maji, nishati na madini, ujenzi, uchukuzi, maliasili na utalii na mengine ya Tanzania bara yasiyo ya Muungano.”
Alisema kutokana na hali hiyo, Tume haikuwa na njia nyingine kwa sababu Serikali ya Muungano haina madaraka ya kutosha juu ya mambo ya maendeleo na uchumi kwa upande wa Zanzibar na kwamba hata utafutaji wa rasilimali zaidi ni kwa ajili ya Tanzania bara kuliko Zanzibar.
Alisema Zanzibar inafanya mipango yake ya maendeleo, kwamba ili ipate rasilimali, kama mikopo na misaada, ni lazima ipitie Serikali ya Muungano jambo ambalo utekelezaji wake umesababisha matatizo mengi.
“Njia pekee ambayo ingeiwezesha Zanzibar kufaidi shughuli za Serikali ya Muungano wa maendeleo ya Zanzibar ni mambo yote kuwa chini ya Muungano kwa maana ya kuwa na Serikali moja, lakini hilo likifanyika kuna hofu ya Zanzibar kumezwa,” alisema.
Alisema tume hiyo imefanya uchambuzi wa mambo 22 ya Muungano ili kubaini kama yanaingilia hadhi ya uhuru wa Zanzibar na kubaini kuwa siyo yote yanayotekelezeka. Mengi yamebadilishwa bila kubadili Katiba au kwa makubaliano ya pande mbili.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni kodi, bandari, viwanda, usafiri na usafirishaji wa anga, utafiti, posta na simu, uraia, takwimu, mafuta na gesi na Mahakama ya Rufaa.
“Kama Katiba ya Zanzibar ikibaki kutakuwa na nchi mbili; zikiwa nchi mbili haitawezekana nchi moja iwe na hadhi na uhuru na nchi nyingine isiwe na hadhi na uhuru, kwa tathmini yetu, tunaona ukarabati huu ni mgumu. Serikali tatu ndiyo suluhisho,” alisema.

Jeshi la jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo FARDC lafaulu kurejesha hali ya utulifu jijini Kinshasa baada ya kutokea uvamizi uliogharimu maisha ya watu zaidi ya sabini

Vikosi vya FARDC karibu na kituo cha  RTNC,jijini Kinshasa, 30 desemba 2013.
Vikosi vya FARDC karibu na kituo cha RTNC,jijini Kinshasa, 30 desemba 2013.
AFP PHOTO/STRINGER

Na Ali Bilali
Serikali ya Jamhuari ya Kidemokrasia ya Congo imesema waasi zaidi ya sabini wamepoteza maisha katika tukio la kuviteka vituo muhimu vya utawala wa rais Joseph Kabila. Kundi la vijana wanaojinasibu kuwa wafuasi wa mwanasiasa Pasta Joseph Mukungubila Mutombo ambaye aliwahi kuwania urais mwaka 2006 nchini humo na  ameiambia RFI kwamba wafuasi wake walikuwa wameandamana nchi nzima kupinga uonevu unatekelezwa na utawala wa Kinshasa.

Serikali ya DRCongo imesema watu sabini wamepoteza maisha wakiwemo wanajeshi watatu katika tukio hilo na jeshi limefaanikiwa kutuliza ghasia hizo zilizo shuhudiwa kwenye maeneo tofauti ya jiji ukiwemo uwanja wa ndege, kituo cha Radio na Runinga ya taifa pamoja na eneo la makao makuu ya jeshi.
Vurugu hizo zilianzia katika mji mkuu Kinshasa ambapo kundi la vijana waliokuwa na silaha za jadi ambao walikiteka kituo cha runinga ya taifa RTNC wakati kikiperusha matangazo yake moja kw amoja huku waandishi wa habari wawili wakashuhudiwa moja kwa moja wakifanyiwa vitisho na vijana hao wa Pasta Joseph Mukungubila ambaye aliwahi kuwania urais mwaka 2006 na kwa sasa anajiita kuwa nabii wa bwana.
Msemaji wa serikali ya DRCongo Lambert Mende amesema jeshi la serikali linadhibiti hali ya mambo, na kwamba uchunguzi umeanzishwa ili kubaini viongozi walionyuma ya vijana hao waasi.
Ghasia kama hizo zimeshuhudiwa pia katika miji ya Kindu na Lubumbashi na kusababisha kukatishwa kwa shughuli za usafiri wa kimataifa kwenye uwanja wa ndege wa Njili. Akizungumza na RFI idhaa ya Kifaransa pasta Joseph Mukungubila Mutombo amesema wafuasi wake hawakuwa na silaha.
 

Monday, December 30, 2013

MAMBO YA GLORIOUS CELEBRATION "WAKAWAKA" NDANI YA MBEYA

Usiku wa kuamkia leo kundi la Glorious Celebration ama waite "Wakawaka" kutoka jijini Dar es salaam, limefanya tamasha kubwa la kusifu na kuabudu katika ukumbi wa Mkapa Hall uliopo jijini Mbeya wakisindikizwa na Shekinah Glory Band. Hizi ni baadhi ya picha kama zilivyopigwa na John Kuyokwa.









HOLLYWOOD KUMTANGAZA YESU MWAKA 2014, MACHO YAELEKEZWA HUKO


Mwaka 2014 unatajwa kama mwaka wa udhihirisho na ukamilisho, hili linaungwa mkono na wasanii maarufu wa filamu duniani kutoka mji wa Hollywood maarufu kwa kutengeneza sinema kwani mwaka 2014 wanatarajia kuachia sinema kutoka katika Biblia. Kati ya sinema hizo ni pamoja na NOAH wakiigiza mambo ya gharika watu waliyoipata kwakutomtii Mungu na nabii wake aliyepewa maelezo ambaye kwakiswahili tunamwita Nuhu. Waigizaji wanaotarajiwa kung'ara katika sinema hiyo ni pamoja na Russell Crowe, Anthony Hopkins, Emma Watson, na Jennifer Connelly. Sinema hii itatoka wakati wa pasaka 2014, mpaka sasa kuna malumbano makubwa katika mtandao wa YouTube kuhusu ukweli wa jambo hili kutokea miaka ya nyuma hususani kwa watu wasioamini.

Sinema nyingine inayotarajiwa kutoka 2014 ni pamoja na filamu kumhusu nabii Moses ama Musa kutoka katika kitabu cha Kutoka ndani ya Biblia takatifu ambapo filamu hii itaonyesha zaidi maisha ya Moses ambayo hayajawahi kuonyeshwa ama kuigizwa katika sinema ikiwa pamoja na uhusiano wake na Farao na watu waliokuwa wakimzunguka kwahiyo itakuwa kitu cha tofauti chini ya muongozaji wake ama director Ridley Scott waigizaji wakuu wakiwa ni Christian Bale, Joel Edgerton, Aaron Paul, Ben Kingsley, na Sigourney Weaver. Sinema hii inatarajiwa kutoka Disemba 2014.

Nyingine ni "Son of God" au mwana wa Mungu kwa kiswahili ambayo imeigizwa kwa mtindo wa tamthilia ikiwa na masaa 10. Ni maisha ya Yesu kuzaliwa, kukua, kufanya kazi, kukamatwa na kusulubiwa na wayahudi kisha kufufuka, filamu hii itakuwa sawa na filamu nyingine inayoitwa "The Bible" ambayo imejaribu kuigiza habari ya Biblia chini ya Mark Burnett pamoja na Roma Downey huku mwigizaji mkuu akiwa Diogo Morgado. Inatarajiwa kuanza kuonyeshwa katika majumba ya sinema mwezi february 2014.

Sinema nyingine inayosubiriwa kwa hamu ni "Day of War" siku ya vita ikiwa ni sinema iliyotumia mamilioni ya pesa kutengenezwa ikielezea vita ya Mfalme Daudi kama ilivyoandikwa na Cliff Graham kupitia mwendelezo wa vitabu vyake vya "Lion of war"lakini ikichukua zaidi kilichoandikwa kwenye Biblia hasa vita ya mfalme Daudi na Goliath. Lakini bado haijafahamika lini filamu hiyo itazinduliwa ndani ya mwaka 2014.

Wakati hayo yakijiri Hollywood watu mbalimbali wameonekana kuvutiwa na mambo yatakayojili mwaka 2014 ikionyesha wazi kwa watu wanaomwamini Mungu kupokea mengi kutoka kwake kutokana na kuwa mwaka wa utimilifu. Lakini watu hao wamekuwa wakimuomba Mungu kwamba sinema hizo zisiwe za kufurahisha watu tu bali zilete maana na ukombozi kwa watu watakaozitazama. Katika historia ya Hollywood inaonyesha kati ya filamu zilizoleta pesa nyingi ama kupendwa ni filamu zilizotokana na habari za Biblia kama "Passion of Christ" ilikuwa ya mafanikio tele nyingine ni "The Prince of Egypt" chini ya Line Cinema na nyinginezo.

Kaa mkao wa kula mdau wa GK, wewe kama ni mwanamaombi zidisha maombi zaidi, kama wewe ndio mtenda dhambi ndio wakutenda zaidi lakini yote katika yote kila mtu atavuna alichopanda. Siku njema.

Habari kwa hisani ya Blog ya Gospel Kitaa

HUYU NDIO BINTI WA MAREHEMU ANGELA CHIBALONZA, MUNGU ANAMTUNZA


Picha ya juu binti wa aliyekuwa nyota wa muziki wa injili Afrika mashariki na kati marehemu Angela Chibalonza, bintiye wa pekee baby Wonder ambaye muonekano wake anafanana na mama yake ingawa GK haijajua kama atafuata nyayo za mama yake ama Mungu amempa talanta nyingine.

Picha hii ni kutoka kwa mama yake wa kufikia ama mlezi ambaye ni mke wa mtume Elisha Muliri ambaye ndiye alikuwa mume wa hayati Angela Chibalonza. Angela bado anakumbukwa na ataendelea kukumbukwa kutokana na alama kubwa aliyoacha kupitia uimbaji wake katika kumtangaza Kristo  kupitia album zake mbalimbali.

Hapa Baby wonder akiwa na mama yake mdogo Tete Meshak mdogo wa Angela Chibalonza ambaye pia ni mwimbaji kama alivyokuwa dada yake. Picha ni mali ya Tete.

Hebu tumalizie mwaka kwa kusikiliza wimbo huu "Wewe ni mwema" kutoka kwake marehemu Angela Chibalonza Muliri kati ya nyimbo ambazo zinabariki kuzisikiliza kutokana na sauti, upako na mpangilio wa vyombo kwa ujumla bila kusahau maneno yake. Barikiwa
Habarina Gospel Kitaa

Nchi ya Urusi yaendelea kukumbwa na mashambulizi na kusababisha vifo vya watu

Mlipuko kwenye kituo che reli mjini Volgograd,umegharimu maisha ya zaidi ya watu kumi

Na RFI
Watu zaidi ya kumi wamekufa na wengine zaidi ya thelathini wamejeruhiwa katika shambulizi la bomu kwenye kituo cha treni mjini Volgograd kusini magharibi mwa nchi ya Urusi. Tuko hilo limetokea, baada ya tukio lingine liliotokea jana jumapili kwenye kituo cha mjini kilichoko karibu na mji wa Caucase, na kugharimu maisha ya watu 17.

Idara ya uchunguzi nchini humo imesema shambulizi hilo limetekelezwa na mtu aliyejitoa mhanga anayeaminika kuwa ni mwanamke aliyejilipua baada ya kuwaona polisi wa ukaguzi.
Serikali ya Urusi imeimarisha usalama katika vituo vya mabasi, reli na viwanja vya ndege ili kukabiliana na mashambulizi zaidi, ambayo yanazidisha hofu ya usalama katika michuano ya Olimpiki ya Sochi inayotarajiwa kuanza nchini humo majuma sita yajayo.
Kamati ya uchunguzi wa tukio hilo imesema katika ripoti yake kwamba mshambuliaji wa kujitowa Muhanga alikuwa ni mwanamke na tayari uchunguzi umeanzishwa ili kubaini tukio hilo la Kigaidi.
Mashahida wa tukio hilo wamesema mshambuliaji huyo alijilipua katika eneo ambako kulikuwa na watu wengi wakiwemo polisi wa Usalama.
Duru za kitabibu zimearifu kuwa watu kumi na sita wamepoteza maisha wengine takriban 45 wamejeruhiwa wakiwemo watoto.
Rais wa Urusi Vladimir Poutine amevitaka vyombo vya dola na vile vya sheria kufanya kila liwezekanalo ili kubaini wahusika wa tukio hilo na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.
Ulinzi na usalama vimeimarishwa zaidi baada ya tukio hilo katika vituo mbalimbali vya treni na kwenye viwanja vya ndege nchini humo.
Umoja wa Mataifa na vikosi vya kujihami vya nchi za magharibi Nato wamelaani vikali shambulio hilo ambalo katibu mkuu wa Nato Anders Fogh Rasmussen amesema halina sababu yoyote.
 

Mashambulizi ya risasi yatokea Congo

Milio ya risasi imesikika katika maeneo ya kituo cha Televishen ya taifa, makao makuu ya Radio na katika uwanja wa ndege.
Taarifa za polisi nchini humo zinasema vijana wenye mapanga na bunduki wamevamia maeneo hayo na kuwateka watangazaji wa vituo hivyo.
Watu walioshuhudia tukio hilo wameeleza kuwa milio ya risasi ilianzia katika uwanja wa kimataifa ambapo pia kuna taarifa kupitia mitandao ya kijamii pia milio ya risasi ilisika katika maeneo ya kituo cha jeshi.
Mashuhuda wanasema risasi zilizkuwa zikifyatuliwa kuelekezwa pande zote hivyo kuwalazimu watu waliokuwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Kinsasa kijificha kukwepa mashambulio hayo
Msemaji wa polisi Kanal Mwana Mputu anasema Polisi wanaendelea kudhibiti eneo hilo huku wakiendelea kuwasaka wanaohusika katika shambulio hilo japo hawaeleza sababu za shambulio hilo.

Jeshi jeupe larudi nyuma Sudan Kusini

Serikali ya Sudan Kusini inasema wengi kati ya maelfu ya vijana ambao waliarifiwa kuwa wanaelekea mji muhimu wa Bor, sasa wameshawishiwa warudi nyumbani.
Waziri wa habari wa Sudan Kusini, MIchael Makuei
Waziri wa habari Michael Makuei ameiambia BBC kwamba wanasiasa wa kabila na Nuer katika eneo hilo, wameingilia kati kuwazuwia vijana hao kuelekea Bor - mji uliokombolewa na jeshi la serikali.
Hapo awali ofisi ya Umoja wa Mataifa Sudan Kusini ilisema helikopta yao iliyokwenda kupeleleza, kuangalia nyendo za kundi hilo la wanamgambo kama kilomita 50 kaskazini-mashariki ya Bor, iliwakuta lakini hawakujua idadi hasa.
Vijana hao wanaitwa "jeshi jeupe" kwa sababu ya jivu wanalojipaka kujikinga na wadudu.
Watu zaidi ya 1,000 wamekufa katika mapigano ya kikabila ya majuma mawili.
Wapatanishi wa Afrika Mashariki wamemuomba Rais Salva Kiir na makamo wake wa zamani, Riek Machar, wasitishe mapigano kati ya wafuasi wao ifikapo Jumaane.

Watoto wapotezana na wazazi Sudan Kusini

Mashirika ya misaada yamesema kuwa maelfu ya watoto nchini Sudan Kusini wanahofiwa kupotezana na wazazi wao kutokana na machafuko yanayoendelea yaliyoanza hivi karibuni nchini humo.
Shirika la Save the Children linasema kuwa idadi kuwa ya watoto wanaishi peke yao katika mazingira ya vijijini, ambapo kati yao wengine wazazi wao wameuawa mbele yao na nyumba zao kuharibiwa.
Katika mapigano yaliyochukua takriban wiki mbili zilizopita kwa mjibu wa shirika la Save the Children yalisababisha watu 1000 kuuawa ambapo watoto 60 katika eneo la Juba walikutwa wakiwa wametengana na familia zao anasema afisa wa shirika la Save the Children Helen Mould.
Zaidi ya watu 100,000 wameyakimbia makazi yao tangia kuanza kwa mapigano hayo huku familia pia zikisambaratika.Mashirika hayo ya misaada yanasema wakati watu wengine wakihifadhiwa katika makambi ya wakimbizi ama kuhifadhiwa katika jamii salama lakini bado watu wengine wakiwepo watoto walipatikana wakiwa wamejificha katika maeneo ya mabwawa ya maji huku wakinywa maji machafu.
Machafuko haya yaliyoanza kama mivutano ya kisiasa katika ya kiongozi wa waasi Riek Machar na Rais Salva Kiir yamechukua ukurasa mpya baada ya kuchukua sura ya mapigano ya kikabila.

Vijana wa Riek Machar wanaelekea Bor

Maelfu ya vijana wa Sudan Kusini wanaompendelea Riek Machar, wanasemekana kuwa wanaandamana hadi mji muhimu wa Bor, mji mkuu wa jimbo la Jonglei.Raia wakikimbia mnapigano ya Bor
Wanajeshi wa serikali wanadhibiti mji wa Bor baada ya kuukomboa kutoka kwa wanajeshi walioasi, huku mapigano ya kikabila yanaendelea nchini.
Vijana hao wa kabila la Nuer wanajulikana kama White Army (Jeshi Jeupe), kwa sababu ya jivu jeupe wanalojipaka kujikinga na wadudu.
Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini ameielezea BBC kwamba wanajeshi wake wanapigana kujaribu kudhibiti visima vya mafuta katika jimbo la Unity, kaskazini mwa nchi.
Ijumaa, Bwana Machar alisema wanajeshi wake wanadhibiti jimbo zima la Unity na jimbo lote la Jonglei, nje ya mji mkuu wa jimbo, yaani Bor.

Raia wa Chad wakimbia Afrika ya Kati

Pia madai kama hayo yameelekezwa kwa askari wa Chad waliopo ndani ya kikosi cha Umoja wa Mataifa kilichopo nchi Jamuhuri ya Afrika ya Kati.
Nchi ya Jamuhuri ya Afrika ya Kati ilikubwa na machafuko tangu mwezi marchi wakati waasi wa Seleka walipompindua Rais wa nchi hiyo Francois Bozize.
Maelfu ya raia wa Chad wanakimbia machafuko nchini Jamuhuri ya Afrika ya Kati na wamekuwa wakiondoka nchini humo siku ya Jumamosi na kujiunga na maelfu ya raia waliondoka wiki iliyopita.
mwanajeshi wa Ufaransa wa kulinda amani Jumuhuri ya Afrika ya Kati
Raia wa Chad waliokuwa wanaishi nchini Jamuhuri ya Afrika ya Kati wamekuwa wakituhumiwa kwamba baadhi yao wamekuwa wakiwasaidia waasi wanaoipinga serikali yaani kundi la wapiganaji la Seleka.
Uhasama ulizidi kupamba moto zaidi hasa pale waasi wa Seleka ambao wengi wao ni waislamu walipoanza kupambana na makundi ya wakristo.
Waislamu kutoka Afrika ya Kati ni miongoni mwa walioripotiwa kukimbia nchi hiyo ya Afrika ya Kati.
Umoja wa Afrika AU imetuma askari wapatao 4,000 nchini Jamuhuri ya Afrika ya Kati wakati Ufaransa ambayo iliwahi kuitawala nchi hiyo nayo imepeleka wanajeshi wapatao 1,600.
Inasadikiwa mamia ya raia wa Chad wanaoishi nchini Jamuhuri ya Afrika ya Kati wengi wao ni wale ambao familia zao ziliiishi nchini humo kwa vizazi kadhaa vilivyopita.
Wakristo wengi wanaishutumu serikali ya Chad ambayo wengi ya raia wake ni waislamu kwamba wamekuwa wakiwasaidia wapiganaji wa Seleka.
Siku ya Jumatano wanajeshi sita wa Chad waliopo kwenye kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani waliuawa kwa shambulizi lililofanywa na wapiganaji wa Kikristo wanaojulikana Anti Balaka katika mji mkuu wa Bangui.
Raia wa Chad waliokuwa wanaondoka katika mji wa Bangui siku ya jumamosi walikuwa wakilindwa na majeshi ya Ufaransa dhidi ya wapiganaji.
Tayari raia wa Chad wapatao 2,743 wameondoaka nchini Jamuhuri ya Afrika ya Kati katika wiki za hivi karibuni taarifa hizo ni kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji International Organisation for Migration (IOM).

Zoezi kunasua meli kwenye theluji

Meli ya Australia imo njiani kuelekea Mashariki wa Antarctica kwa ajili ya kukwamua meli ya wanasayansi iliyokwama kwenye theluji tangu siku ya jumanne.
Meli ya Shokaliskiy iliyonasa kwenye theluji
Awali juhudi za uokoaji zilifanywa na wavuja theluji wa Uchina na Ufaransa lakini walikwama kutokana na unene wa theluji.
Hata hivyo mwandishi wa habari wa BBC aliyepo kwenye meli ya utafiti ya Urusi anasema tayari theluji imeanza kupasuka na kuongeza matumaini ya meli hiyo iliyonasa kujikwamua yenyewe na kuanza kuondoka.
Wanasayansi wapatao sabini na nne, watalii na wafanyakazi wa meli wapo kwenye meli hiyo iliyokwama inayoitwa .
Meli hiyo imekuwa ikitumiwa na taasisi ya Australasian Antarctic Expedition kufuatilia njia mtafiti Douglas Mawson aliyesafiri kwenye njia hiyo karne iliyopita.
Shokalskiy imejaa chakula cha kutosha na hakuna hatari hii ni kwa mujibu wa timu ya uokoaji.
Pamoja na kunasa, wanasayansi wanaendelea na majaribio ya kisayansi, kupima nyuzi joto kuzunguka theluji iliyoanza kupasuka.
Mamlaka ya Usalama wa Majini ya Australia ambayo ndio inayoratibu uokoaji imesema kikosi cha uokoaji cha Aurora Australis kilitarajiwa kuwasili katika eneo meli hiyo iliponasa siku ya jumapili majira ya saa 9 kwa saa za Afrika Mashariki.
Mitambo mikubwa ya kukata theluji ina uwezo wa kukata theluji yenye unene wa mita 1.6 na uwezo wa kuzoa theluji ya ukuta wa mita tatu kuzunguka eneo la Shokalskiy.
Kama operesheni hiyo ya uokaji itashindikana itabidi helkopa zitumike kuwaokoa.

UN kutuma ndege za upelelezi Sudana K.

Umoja wa Mataifa nchini Sudan umesema kuwa utatumia ndege za upelelezi kujaribu kuhakikisha idadi ya vijana walioripotiwa kuandamana kwenda kwenye mji wa Bor.
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini
Serikali ya Sudan Kusini ilisema siku ya jumamosi kuwa kulikuwa na maelfu ya vijana ambao ni wafuasi wa kiongozi wa waasi Riek Machar
Vijana hao waliobeba silaha za jadi na fimbo inaelezwa hawana mafunzo yoyote ya kijeshi, Msemaji wa Umoja wa Mataifa ameiambia BBC.
Lakini msemaji wa waasi amesema kulikuwa na askari wa kawaida ambao walikuwa wakirejea serikalini. Msimamizi wa mazungumzo kutoka Afrika amewapa Bwana Machar na Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir hadi Decemba 31 wawe wameanza mazungumzo.
Karibu watu 1000 wamekufa katika mapigano yaliyochukua mwezi mmoja sasa, huku wengine 121,600 wanahofiwa kuyakimbia makazi yao.
Tayari maelfu ya raia wanatafuta hifadhi ya ukimbizi katika kambi za Umoja wa Mataifa huku wanajeshi zaidi wa kuongeza nguvu wa Umoja wa Mataifa wakiwa wamewasili nchini humo kwa ajili ya kuimarisha usalama wa raia.

Radi yauwa wanane Malawi

Watu wanane wamekufa nchini Malawi wakati radi ilipopiga kanisa katika mji mkuu, Lilongwe.
Soko mjini Lilongwe, Malawi
Walioshuhudia wanasema kulitokea mtafaruku katika kanisa la Sabato baada ya jengo la kanisa kupigwa na radi Jumamosi jioni.
Wakuu wa afya wanasema mtoto mmoja ni kati ya watu waliokufa.
Wameeleza kuwa watu 40 wengine wanatibiwa katika hospitali kuu.
Vyombo vya habari vya Malawi vinaripoti kuwa radi iliuwa watu watatu wengine katika matukio mbali-mbali tangu majira ya mvua kuanza mwezi uliopita.

Kwa heri 2013, najua umewatesa vilivyo Watanzania


                                                                                                            MCL
Na Ndyesu
Ninakamilisha wiki 51 nyingine za mwaka huu, miezi 12 kamili kwa kuwasiliana nawe kwa mara nyingine. 
Leo, ninafanya hivyo nikiwa mwenye furaha tele, nakutakia heri ya mwaka mpya, yaani 2014, mwaka  ambao panapo majaliwa tutauanza hapo keshokutwa.
Ninasema kwa wiki 51 kati ya 52 mwaka huu nimekuwa nawe bila kukosa. Ni wiki ambazo sikukosa kuwa nawe, ingawa kwa wiki moja sikuonekana.
Ninatambua vizuri wajibu wangu kwako kwani kwa wiki ile moja ambayo hukuwa nami, hakika ulinikosa.
Kwa bahati mbaya, sikupata nafasi ya kukuomba radhi msomaji wangu mtukufu kwa kukunyima uhondo ule wa siku zote ambao kwa zaidi ya miaka minne umeupata kupitia safu hii.
Kwa kipindi hiki cha karibu miaka minne huenda nimekukwaza kwa namna moja au nyingine, naomba unisamehe, kama ambavyo pia ninafanya hivyo kwako.
Kwa pamoja tunaukamilisha mwaka hapo kesho, lakini, ni mwaka ambao kama ilivyokuwa mingine iliyotangulia, tumeshuhudia mambo mengi yakiwamo yale ambayo hakika hayakuwa yenye kupendeza au hata kuvutia. Hata katika familia moja moja, jamii au hata kitaifa, tumepitia katika mambo mengi magumu ambayo siwezi kuyaorodhesha hapa chini.
Kikubwa, kama taifa tulifanikiwa katika moja, lile la kuendelea vyema na mchakato wa kuandika Katiba Mpya.
Nimeambiwa kuwa leo, mchakato huo unaingia hatua yake ya  pili kwa Rais Jakaya Kikwete kupokea rasimu ya pili.
Ninaamini kazi iliyofanywa kwa umakini, umahiri mkubwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba , chini ya Jaji Joseph Sinde Warioba na wenzake wengi ni ya kupongezwa. Hata hivyo, niitaje kazi ya tume hiyo,  nikigusia pia kifo cha mjumbe wake, Dk Edmund Sendongo Mvungi aliyefariki dunia miezi michache iliyopita na kuiacha kazi hiyo ikiwa bado jikoni.
Ninachukua nafasi hii kumwombea pumziko la milele, Dk Mvungi pamoja na Watanzania wengine wote ambao wamepoteza maisha yao, mwaka 2013 kwa sababu zozote zikiwamo za ukatili wetu, sisi binadamu.
Kwa wenzetu, wale ambao wamefariki dunia kwa ajali za aina mbalimbali  kama za barabarabani, angani, majini, kwa hakika ninawakumbuka, pia nawaombea pumziko la milele, nikiomba Mwenyezi Mungu awaangazie mwanga wa milele. Ninamkumbuka Padri Evarist Mushi wa Parokia ya Minara Miwili, Jimbo Katoliki la Zanzibar ambaye aliuawa kikatili kwa risasi, siku ya Jumapili, Februari 17.
Matukio haya ya ukatili  yalikuwa mengi, kama nilivyoeleza awali ni pamoja na kuvamiwa, kupigwa, kuumizwa kwa Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mtanzania linalomilikiwa na New Habari Corporation, Absalom Kibanda.
Kibanda, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania alivamiwa wakati akirejea nyumbani kwake, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, Machi 6, 2013 na kisha kuumizwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake  na hadi sasa ingawa amepata nafuu baada ya matibabu ya gharama kubwa kule Afrika Kusini, hatuambiwi sababu, chanzo na hata wahusika wa tukio hilo.
Kama vile haitoshi, Padri Anselmo Mwang’amba, pia kutoka Jimbo Katoliki la Zanzibar alivamiwa na kumwagiwa tindikali kama ilivyokuwa kwa katibu wa Mufti wa Zanzibar, Shehe Fadhil Soraga karibu na mwisho wa mwaka 2012.
Tukio hilo la Septemba linazidi kutia chachandu matukio hayo mabaya ya kikatili ambayo yameukumba mwaka ambao funguo zake zinawekwa kando, lakini pia unatukumbusha mengi yaliyoitia doa nchi yetu.
Tukio la kumwagiwa tindikali kwa wasichana wa Kizungu kule Zanzibar, hadi sasa halijawekwa wazi na vyombo vya dola iwe kule visiwani au Tanzania kwa jumla, ni aibu nyingine ambayo nchi yetu haiwezi kujivua.
Wasichana hao,Kirstie Trup na Katie Gee, wenye umri wa miaka 18 walikuwa visiwani humo kwa kazi ya kujitolea, walimwagiwa tindikali  Agosti wakati wakiwa matembezi eneo la Mji Mkongwe , Zanzibar.
Jambo la kushangaza ni kuwa tangu wakati ule mbali ya kuhudumiwa katika hospitali zetu, Mnazi Mmoja na Muhimbili, kisha kusafirishwa kwenda kwao, Uingereza walikofanyiwa upasuaji wa kurekebisha sura zao, hatuambiwi nani mhusika.
Nimesoma mahali wasichana hao wanamedhamiria kurudi Zanzibar kuendelea na kazi zao, wanailaumu serikali  yaani SMZ (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) au ile ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na pia huenda hata ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayosimamia vyombo vya dola likiwamo Jeshi la Polisi ambalo ndilo lenye dhamana ya kulinda raia na mali zao.
Tukio jingine n mfanyabiashara  wa Dar es Salaam, ambaye naye alimwagiwa tindikali na kuumizwa vibaya katika mlolongo wa matukio hayo mabaya yanayoupamba mwaka huu.
Tukio hili na jingine la Arusha kwa mfanyabiashara mwingine, pia yote yaliyotangulia limebaki siri  baina ya watendaji wake, polisi wanaochunguza na jamii inayosubiri kuona kinachoendelea .
Tumeambiwa kuwa mfanyabiashara huyo  na mmiliki wa maduka ya Home Shopping Centre, Said Mohammed Saad alimwagiwa tindikali  kwenye maeneo ya Msasani City Mall, saa 2 usiku ambako inadaiwa kuwa mhusika aliyekuwa  na pikipiki  alitoka mbio, eti juhudi za mlinzi kujaribu kumkamata zilikwamishwa na utelezi.
Hata hivyo, kama nilivyoeleza mwaka unaisha, lakini cha moto Watanzania walio wengi  tumepata.
Hali ya maisha yetu,  wengi imeendelea kuwa duni, ngumu, karibu kila kitu kimepanda bei, isipokuwa hewa ambayo Mwenyezi Mungu hugawa bure.
Mategemeo ya wengi kupata hali nzuri, maisha bora ambayo tuliahidiwa na Rais Kikwete wakati ule wa kampeni yake ya kuwania muhula wa pili wa uongozi wake, mwaka 2010 kwa jumla yamebakia ndoto za mchana.
Kisiasa, wananchi  tumeendelea kusikiliza ngonjera za viongozi wetu wakiwamo wabunge wakiwa Dodoma ambako hupigana vijembe, kejeli nyingi au  kelele lukuki ambazo hazina tija.
Kelele zao (wanasiasa) hazina mwisho ,hazielekei hata siku moja katika kuwafikisha kokote Watanzania hasa katika safari waendako, ile ya kuishi vizuri tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita.
Kama kidonda  chetu Watanzania kimetiwa chumvi na ndimu, maisha yetu, wakulima na wafugaji yamewekwa rehani na mapigano baina yetu ambayo yamezikumba wilaya na mikoa mingi nchini.
Uhasama umezidi, wengi wanaishi mtihili ya chui na paka, viongozi wetu wamekosa mbinu za kuimaliza mizozo hii, wameshindwa kuandaa mipango ya kutenga maeneo ya kudumu  ya mifugo na kilimo  bila bughudha.
Binafsi, nasema yote yanawezekana, endapo kuna dhamira hasa kwa uongozi wetu wa ngazi mbalimbali kujaribu kufanya hivyo. Kama nchi, tujaribu tuone, naamini tunaweza.

Katiba: Mwelekeo mpya kujulikana leo

Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakitia saini Rasimu ya Pili ya Katiba juzi. Rasimu hiyo itakabidhiwa leo kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais Ali Mohamed Shein, Karimjee, Dar es Salaam. Picha ya mtandao. 
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Swali la nini kilichomo katika Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya litajibiwa leo wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba itakapokabidhi rasimu hiyo kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.
Rasimu inayosubiriwa kwa hamu na wananchi wa kada zote itatolewa ikiwa imepita miezi saba tangu tume hiyo ilipotoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba ambayo ilijadiliwa na kuboreshwa katika Mabaraza ya Katiba yaliyoketi kuanzia Julai 12 mpaka Septemba 2, mwaka huu.
Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 3, 2012 kwa kukusanya maoni ya wananchi, iliandaa rasimu ya kwanza iliyotangazwa Juni 4, mwaka huu.
Hafla ya kukabidhi rasimu hiyo itafanyika leo saa 6.00 mchana katika Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na asasi mbalimbali.
Baada ya kukabidhi rasimu hiyo ya Katiba, Tume ya Mabadiliko ya Katiba itavunjwa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Warioba ndiye atakayesoma rasimu hiyo kwenye Bunge Maalumu la Katiba linalotazamiwa kuanza vikao vyake Februari, mwakani.
Alipoulizwa nini kilichoongezwa au kupunguzwa katika rasimu hiyo, Jaji Warioba alisema: “Siwezi kueleza kama kuna kilichoondolewa au kurekebishwa... kesho (leo), Watanzania watapata fursa ya kujua mapendekezo ya tume, wasubiri.”
Baadhi ya mambo yanayosubiriwa kwa hamu kujua kama yamefanyiwa marekebisho au la kwenye Rasimu Mpya ni pamoja na mfumo na muundo wa Muungano, umri wa kugombea urais, wabunge kutokana na mikoa, umri wa kugombea urais na mengine.
Serikali Tatu
Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupitia Rasimu ya Kwanza ilipendekeza kuundwa kwa Serikali Tatu na alipokuwa akizungumzia hilo wakati akitangaza Rasimu ya Kwanza, Jaji Warioba alisema uamuzi huo ulifikiwa kwa kuwa yalikuwa ni maoni ya wananchi walio wengi.
Hata hivyo, pendekezo hilo lilizua mjadala mkubwa kwani chama tawala, CCM, kilipinga na kuweka bayana kwamba kinataka muundo wa Muungano uendelee kuwa wa Serikali mbili.
Vyama vya upinzani kwa upande wake, viliunga mkono pendekezo hilo la muundo wa Serikali Tatu huku CUF kikienda mbali zaidi kwa kutaka Zanzibar ipewe mamlaka ya kuwa na dola kamili.
Katika Rasimu ya Kwanza ilipendekezwa mambo saba tu ndiyo yabakie kwenye mamlaka ya Muungano.
Mambo hayo ni pamoja na Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi na Usalama, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa na Ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.
Mambo hayo, ilipendekezwa na Tume hiyo kuwa chini ya wizara ambazo zitaongozwa na mawaziri wakazi ambao hawatatokana na wabunge kwani watatakiwa kuchaguliwa nje ya taasisi hiyo.
Kurejeshwa kwa jina la Tanganyika
Baada ya kutolewa kwa Rasimu ya Kwanza, mjadala mwingine ulioibuka hasa baada ya kupendekezwa kwa muundo wa Muungano kuwa wa Serikali Tatu ni hatua ya Tume kuendelea kutumia jina la Tanzania Bara.
Baadhi ya wadau walikosoa pendekezo hilo wakitaka jina la Tanganyika litajwe katika Katiba badala ya Tanzania Bara.
Katika Rasimu ya Kwanza, Tanzania Bara na Zanzibar zilihesabiwa kuwa washirika wa Muungano.
Ikiwa Serikali tatu zitarudishwa swali linakuja kama Tanzania Bara itatumia jina la Tanganyika ambalo ililitumia kuanzia mwaka 1961  hadi 1964 ilipoungana na Zanzibar.
Kufutwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu
Rasimu ya kwanza ilipendekezwa kufutwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu kwenye Serikali ya Muungano na badala yake kupendekeza kuwapo kwa Rais na Makamu wake.
Baadhi ya wadau walihoji juu ya usimamizi wa kazi za kila siku za Serikali jukumu ambalo kwa sasa lipo kwa Waziri Mkuu.
Umri wa kugombea urais
Suala hilo nalo lilizusha mjadala mkali wakati wa mchakato wa kukusanya maoni ya Katiba Mpya.
Mapendekezo ya Rasimu ya Kwanza yalitaka moja ya sifa za mgombea urais kuwa miaka 40 lakini baadhi ya wanasiasa, hasa vijana, wametaka umri huo ushushwe hadi miaka 35.
Wagombea binafsi
Jambo jingine lililopendekezwa katika Rasimu ya Kwanza ni kuwapo kwa mgombea binafsi kuanzia ubunge hadi urais.
Hilo halikuwa na mjadala mkubwa miongoni mwa wadau mbalimbali kutokana na ukweli kwamba ni jambo ambalo limekuwa likipigiwa kelele kwa muda mrefu na wananchi.
Muundo wa Bunge la Muungano
Rasimu ya Kwanza ilipendekeza kuwa wabunge watakuwa 75.
Kwa maana ya 50 kutoka Tanzania Bara, 20 kutoka Zanzibar na watano kutoka kundi maalumu ambao watateuliwa na Rais kwa ajili ya kuwatetea watu wenye ulemavu.
Kwa mujibu wa mapendekezo ya Rasimu ya Kwanza, wabunge wa kuchaguliwa watagombea kupitia mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Rasimu ya kwanza ilipendekeza kuwa kila mkoa utachagua mbunge mmoja wa kike na wa kiume ili kuleta uwiano na kupendekeza kufutwa kwa viti maalumu suala ambalo lilizua mjadala.
Haki za Binadamu
Moja ya mambo ambayo yaliibuka mjadala ni haki za binadamu. Katika Rasimu ya Kwanza, ilipendekezwa kuundwa kwa Tume ya Haki za Binadamu itakayokuwa na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wasiozidi saba.
Lakini wadau wengi waliotoa maoni yao walitaka sheria kandamizi 40 za Tume ya Nyalali zisiwepo katika Katiba Mpya.
Mambo mengine
Kuhusu madaraka ya Rais, Tume hiyo ilipendekeza katika Rasimu yake ya Kwanza kwamba yabaki kama yalivyo hasa kwa uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu, pia ashirikiane na taasisi na vyombo vingine katika uteuzi.
Katika Rasimu hiyo ya Kwanza, pia ilipendekezwa kusiwepo na uchaguzi mdogo, isipokuwa kama nafasi hiyo itaachwa na mgombea binafsi lakini kama ni wa kutoka katika chama cha siasa, ijazwe na mtu kutoka chama chake.
Kuhusu Tume ya Uchaguzi, Tume hiyo ilipendekeza katika Rasimu ya Kwanza kwamba jina la Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC), libadilishwe na iitwe Tume Huru ya Uchaguzi.
Rasimu hiyo, ilipendekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu (Supreme Court), majaji wa Mahakama ya Juu na Mahakama ya Rufani watateuliwa na Rais, baada ya kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.